• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:11 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Aina za wahusika

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Aina za wahusika

Na MARY WANGARI

Mhusika wa kidhanaishi

AINA hii ya mhusika huakisi sifa kadhaa zinazohusishwa na falsafa ya udhanaishi ambazo msingi wake ni kudadisi ukweli, furaha na hali ya kuweko maishani.

Mfano mzuri wa wahusika wa kidhanaishi ni katika kazi za kifasihi za mwandishi maarufu E. Kezilahabi ikiwemo ‘Nagona’ na ‘Mzingile’.

Katika riwaya ya Nagona, wahusika Paa na Mimi ni wanawakilisha kundi la wahusika wa kidhanaishi.

Wafula na Njogu (2007), wanasema kwamba mhusika anaweza kuangaliwa kama mtu binafsi na maisha yake.

Wataalam hao pia waliwaainisha wahusika katika vitengo mbalimbali ikiwemo: jaribosi, nguli, kivuli na wengineo.

Mhusika Nguli – aghalabu huwa mhusika mkuu mbaye husafiri kwa nia mahsusi. Safari hiyo aghalabu huanzia utotoni hadi anapofikia utu uzima.

Wakati mwingine, safari hiyo inaweza kuwa ya kikweli ambapo nguli hujizatiti kukisaka kitu fulani au kujisaka nafsi yake mwenyewe.

Aidha, huwa kuna mkinzani wa nguli ambaye hupambana na kuiharibu mipango ya nguli akijaribu kumwangamiza.

Mhusika huyu huwa mzinzi, mlafi na wakati mwingine huwa tajiri kama vile Mzoka katika riwaya ya Miradi Bubu ya Wazalendo.

Katika riwaya ya ‘Adili na Nduguze’, tunakumbana na mhusika Adili anayesafiri kwa ajili ya kufanya biashara. Katika safari hizo tunaonyeshwa ndugu zake Mwivu na Hasidi wanavyoamua kumtupa baharini kutokana na wivu na choyo. Hatimaye tunaona jinsi anavyookolewa na mtoto wa Mfalme wa Kijini, Huria.

Uhakiki wa wahusika una umuhimu mkubwa na manufaa kwa wanafasihi kuwa kuwa huwawezesha kutumia vigezo hivyo kubaini aina ya wahusika wanaotumiwa na mwandishi katika kazi anuai za fasihi.

 

Wasiliana na mwandishi ukitumia baruapepe: [email protected]

Marejeo

Njogu, K. na Chimerra, R. (1999). Ufundishaji wa Fasishi: Nadharia na mbinu. Nairobi- Jomo Kenyatta Foundation.

Syambo, K. Mazrui (1992). Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African Educational Publishers Ltd

You can share this post!

Kamati ya kitaifa ya Olimpiki kuwapa wanariadha wastaafu...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mbinu za usawiri wa wahusika

adminleo