UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana ya miiko na utafiti kuhusu utamaduni wa Waswahili
Na MARY WANGARI
BAADHI ya miiko katika jamii ya Waswahili na Waafrika kwa jumla ni kama vile: kula gizani ni kula na shetani huweza kutumika kukataza tabia ya uchoyo.
Kunywa maji msalani mtu huwa mwongo; huweza kutumika kuhakikisha usafi na nidhamu.
Bundi akilia juu ya nyumba anatangaza kifo na kadhalika.
Kwa mujibu wa Mbaabu, Itikadi zina mafunzo mengi yanayostahili kuhifadhiwa na kuzingatiwa.
Kufikia sasa, sehemu kubwa ya utafiti kuhusu utamaduni wa Kiswahili, imejumuishwa na tasnifu ya mwanafalsafa Mwalimu Sengo kuhusu Sanaajadiiya ya Visiwani.
Utafiti kuhusu utamaduni wa Waswahili
Katika tasnifu hii, mwandishi wake alivitalii visiwa vya Pemba na Zanzibar kwa utafiti wa kina na kuibuka na hoja za kuueleza utamaduni wa Waswahili wa Visiwani kwa kuheshimu utata uliosababishwa na Bahari ya Hindi.
Aidha, ni muhimu kuelewa kuwa Waswahili wenyewe wanatofautiana na kuchanganyikana miongoni mwao kupitia sifa mbalimbali kuanzia maumbile, historia, asili, matukio, itikadi, imani na kadhalika.
Baadhi ya mambo yanayowaleta pamoja Waswahili wote kwa jumla ni pamoja na Bahari ya Hindi, historia ndefu ya Uislamu na lugha ya Kiswahili.
Mambo hayo ni nguzo kuu muhimu zinazowafanya Waswahili kujihisi kitu kimoja au ukipenda jamii moja kilugha, kiutamaduni na kihisia.
Isitoshe, ni vyema kuzingatia kuwa Uafrika asilia umepewa nafasi ya mwanzo katika haki na hadhi ya Waswahili.
Kwa mantiki hii, suala la ugozi halipaswi kutazamwa kisiasa tu kwa kuwa kimaumbile, watu huwa na rangi mbalimbali ya ngozi ili kuwawezesha kutambuana na kuelewana kirahisi katika kuendesha shughuli za kila siku maishani.
Kwa mujibu wa mtafiti wa tasnifu ya Sanaajadiiya ya Visiwani, utafiti huo haukujikita tu katika kujaribu au kugeza kutoa jawabu za mwisho na za pekee kuhusu masuala ya utatanishi wa Bahari ya Hindi na Sanaajadiiya ya Kiswahili. Hata hivyo, utafiti huo pia ulidhamiria kupendekeza hoja za kurahisisha tafiti za siku za usoni kuhusu utamaduni kwa jumla.
Marejeo
Nurse D. na Spear Th. (1985). The Swahili: Reconstructing the History and Language of an African Society, 800-1500. Philadelphia.
Sengo T.S.Y. (1985). The Indian Ocean Complex and the Kiswahili folklore:The case of Zanzibarian Tale-Performance. Unpublished Ph.D thesis. Khartoum University.
Shariff I.N. (1988). Tungo Zetu. Trenton: The Red Sea Press, Inc.