Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Hatua za mwanzo za usanifishaji Kiswahili

August 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

KIPINDI cha kuanzia mwaka 1930 hadi mwaka 1938 kilikuwa muhimu sana kwa historia ya usanifishaji wa Kiswahili.

Katika kipindi hicho, msingi imara sana uliwekwa na kukaanzishwa kiwango cha juu cha kufanya kazi.

Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilihitaji msingi imara, hivyo ili kuiwezesha kufanya kazi wakati wa vita.

Sifa nyingi za mafanikio ya Kamati inatokana na kazi nyingi na za kuchosha zilizofanywa na Frederick Johnson, aliyekuwa katibu wa kwanza wa kamati hiyo.

Mbali na kutafsiri vitabu vingi, Johnson alifanya kazi kubwa ya kutunga kamusi za Kiswahili-Kiswahili, Kiswahili-Kiingereza na Kiingereza-Kiswahili.

Serikali zote za Afrika Mashariki, Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar ziliunga mkono kamati hii kwa kuwa zote ziliwakilishwa katika kamati hiyo.

Sera ya lugha za nchi zote zilikisaidia Kiswahili sana katika maenezi yake.

Wafanyakazi Wazungu wa nchi hizi zote ilibidi wajifunze Kiswahili na wafaulu mitihani.

Walioshindwa kufaulu mitihani hiyo walibaki kuwa wafanyakazi wa muda wala si wa kudumu.

Kwa hivyo, iliwabidi maafisa wa serikali Wazungu wajifunze Kiswahili.

Ili kupandishwa cheo kazini, iliwabidi wafaulu mitihani ya juu ya Kiswahili.

Serikali hii ilikipa Kiswahili hadhi. Mitihani hiyo ya Kiswahili ilisababisha mahitaji ya kuchapisha vitabu vitakavyowasaidia maafisa hao kujitayarisha kufanya mitihani hiyo.

Pia, vitabu hivyo vilinunuliwa kwa wingi kwa kuwa maafisa hao walitamani kupita mitihani ili wahifadhi kazi zao.

Kwa hivyo, mitihani hiyo ilisaidia kukikuza na kukieneza Kiswahili, pamoja na kuongeza idadi ya vitabu vilivyochapishwa wakati huo.

Swali lifuatalo ni: Sera ya Lugha ilikuwa vipi katika kila nchi?

Nchini Kenya, kulingana na barua ya Katibu Mkuu namba 40 ya Juni 1, 1931, mbali na mitihani ya Wazungu waliokuwa wafanyakazi wa Jeshi la King’s African Rifles ambayo ilikuwa na maagizo yake tofauti, maafisa wengine wote Wazungu waliokuwa wakifanya kazi katika Koloni iliwabidi wafanye mitihani ifuatayo ambayo ilikuwa ya lazima.

Mtihani uliotangulia ulikuwa mtihani wa kwanza wa mahojiano kwa Kiswahili ambao ilibidi ufanywe kabla ya mwaka mmoja kwisha tangu kuajiriwa kwa kazi isiyokuwa ya kibarua.

Iwapo afisa aliyehusika hangefaulu mtihani huo, ilimaanisha kwamba hangepata nyongeza ya mshahara ya kila mwaka.

Zaidi ya hayo, hilo pia lingempelekea kushushwa cheo na kuwa mfanyakazi.

Kiwango cha Kiswahili kilichohitajika ni cha kumwezesha afisa huyo kufanya kazi kwa kutumia Kiswahili pasipo mahitaji ya mkalimani.

Mtihani wa pili ulikuwa wa Kiswahili sanifu kiwango cha chini.

Mtihani huu ulitahiniwa baada ya mwaka mmoja kwisha na kabla ya miaka miwili na nusu kwisha tangu afisa aajiriwe.

Wale ambao hawakupita mtihani huo walichukuliwa hatua, sawa na wale ambao hawakupita mtihani wa kwanza.

Ili mtu aweze kupita mtihani huo, ilibidi awe amefikia kiwango cha kuelewa na kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha na ujasiri.

Mtihani wa Kiswahili sanifu kiwango cha juu ndio uliokuwa wa tatu na wa juu sana kati ya hiyo mitihani ya lazima.

Mtihani huo ulikuwa wa mahojiano pamoja na wa kuandika.

Ulikuwa wa Wazungu wenye vyeo vikubwa na ulifanywa baada miaka mitatu na kabla ya miaka kumi haijaisha tangu waajiriwe.

Kukosa kupita mtihani huo kwa muda uliowekwa kuliathiri cheo cha afisa aliyehusika na kumaanisha kwamba hangeendelea kupewa nyongeza za mshahara.

Kuijua sarufi

Ili mtu aweze kupita mtihani huo, ilibidi ajue vizuri sarufi ya Kiswahili.

Maagizo yaliyoihusu Uganda yanapatikana katika tangazo la barua Namba 40 ya Desemba 29, 1928, kutoka ofisi ya Katibu Mkuu.

Maagizo hayo ni sawa na ya Kenya, isipokuwa kuna tofauti chache tutatazorejelea.

Kuhusu mtihani wa kiwango cha kwanza wa mahojiano, maafisa waliokuwa wakifanya kazi Buganda, waliruhusiwa kufanya mtihani wa kiwango hicho, lakini maafisa waliokuwa wakifanya kazi katika sehemu nyingine za Uganda, ilibidi wafanye mtihani wa Kiswahili.

Maafisa waliokuwa wakifanya kazi katika tawala za mikoa na Idara ya Elimu ilibidi wafaulu katika mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha chini kabla hawajathibitisha kazini.

Hizo ndizo zilizokuwa hatua za kwanza ambazo zilikipa Kiswahili msingi wa ukuaji mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.