UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mtazamo wa kimakro katika uhakiki wa Isimujamii
Na MARY WANGARI
LEO hii tutaangazia mkabala wa kimakro au mkabala finyu katika uchambuzi wa isimujamii.
Mtazamo mpana ni tofauti na mtazamo finyu katika uchambuzi wa isiumjamii kwa kuwa unahusisha watu wengi kijiografia.
Katika mkabala huu, lugha hufafanuliwa kwa kutumia mwingiliano wa mbinu na dhana anuwai kutoka kwa taaluma nyingine za kijamii.
Aidha, mtazamo huu huangazia mambo yote yanayohusu matumizi ya lugha kwa jumla. Kimsingi, mkabala huu hujihusisha na hatua ya kufahamu lugha zilizopo katika jamii na uhusiano wake na lugha nyingine.
Kwa mfano, mwanaisimu jamii kulingana na mtazamo huu hujishughulisha na kubaini sababu za kimsingi zinazofanya lugha moja ama iteuliwe kuwa lugha ya taifa, lugha rasmi, au lugha ya kufundishia katika elimu.
Sababu kama hizo aghalabu huwa hazina budi zitokane na misingi ya pamoja ya kiisimu na kijamii. Aidha, mkabala huu hutilia maanani lugha ambazo hazikuteuliwa kutwaa dhima fulani kitaifa.
Mtazamo huu huziangazia lugha hizo kama zenye umuhimu na zinazopaswa kukuzwa na jamii zinazohusika ili kuzindumisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Katika isimujamii wanaisimu hujishughulisha kujua ni nani anazungumza lugha fulani, ni lugha ipi inayozungumza, inazunguzwa wapi, inazungumza kwa nini na kwa shabaha gani pamoja na maswala mengineyo muhimu.
Isitoshe, mwanaisimu huangazia maana pekee yake bali huangalia maana kwa kuzingatia taratibu na kanuni za mawasiliano zinazotumika katika jamii inayohusika.
Hii inamaanisha kwamba uchambuzi wa kupata maana katika lugha haufanywi bila kuzingatia taratibu za kijamii na mazingira ya tamko huika.
Tunaposema mazingira tunamaanisha hali ya kuhusisha mahali tamko liliposemwa, kujua habari za mzungumzaji na msikilizaji pamoja na uhusiano wao na kufahamu taratibu na kanuni zinazotawala mawasiliano ya lugha inayohusika.
Isitoshe, mkabala huu hujihusisha na uchambuzi wa sentensi zisizotumiwa katika mazungumzo ya majibizano.
Katika mtazamo huu, masuala kama vile utamaduni, mila, kaida na itikadi zinazohusika na mawasiliano katika jamii na kadhalika zinapaswa kuzingatiwa katika mchakato wa uchambuzi.
Aidha, kulingana na kanuni za mawasiliano katika jamii husika, mtu mwenye umri wa chini anastahili kutumia kiambishi cha nafsi ya kwanza wingi badala ya umoja anapozungumza na mtu wa umri wa juu kama ishara ya heshima.
Hii ni kuambatana na kanuni na kaida zinazotumika katika mawasiliano ya lugha husika.
Kwa mujibu wa Fishman (1972), ni muhimu kwa wataalamu kutumia mbinu za pamoja (kiisimu na kijamii) katika kufikia uteuzi wa lugha ili zichukue dhima mbalimbali katika jamii.
Mtazamo wastani
Mtazamo mwingine unaohusika katika uchambuzi wa isimujamii ni mtazamo wastani au ukipenda mkabala kati.
Kimsingi, mtazamo huu huzingatia mambo ya kimsingi tu yanayotokana na mkabala mpana na mkabala finyu. Hoja kwamba lugha inapaswa kufafanuliwa kwa kuzingatia kanuni za kiisimu pekee ni hoja ya upeo wa juu.
Hata hivyo, mtazamo wa kimaikro ungali unasheheni mambo ya kimsingi yanayoweza kutumika kueleza lugha kwa kutumia msingi wa isimu jamii.
Baadhi ya kanuni za fonolojia na mofolojia kwa mfano zinaweza kutumiwa sambamba na sifa nyingine za kijamii ili kueleza kaida zinazofuatwa na watumiaji wa lugha katika mazingira mbalimbali.
Mwanaisimu jamii ana uhuru wa kushughulikia uchambuzi wa lugha kwa viwango na idadi ya wanajamii wanaoitumia lugha anayoipendelea kulingana na lengo la kazi yake.
Miongoni mwa wanaisimu wanaoegemea mtazamo wastani ni pamoja na Erin Tripp (1971). Mwanaisimu huyu anasisitiza umuhimu wa kuchunguza kanuni za kijamii zinazotawala mazungumzo mbalimbali ya kila uchao.
Vilevile, anahoji kwamba mazungumzo yanayofanywa na watu hayafanyiki kiholela bali hufuata kanuni za mawasiliano katika jamii zinazohusika.
Kwa mujibu wa mtazamo huu, isimujamii inapaswa kushughulikia uchunguzi wa kanuni na kaida za kijamii zinazotawala mawasiliano kwa jumla.