UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mchango wa mazingira katika mabadilikoya lugha kihistoria
Na CHRIS ADUNGO
MWANADAMU daima hujikuta katika mazingira mbalimbali. Kwa kuyachunguza mazingira hayo, binadamu hupata fikira na dhana mbalimbali kuhusu vitu vilivyomo katika mazingira hayo.
Wakati mwingine, huhitaji kuzieleza fikira na dhana hizo kwa wengine. Ili aweze kufanya hivyo, mwanadamu hutumia lugha. Katika mtazamo huo, lugha ni chombo cha kuyawasilisha yale aliyonayo akilini mwake kwa wengine. Katika mtazamo wa kijumla, lugha hujengwa na maneno na maneno huwakilisha mawazo. Hivyo, mwanadamu hutumia lugha kuelezea mawazo aliyonayo. Lakini maneno ayatumiayo mwanadamu kichwani hayana budi kuchukuliwa kwa hadhari.
Kwa kuchukua jinsi yalivyo, zinaweza zikapatikana fikira kwamba uhusiano uliopo baina ya neno na dhana ni ule wa neno moja kuwakilisha dhana moja au kwamba uwiano uliopo baina ya maneno na dhana ni ule wa 1:1.
Fikira za namna hii zina matatizo yake kwani inawezekana kabisa neno moja likawakilisha dhana zaidi ya moja au maneno mengi yakawakilisha dhana moja. Aidha, mara nyingi imetokea kwamba mtu anaweza kukiona kitu akilini mwake lakini akashindwa kupata maneno ya kukielezea.
Kadri jamii inavyozidi kuendelea na mambo mapya kuibuka ndivyo dhana mpya zinavyozidi kujitokeza. Kwa kuwa dhana hizi ni mpya, inabidi zitafutiwe maneno ya kuziwakilisha. Lakini wakati uo huo, inaweza kukubalika kwamba utaratibu wa usemaji na matumizi ya maneno katika lugha vimejengwa katika msingi wa iktisadi ya maneno. Yaani wasemaji wa lugha siku zote hujaribu kutumia maneno machache kadri iwezekanavyo kuwasilisha yale waliyonayo akilini mwao.
Kutokana na utaratibu uu huu wa iktisadi ya maneno, mwanadamu hutumia uwezo alionao wa kupanga mamabo akilini mwake akatafuta dhana zinazoshabihiana kwa namna fulani au ambazo zina chimbuko moja la maana akazipa neno moja tu liziwakilishe. Ndivyo kusema katika lugha, yawezekana kupata neno moja tu likiwakilisha dhana kadhaa zilizo na uhusiano wa namna fulani.
Katika utaratibu uu huu wa iktisadi ya maneno, inawezekana pia kutumia maneno ambayo hapo zamani yalikuwa yanawakilisha dhana fulani yakaweza kuwakilisha dhana mpya ambazo zina uhusiano wa namna fulani na dhana hizo za zamani. Utaratibu huu wa neno moja kuweza kuwakilisha dhana zaidi ya moja na ambazo zina mshabaha wa namna fulani hujulikana kama polisemia.
Polisemia inaweza kutazamwa katika sura mbili mahsusi. Inaweza kutazamwa kihistoria; na inaweza pia kutazamwa kiwakati uliopo. Ikitazamwa kihistoria, polisemia ina maana kwamba neno moja katika lugha inaweza kubakia na maana yake ya awali na wakati uo huo likaweza kupata maana nyingine mpya. Na ikitazamwa kiwakati uliopo, polisemia ina maana kwamba neno moja katika lugha linaweza kuwa na maana zaidi ya moja (Ullman 1997).
Kihistoria
Dhana husemekana kuwa na msingi wa uhusiano wa kihistoria ambapo historia ya dhana hizo, ikichunguzwa inadhihirika kuwa ama zimetokana na neno moja au maana moja imetokana na nyingine iliyokuwa ya awali ambazo si lazima zilingane au zipatane (coincide). Maana mbili zinahusiana kihistoria ikiwa zinaweza kurejelewa nyuma kwa chemchemi au chanzo kile kile kimoja (same source) au ikiwa maana moja inaweza kutoholewa kutoka kwa ile nyingine.
Kisinkronia
Polisemia hutokea tu inapokuwa kuna dhana zaidi ya moja ambazo zinawakilishwa na neno moja. Lakini dhana hizo sharti ziwe na uhusiano wa namna fulani. Leech (1984:228-9) anaita aina hii ya polisemia, polisemia kisaikolojia. Polisemia kisaikolojia hutukia ambapo neno moja ambalo limetokana na maneno mawili au zaidi tofauti lakini watumiaji wa lugha husika kwa kuvichunguza vihusika viwakilishavyo maneno hayo, wakahisi kwamba vinahusiana kwa namna fulani.