• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Fasiri mbalimbali za Fasihi Simulizi

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Fasiri mbalimbali za Fasihi Simulizi

Na ALEX NGURE

FASIHI ni moja, lakini husemekana ni za aina mbili; fasihi andishi na fasihi simulizi.

Matawi haya mawili yanatofautiana kutokana na uwasilishaji; yaani jinsi taarifa zinavyohifadhiwa na hatimaye kuifikia jamii (hadhira).

Kwanza, ni fasihi andishi ambayo huhifadhiwa kwa maandishi na kuwasilishwa kwa maandishi. Hii huwa ni matukio, habari ndefu au fupi za kubuni ambazo huandikwa.

Fasihi simulizi kwa upande wake huwasilishwa na kuenezwa kwa njia ya mdomo (mapokeo ya mdomo) kama vile kughani na kusimuliana. Hata hivyo, siku hizi fasihi simulizi imeweza kuhifadhiwa katika maandishi na kanda hasa kwa ajili ya kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Makala haya yataangalia maana ya fasihi simulizi kwa kuchukua mawazo ya baadhi ya wataalamu mbalimbali.

Kirumbi (1975) anasema kwamba, fasihi simulizi ni masimulizi tunayoyapokea mdomo kwa mdomo, si masimulizi yaliyoandikwa tangu awali. Kwa njia hii basi,tunaona kuwa katika fasihi simulizi kuna utumiaji wa ulumbi (ufundi wa kusema).

Matteru (1983) anafafanua kuwa, fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo kwa kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa na wasikilizaji na watumiaji wake. Aidha,Matteru anaendelea kusema kwamba, fasihi simulizi ikiwa ni sanaa itumiayo maneno katika kutoa dhana fulani, hutegemea sana nyenzo mbalimbali za kuonekana na kusikika zitumiwazo na binadamu katika kujieleza.

Msokile (1992) anafafaua kwamba, fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha. Kazi hii huhifadhiwa kichwani na kusambazwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Anamalizia kwa kusema kwamba, fasihi simulizi imekuwa ikirithishwa kutoka kizazi hadi kizazi.

Mlacha (1995) anatueleza kwamba, fasihi simulizi ni uwanja katika maisha ya jamii ambao huchangia sana katika kuiendeleza na kuidumisha historia ya jamii husika. Katika kufafanua zaidi kuhusu fasihi simulizi, Mlacha anasema kuwa ‘fasihi simulizi huchangia katika kuelimisha jamii kuhusu asili yake; chanzo na maendeleo ya utamaduni wake na maisha ya jamii hiyo kuanzia zamani’.

Wamitila (2003) anatueleza kwamba, fasihi simulizi ni dhana inayotumika kurejelea kazi ambazo kimsingi hupokezanwa kwa njia ya masimulizi au kwa mdomo.

Wamitila kwa hakika hayuko mbali sana na msingi mkuu wa fasihi simulizi uliosababisha kuwepo kwa tawi hili la fasihi.

Anatueleza kuwa tawi hili la fasihi linatumiwa katika jamii kama njia ya kupashana maarifa yanayohusu utamaduni fulani, historia ya wanajamii, matamanio yao na mtazamo wao.

Kwa mantiki hiyo ya Wamitila, tunaweza kujumuisha kuwa fashi simulizi ndicho chombo muhimu cha jamii.

Prof Kimani Njogu (2006), anatueleza kuwa fasihi simulizi ina ubunifu na uhai wa kipekee wenye kutoa fursa njema ya kuibua nadharia za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Prof Kimani Njogu anaifananisha aina hii ya fasihi na uti wa mgongo wa maendeleo ya binadamu; kwani ndani yake kuna masimulizi, maigizo, tathmini za mazingira na mahusiano ya kijamii.

Kwa mawazo ya wataalamu hawa, tunaweza kuhitimisha kuwa fasihi simulizi ni sanaa inayotumia lugha ya mazungumzo ya ana kwa ana katika kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira husika. Hii ni sanaa ambayo ujumbe wake upo katika mfumo mzima wa pande mbili za mawasiliano.

Mawasiliano ya ana kwa ana

Hii ikimaanisha kuwepo mawasiliano ya ana kwa ana kati ya fanani, yaani mtu anayerithisha (msimuliaji) na hadhira, yaani mtu anayerithishwa (msimuliwaji).

Kwa njia hii, fasihi simulizi hushirikisha au huwafikia watu wengi na mawazo ambayo jamii iliyakubali, imeyakubali, inaendelea kuyakubali yatokeapo na inayapitisha au inayakabidhi kwa jamii husika na kuendelezwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo.

Kwa hali hiyo basi, kwa kuwa taarifa zinazopatikana zimepitishwa kwa mdomo, upo uwezekano wa utata, upotoshwaji na upoteaji wa taarifa muhimu za kale ambazo kama zingeliandikwa, zingedhihirisha ukweli wa mambo yalivyokuwa hasa.

Haiyumkini mapokeo ya fasihi simulizi yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuiunda, kuirekebisha, kuifundisha na kuiboresha jamii. Fasihi simulizi ndiyo fasihi ya awali.

Aina hii ya fasihi imeanza wakati binadamu alipoanza kutumia lugha kama mojawapo ya vyombo vya mawasiliano. Tangu hapo, ndipo mwanadamu alipoanza kuimba, kutumia methali, vitendawili, nahau na kadhalika.

 

[email protected]

You can share this post!

Ruto arejea nyumbani kuzima moto

Baadhi ya wanachama Knut wazidi kushinikiza Sossion ajiuzulu

adminleo