UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Matumizi ya vihisishi katika sajili isiyo rasmi
Na MARY WANGARI
AGHALABU mazungumzo ya kawaida huandamana na matumizi ya vihisishi kama vile eeh! mmh! aah!
Vihisishi vilivyozoeleka katika Kiswahili ni masalale! na ala!
Hali hii hutokea ili kumpa msemaji fursa ya kufikiri na kuwa na uhakika na anachotaka kusema.
Ubadilishanaji au uchanganyaji ndimi
Ubadilishaji msimbo hutokea wakati ambapo mzungumzaji anasema katika lugha moja kisha baada ya muda akaongea kwa lugha ya pili na kuweza kuongea kwa muda.
Hali hii hutokea wakati ambapo wahusika katika mazungumzo wanapokuwa na uwezo wa kutumia lugha wanazozijua.
Aidha, ubadilishaji ndimi huweza kasababishwa na hali ya wahusika kuonyesha madaha hasa yanayochukuana na tabaka fulani.
Matumizi ya lugha rasmi, isiyo rasmi au lugha ya ucheshi na utani
Matumizi ya lugha kwa njia hii hutegemea wahusika na muktadha. Kwa mfano, mtoto anapoongea na baba yake katika hali ya kawaida, mara nyingi watatumia lugha rasmi kuonyesha heshima na unyenyekevu. Hiki ni kinyume na watani wawili ambao watatumia lugha ya utani na yenye ucheshi mwingi.
Msamiati kubadilikabadilika
Msamiati hubadilika kutegemea mada, uwezo wa lugha wa wasemaji na pia muktadha wa mazungumzo.
Iwapo wasemaji hawana umilisi mkubwa wa lugha, msamiati sahili unaoeleweka kwa urahisi utatumika.
Iwapo wana umilisi mkubwa, mazungumzo yatakolezwa kwa matumizi ya msamiati usiowa kawaida, pamoja na istilahi hasa kutegemea mada.
Sajili za lugha ni miundo au namna mbalimbali za matumizi ya lugha husika. Kila sajili au rejista ina sifa bainifu zinazoitofautisha na lugha jinsi ifuatavyo.
Sarufi – Vipengele vya kisarufi hujitokeza katika sajili kutegemea shughuli. Kwa mfano katika muktadha wa mahakamani na hospitalini, lugha itakuwa na miundomsingi ya kuamuru, kukanusha na maswali.
Kanuni za lugha – Kanuni zinazotawala matumizi tofauti kutegemea sajili. Kwa mfano, lugha ya kitaaluma huhitaji maneno yatamkwe kikamilifu na kwa usahihi.
Adabu: Lugha kwa mfano katika shughuli rasmi maabadini huwa yenye adabu, tofauti na lugha ya faraghani. Katika shughuli kama vile za tohara na ulevi, matumizi ya lugha chafu huwa jambo la kawaida.
Marejeo
Massamba, D.P.B., (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Ipara, I. O. & Waititu, F.G. (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.
Habwe, J., (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.
Maddo, U. & Thiong’o, D. (2006). Mazoezi na Udurusu: Kiswahili 102/2. Nairobi: Global Publisher.