UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Lahaja za Kiswahili na maeneo zinakozungumzwa
Na MARY WANGARI
KISWAHILI ni lugha inayosheheni lahaja chungu nzima.
Japo wataalamu hawajaafikiana kuhusu idadi kamili ya lahaja zenyewe na mipaka yake,wengi wao wanakubaliana kwamba kuna lahaja zaidi ya kumi na tano.
Baadhi ya lahaja hizo kwa kurejelea maeneo zinakozungumzwa ni kama zifuatazo:
LAHAJA ZA KASKAZINI
KIAMU
Ni lahaja inayozungumzwa kwenye kisiwa cha Lamu ambacho zamani kilifahamika kama Amu. Kiamu ni lahaja ambayo, sawa na Kimvita,inatumiwa sana katika tungo nyingi za zamani za ushairi. Lahaja ya Lamu ina sifa ile ile sawa na Kimvita ya kutumia sauti ‘t’ badala ya ‘ch’. Sifa nyingineya lahaja hii ni sauti ‘g’ na ‘l’ kudondoshwa inapotokea baina ya irabu au sauti za irabu.
Tazama mifano ifuatayo:
KIAMU | KISWAHILI SANIFU |
ndia | njia |
mbegu | mbeu |
Kiyakazi | kijakazi |
nduu | ndugu |
Mbele | mbee |
KIPATE
Hii ni lahaja ya Kiswahili inayozungumwa katika kisiwa cha Pate.
Ni lahaja ambayo pia inatumiwa sana katika maandishi mengi hasa ushairi wa zamani.
Katika lahaja hii, sauti ‘th’ hutumiwa katika maneno ambayo yana sauti ‘z’,‘dh’ au hata ‘v’ katika Kiswahili sanifu.
Kwa mfano:
KIPATE | KISWAHILI SANIFU |
Baratha | baraza |
Uthia | Udhia |
Muhuwa | Marehemu |
Pija | Piga |
Kondo | Vita |
KISIU
Hii ni lahaja ambayo hutumiwa katika kisiwa cha Siu, kilicho karibu nakisiwa cha Pate, na eneo lililoko baina ya Pate na Faza.
Lahaja hii inakaribiana sana na lahaja ya kipate na kwa kiasi lahaja ya Kiamu.
Katika lahaja hii, sauti ‘ch’ hutumiwa pale ambapo katika Kiswahili sanifu pana sauti ‘t’.
Kwa mfano:
KISIU | KISWAHILI SANIFU |
dhiumbe | viumbe |
mbako | baba yako |
kufura | kushiba |
kuchuma | kutuma |
mchu | mtu |
KITIKUU/ KIBAJUNI
Ni lahaja inayozungumzwa kaskazini mwa Pate na Lamu kufikia Kismayu.
Mifano:
KITIKUU | KISWAHILI SANIFU |
nyawe | Mama yako |
kichoweo | kitoweo |
uwavu | ubavu |
nkuru | mkubwa |
peche | pete |
CHIMIINI/ CHIMBALAZI/ KIBARAWA
Hii ni lahaja inayotumiwa na wazungumzaji wa Kiswahili katika eneo la kati kati ya Mogadishu na Somalia.
Lahaja hii huzungumzwa katika maeneo ya Marka na Barawa, si ajabu baadhi ya wataalamu huizungumzia kama lahaja ya Kibarawa.
Marejeo
Massamba, D.P.B., (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Ipara, I. O., Waititu, F.G. (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.
Habwe, J. (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.
Maddo, U., Thiong’o, D. (2006). Mazoezi na Udurusu: Kiswahili 102/2. Nairobi: Global Publishers.