• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Jinsi ya kushughulikia dosari za wanafunzi katika ufundishaji wa lugha ya pili

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Jinsi ya kushughulikia dosari za wanafunzi katika ufundishaji wa lugha ya pili

Na MARY WANGARI

KATIKA ufundishaji wa lugha ya kigeni au ukipenda lugha ya pili, mkufunzi atakumbana na matatizo tofauti kulingana na wanagenzi wake.

Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kwamba kila mwanafunzi wa lugha ya pili huwa ana dosari katika kujifunza lugha ya pili.

Ni jambo la msingi kushughulikia dosari za wanafunzi lakini zingatia ni wakati gani unaopaswa kushughulikia dosari hizo. Hii ni kulingana na muktadha wa darasa, aina ya wanafunzi, haiba yao, mihemko, aina ya dosari, umri na kadhalika.

Iwapo itawezekana, dosari hizo zinapaswa kushughulikiwa ili kuhakikisha hazitajirudia.

Baadhi ya wataalamu wanapendekeza kushughulikiwa kwa dosari hizi.

Mfano ni kama vile kina Krashen na Terrell (1983), wanaosema kuwa mwanafunzi aachwe mwenyewe atazidi kugundua dosari hizo na atazishughulikia mwenyewe.

Kwa upande wake Kathleen Bailey (1985), anapendekeza mambo saba  yafuatayo:

Puuza dosari hizo.

Dosari zishughulikiwe papo kwa papo.

Kuhusisha wengine katika kurekebisha dosari hizo. Kwa mfano, miongoni mwa wanafunzi hao hao unaweza kuhusisha na wakakosoana wenyewe.

Kuhusisha wanafunzi mahususi hasa kumtumia mwanafunzi wa karibu na mwenzake kumsahihisha akikosea.

Kumshajiisha anayekosea “unaweza kufikiri zaidi juu ya hilo?”

Kuwaruhusu wanafunzi wengine kutoa tathmini.

Kumpa nafasi ya kujaribu tena na tena mfanyaji wa dosari baada ya vitendo fulani kufanyika ndani ya darasa.

 

Katika harakati za kushughulikia dosari miongoni mwa wanafunzi, ni muhimu kutilia maanani vipengele vifuatavyo:

Ni sharti usahihi na uhalali wa dosari uwe umedhihirika.

Sehemu na mahali dosari imefanyika iwe imebainishwa wazi wazi. Mfano kama ni kwenye neno, tungo na kadhalika.

Nafasi ya kurudia na kujirekebisha kwa mfanyaji dosari iwe imetolewa

Mifano mbalimbali ya dosari na usahihi wa semi uwe umetolewa na kuonyeshwa kwa uwazi

Aina ya dosari iwe imeonyeshwa. Kwa mfano, kama ni dosari ya kimpangilio, kimatamshi na kadhalika.

Marekebisho yawe yamefanywa kwa mifano anuwai

Mhusika awe amesifiwa au kama ameepuka hizo dosari.

 

[email protected]

You can share this post!

Kizaazaa pacha wakitibua jaribio la kuwatenganisha

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mambo yanayoathiri mchakato wa...

adminleo