• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Istilahi muhimu kwa anayejifunza lugha

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Istilahi muhimu kwa anayejifunza lugha

Na MARY WANGARI

Dosari

DHANA ya uchambuzi wa dosari inarejelea njia ya kuainisha, kupambanua na kufafanua dosari mbalimbali za wajifunzaji wa lugha ya kigeni au lugha ya pili.

Mwasisi wa suala la uchambuzi wa dosari ni Corder (1967), anayesema ni ukiukwaji wa kanuni na taratibu za lugha lengwa.

Katika uchambuzi wa dosari, wachanganuzi huangazia mambo makuu manne kama yafuatayo:

Jinsi anayejifunza anavyoielewa lugha ya kigeni anayojifunza.

Jinsi anayejifunza anavyojifunza lugha ya kigeni au mbinu anazotumia.

Matatizo anayokabiliana nayo wakati anajifunza lugha ya kigeni.

Kung’amua mchakato au kutambua michakato inayotumiwa katika kujifunza lugha ya kigeni.

 

Dhima na nafasi ya dosari kwa wanaojifunza lugha ya pili

Dosari zinazofanywa na wanafunzi wanaojifunza lugha ya kigeni hutumiwa kama kioo kinachoakisi hali halisi iliyofikiwa na wajipatiaji wa lugha ya pili.

Dosari hizi humpatia mwalimu nafasi ya kutathimini jitihada zilizofikiwa na wanafunzi wake kwa minajili ya kuboresha au kuendeleza mbinu za kujifunza lugha na humsaidia mwalimu kubadilisha vifaa anavyotumia katika ufundishaji.

Kwa ujumla, umuhimu wa dosari unaangaliwa katika namna nne kuu:

Kwa upande wa mwalimu, huonyesha jitihada zilizofikiwa na wanafunzi na kusaidia kuboresha.

Kwa watafiti, huonyesha jinsi lugha inavyopatikana au inavyoamiliwa.

Kwa mwanafunzi, humsaidia mwanafunzi kujua ruwaza (pattern) ya maendeleo ya mwanafunzi alipofikia.

Kwa waandalizi wa mitalaa, huwasaidia kuboresha uandaaji wa vitabu na machapisho mbalimbali kwa kujifunza.

Aina za dosari

Aina hizi za dosari zimeainishwa kutokana na mbinu wanazotumia wanafunzi kujifunza lugha.

Dosari majumui/majumuisho

Hizi ni dosari ambazo mwanafunzi hutumia kanuni ya jumla ya lugha ya kwanza na kuitumia katika lugha ya pili. Hii inasabisha kukiuka matumizi ya lugha lengwa. Kwa mfano, katika lugha ya Kiingereza vitenzi vingi huongeza “ed” mwanafunzi wa Kiswahili na Kiingereza anaweza kupata shida kwani anaweza kuwa anaongeza ed katika kila kitenzi jambo ambalo sio sahihi.

Uepukaji/avoidance

Huu ni ule utaratibu wa anayejifunza lugha ya kigeni kujaribu kuepuka matumizi ya kanuni, maumbo au miundo fulani ya lugha. Kwa mfano, mwanafunzi anapojaribu kuepuka matumizi ya neno fulani atajaribu kuliepuka hilo neno na kutumia neno lingine; jambo ambalo litasababisha makosa. Hata hivyo, si rahisi kujua kama mtu fulani amekwepa matumizi ya neno fulani.

Urahisishaji

Mwanafunzi anapoamua kurahisisha muundo wa lugha fulani hujikuta katika dosari.

Uhawilishaji

Dhana hii inahusu uhamishaji wa miundo na kaida za lugha ya kwanza kwenda lugha ya pili. Miundo hii inapohamishwa basi hukiuka miundo ya lugha ya pili. Kwa mfano baadhi ya jamii ya hukiuka sana kanuni za Kiswahili. Mfano, baadhi ya watu hawawezi kusema ‘njoo’ bali watasema “ndoo” pia. Wengine badala ya kusema ‘kuja’ watasema ‘kuya’.

Utumizi ziada/over use

Huku ni kuongeza matumizi yasiyohitajika katika utumizi wa lugha

 

[email protected]

Marejeo

Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili in Teacher Training Colleges in Tanzania”. Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

Mtembezi, I. J. (1997). “Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia”. Dar es Salaam: BAKITA.

Mulokozi, M. M. (1991). “English versus Kiswahili in Tanzania’s Secondary Education”. Swahili Studie Ghent

You can share this post!

Ratiba ya Ligi Kuu ya Kenya msimu 2019-2020 yatangazwa

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Misingi ya uainishaji wa dosari

adminleo