Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Lugha na jamii katika Kiswahili

March 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

NI upi uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii?

Ili kujibu swali hili, ni vyema kwanza kujifahamisha kuhusu dhana muhimu zifuatazo:

Lugha

Inaweza kufafanuliwa kama mfumo wa sauti za nasibu zilizokubaliwa na watu au jamii ili zitumike katika mawasiliano yao ya kila siku ili kueleza hisia, mawazo, matakwa na mahitaji yao.

Jamii

Jamii inaweza kuelezwa kama kundi la watu wanaoishi katika eneo fulani, wanaojitambulisha kama kundi moja, wenye utamaduni mmoja na aghalabu lugha moja.

Isimujamii ni nini? 

Isimujamii ni kipengele cha isimu matumizi kinachoshughulikia uhusiano wa maswala ya jamii-lugha.

Huchunguza matumizi ya lugha katika jamii katika sekta na sajili au rejista mbalimbali. Dhana hapa ni kwamba kila jamii ya watu huwa na upekee wa kutumia lugha kufikia malengo mbalimbali.

Neno isimujamii limejumuisha maneno mawili: isimu na jamii. Tunaweza kuyafafanua maneno hayo jinsi ifuatavyo:

Isimu – Ni sayansi ya lugha.

Jamii – ni mkusanyiko wa vitu vinavyofanana.

Kwa mujibu wa Wardhaugh (1986), isimujamii inahusika na uchunguzi wa kuweka wazi uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii ikiwa na lengo la kuelewa muundo wa lugha na jinsi lugha inavyofanya kazi katika mawasiliano.

Katika isimujamii tunaichunguza jamii ili kufahamu mengi zaidi kuhusu lugha.

Kwa upande wake William Labov (1980), anaeleza kuwa eneo jingine la utafiti ambalo linajumuishwa katika isimujamii ni sosholojia ya lugha. Hii hushughulika na maswala mengi ya kijamii na jinsi yanavyoingiliana na lugha na lahaja.

Haya ni matatizo yanayohusishwa na kudhoofika na hata kufa kwa lugha na kumezwa kwa lugha zenye watu wachache, maendeleo ya uwili lugha, usanifishaji wa lugha, na upangaji wa lugha, hasa katika mataifa yanayoendelea.

Ethnografia

Ni eneo jingine linalojumuishwa katika isimujamii na linahusika na lugha katika matumizi yake.

Ethnografia ni maelezo ya kisayansi kuhusu mbari, mila, itikadi na utamaduni wa binadamu.

Mambo yanayohusika hapa ni kuchanganua ruwaza za matumizi ya lugha na lahaja zake katika utamaduni fulani: matukio yanayozusha mazungumzo, uhusiano kati ya wazungumzaji, hadhira, mada, njia za kuwasiliana na muktadha.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Mekacha, R.D.K., (2000). Isimujamii: Nadharia na Muktadha wa Kiswahili. Osaka: Osaka University of Foreign Studies.

Onyango, J.O., (2002), AKS 102: Historical Development of Kiswahili: Kiswahili Module. Nairobi: Institute of Open Learning, Kenyatta University.

Masebo, J.A., Nyangwine A. D., (2002). Nadharia ya Lugha: Kiswahili 1. Dar es Salaam: Afroplus Industries Ltd.