• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:01 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Jazanda, chuku na maswali balagha

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Jazanda, chuku na maswali balagha

Na MARY WANGARI

JAZANDA (SYMBOLISIM)

Kwa mujibu wa Mbatia (2000), jazanda ni kunga ya utunzi ambapo lugha inatumia kusawiri picha fulani kutokana na maelezo yanayotumia maneno teule au tamathali za usemi.

Kwa njia hii mtunzi anamwezesha msomaji kuona, kuhisi kitu kinachoelezwa. Kwa ufupi, jazanda inahusisha hali ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja bila kutumia viunganishi.

CHUKU (HYPERBOLE)

Chuku ni hali ambayo sifa fulani hukuzwa kupita kiasi kwa mujibu wa Wamitila (2003).

Kwa upande wake Mbatia (2000), anafafanua chuku kama matumizi ya lugha ili kutilia chumvi kitu au hali fulani aghalabu kwa madhumuni ya kusisitiza.

Tamathali hii hutumika kuikuza sifa fulani kupita mipaka.

Lengo kuu la kutumia chuku ni kulifanya jambo au kitu kionekane kwa udhahiri zaidi.

Chuku pia inaweza kufafanuliwa kama hali ya kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani au kusifia kitu. Kutilia Chumvi.

MASWALI YA BALAGHA (RHETORICAL QUESTIONS)

Kwa mujibu wa Msokile (1993), haya ni matumizi ya maswali ambayo majibu yake kwa kawaida yanakuwa yameeleweka na hayahitaji kujibiwa. Ni maswali yanayoulizwa na msimulizi au mhusika ambayo hayahitaji jibu.

Kwa mujibu wa Thornborrow na Wareign (1998), neno ukiushi katika lugha lilitumika kwa mara ya kwanza na mwanaisimu wa shule ya Prague kwa jina Mukarowsky (1982), kueleza namna lugha ya kifasihi inaweza kutofautiana na matumizi ya kawaida ya lugha.

Neno hili ukiushi linatokana na neno kiuka linalomaanisha fanya isivyostahili, vunja sheria au fanya makosa. Naye Shake (1991), anahoji kwamba maingiliano yoyote yanayoathiri lugha kimuundo, kisarufi na hata kimsamiati ambayo yanazivunja sheria za lugha hiyo ni ukiushi wa kimatumizi.

Kwa upande wake Mbatia (2000), anasema kuwa ukiushi ni uvunjaji wa kimakusudi wa kaida za matumizi lugha ili kubuni njia mpya za kujieleza . Hii inamaanisha kuwa msanii anatumia mbinu hii ya ukiushi kuzivunja sheria za matumizi ya lugha ili kupata malengo yake katika kazi ya kifasihi.

Katika ukiushi kanuni za lugha sanifu zinaweza kukiukwa ama kimaksudi au bila kujua. Kutokana na umilisi wa lugha alio nao mwanajamii anaweza kuyatambua makosa ya kisarufi ili kubainisha ukiushi katika matumizi ya lugha.

 

[email protected]

Marejeo

Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili niTeacher Training Colleges in Tanzania”. Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

Mtembezi, I. J. (1997). Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia. Dar es Salaam

BAKITA. Mulokozi, M. M. (1991). English versus Kiswahili in Tanzania’s Secondary Education. Swahili Studie Ghent

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana ya tamathali za usemi...

Vitambulisho hukosesha maelfu mikopo ya Helb

adminleo