UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kukua na kuenea kwa Kiswahili nchini Tanzania baada ya uhuru
Na ALEX NGURE
NILIPOZURU Dar Tanzania mwaka 2018 niligundua kwamba Tanzania imeonekana kukipatia Kiswahili hadhi na heshima hata kabla ya kujinyakulia uhuru.
Kwa mfano, chama cha TANU kilipoundwa mwaka 1954 kilikitambua Kiswahili kama lugha ya kupigania uhuru.
Baada ya uhuru,watawala Waafrika waligundua kuwa lugha ni kipengele muhimu katika utamaduni wa taifa.
Swali lililowakabili viongazi hawa lilikuwa: ni ipi kati ya lugha zaidi ya mia moja za kikabila ingefaa?
Lakini tayari palikuwa na Kiswahili ambacho hakikuwa lugha ya kabila lolote lile nchini Tanzania.Isitoshe, lugha hii ilikuwa imesambaa kote nchini.
Viongozi hawa waliona wazi kuwa, bila shaka Kiswahili kingeondoa matabaka yaliyoibuka baada ya uhuru na kujenga umoja halisi nchini.
Kufikia sura hii mpya ya uhuru, wananchi walikuwa wamegawanyika kwa vikundi viwili: Kimoja kilikuwa cha walioelimika na waliowahi kukitumia Kiingereza kwa urahisi sana.
Kundi la pili lilikuwa la wasioelimika na waliokuwa wanakijua Kiswahili. Kundi hili la kwanza lilijumuisha limbukeni wachache walioachiwa hatamu za uongozi na wakoloni, ilhali wale wa kundi la pili hawakupewa nafasi yoyote ya kutawala.Yafuatayo ni baadhi ya mambo yaliyochangia kukua na kuenea kwa Kiswahili baada ya uhuru:
i) Kuteuliwa kwa Kiswahili kuwa lugha ya taifa:Kutokana na hatua hiyo mwezi Septemba 1962, iliamuliwa kuwa Kiswahili kitumike katika Bunge na katika shughuli zote za kiserikali. Katika kutekeleza azma hiyo, Rais wa kwanza wa Tanganyika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza kwa lugha ya Kiswahili na hatimaye Kiswahili kikapewa nafasi ya pekee katika mipango mbalimbali ya kiserikali.
ii) Kutumika katika kutolea elimu: Mwaka 1965 Kiswahili kilifanywa kuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi.Wizara ya elimu ilihimiza utungaji wa vitabu vya Kiswahili vyenye kuzingatia siasa na utamaduni wa Watanzania. Hivyo, vitabu kama vile ‘Mashimo ya Mfalme Suleiman’, ‘Hadithi za Allan Quarterman’, ‘Hekaya za Abunuwasi na Hadithi Nyingine’, Mazungumzo ya ‘Alfu Lela Ulela’ havikutumika tena shuleni, kwani havikuzingatia mazingira halisi ya jamii ya wanafunzi wa Kitanzania. Vilevile, Kiswahili kilifundishwa kama somo kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha sita.
Mwaka 1970, Kiswahili kilianza kufundishwa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam.
iii) Kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Taifa(BAKITA): Baraza hili liliundwa kwa sheria ya Bunge ya mwaka 1967. Baraza hilo lilipewa kazi ya kuratibu shughuli zote za ukuzaji na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili kote nchini.
iv) Kuundwa kwa asasi za kueneza na kukuza Kiswahili: Aidha, serikali iliamua kuiundia lugha hii asasi ambazo zingefanya kazi ya kujenga, kuendeleza na kueneza Kiswahili. Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki iliyoundwa enzi ya ukoloni ilipandishwa hadhi na kufanywa Taasisi ya Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili, ikiwa ni mojawapo ya asasi za utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge ya mwaka 1970. Serikali pia ilianzisha Idara ya Kiswahili ikiwa ni mojawapo ya idara za Chuo Kikuu hicho. Idara hiyo ikapewa dhima ya kufundisha lugha hii katika kiwango cha Chuo Kikuu kwa kutumia lugha yenyewe kama lugha ya kufundishia.
v) Vyombo vya habari: Vyombo vya habari hasa magazeti, redio, na televisheni vimetekeleza wajibu muhimu sana katika kueneza lugha ya Kiswahili nchini Tanzania. Kuna magazeti mengi sana yanayotolewa kila siku, kila wiki, na kadhalika. Baadhi ya magazeti hayo ni ya serikali; ya mashirika ya kidini; ya watu binafsi; vyama vya siasa, nMagazeti hayo ambayo huandikwa kwa lugha ya Kiswahili,hujadili baadhi ya vipengele vinavyohusu lugha ya Kiswahili kama vile Isimu, Fasihi, Ushairi,licha ya kuandika makala mbalimbali yenye kuelimisha jamii.
Kwa upande wa radio, kunazo stesheni nyingi kama vile: TBC, Radio One, Radio Tumaini, Radio Free Afrika, Wapo Radio Radio hizo hutoa habari zake kwa lugha ya Kiswahili, hivyo husaidia katika kueneza Kiswahili nchini Tanzania.Televisheni nazo zinachangia kuenea kwa Kiswahili nchini. Televisheni hizo ni: ITV, TBC,Star TV, CTN, DTV,Channel Five, Channel Ten, Capital TV, TVZ na kadhalika. Hizi zote hutoa habari zake kwa lugha ya Kiswahili na kwa kufanya hivyo, husaidia kueneza Kiswahili.
vi) Dini: Dini zote mbili –Ukristo na Uislamu huendesha mahubiri yake kwa lugha ya Kiswahili; jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kukikuza na kukieneza Kiswahili nchini Tanzania tangu enzi za uhuru hadi sasa.
vii) Biashara: Misafara ya biashara nchini na hata nje ya Tanzania husaidia sana kukieneza Kiswahili.
viii) Kampeni za kisiasa:Kampeni za kisiasa tangu zile za vyama vilivyopigania uhuru hadi sasa; mfumo wa chama kimoja; Azimio la Arusha; kampeni za mfumo wa vyama vingi(mageuzi) na kampeni za chaguzi mbalimbali zimesaidia sana katika kueneza Kiswahili nchini Tanzania kwa sababu hadi sasa hutumia lugha ya Kiswahili.
x) Utawala: Shughuli zote za utawala nchini Tanzania kama vile ofisini, bungeni, mahakamani, shuleni, n.k.hutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano.
Baruapepe ya mwandishi: [email protected]