Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Lafudhi katika lugha ya Kiswahili

April 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

HAYA ni matamshi  ya mzungumzaji yanayojitokeza kutokana na athari za lugha yake ya kwanza; lugha inayotumika katika mazingira anamoishi au maumbile katika ala za sauti.

Aidha, tunaweza kufafanua lafudhi kuwa ni upekee unaojitokeza kwa mtu binafsi na huleta tofauti baina ya wasemaji au jamii.

Lugha ishara

Hii ni lugha ya mawasiliano inayotumia ishara badala ya sauti na maneno.

Lahaja (Dialect)

Hii ni tofauti katika matamshi, maumbo na matumizi ya maneno zitokanazo na tofauti katika maeneo mbalimbali kwa lugha yenye asili moja.

Lahaja inaposanifishwa hupata hadhi ya kuwa lugha.

Hakuna makubaliano kamili kuhusu idadi ya lahaja za Kiswahili na mipaka yake. Hii ni kwa sababu uchunguzi kamili haujafanywa.

Asili ya lahaja tofauti ndogondogo katika lugha hutegemea maeneo mbaimbali na hutokea katika vipengele vifuatavyo:

  1. Kutawanyika kwa watu wanaotumia lugha moja, ambao huenda kuishi maeneo mbalimbali ambako mazingira ni tofauti.
  2. Kuingiliana na kuoana kwa watu, na hivyo kuathiri lugha kwa namna fulani.
  3. Uhusiano baina ya watumiaji wa lugha kama vile wa biashara.
  4. Dini, mathalani Uislamu na Ukristo, huweza kusababisha kuzuka kwa lahaja.
  5. Elimu husababisha kuzuka kwa lahaja ambapo aina Fulani ya lugha kama vile Kiswahili sanifu hutumiwa katika mafunzo.
  6. Utengano kijiografia. Tofauti za kimasafa huweza kusababisha kuzuka kwa lahaja.
  7. Lahaja maalumu hutokea pale lugha inaposanifishwa kwa matumizi rasmi, kwa mfano, elimu, maandishi na kadhalika.

Matumizi na manufaa ya lahaja

Ijapokuwa lahaja kwa kiwango fulani hutatiza mawasiliano, zina umuhimu wake jinsi tutakavyoainisha ifuatavyo:

Hutumiwa katika kukuza lugha kwa kupanua msamiati wake. Kwa mfano, maneno kama vile rununu, kipakatalishi, tovuti na kadhalika.

Hutumiwa katika kusanifisha lugha.

Hudhihirisha utajiri wa lugha kupitia mitindo mbalimbali ya wazungumzaji.

Hunogeza lugha kwa kutia ladha mazungumzo ya wasemaji mbalimbali.

Huwakilisha historia ya lugha.

Hudhihirisha ukwasi wa lugha

Kuna lahaja mbalimbali za Kiswahili ambazo huainishwa kulingana na eneo la kijiografia zinakozungumzwa.

[email protected]

Marejeo

Chiraghdin, S., Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.

Richards, J.C., (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.

Wardhaugh, R. (1986). An Introduction to Socio-Linguistics. New York: Blackwell Publishers