UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Muktadha wa ufundishaji lugha; ufundishaji wa darasa mseto
Na MARY WANGARI
ILI kufanikiwa katika mchakato wa kujifunza lugha ni sharti mwanagenzi atilie maanani mambo yafuatayo:
Ni muhimu mwanafunzi azingatie majukumu ya kijamii. Kwa mfano, ataanzaje kuzungumza na mtu asiyemjua? Baadhi ya watu wana mamlaka fulani hivyo kuna utaratibu wa kuzungumza nao.
Majukumu ya kisaikolojia pia ni muhimu. Kwa mfano, mtu anayejifunza lugha hapaswi kuegemea upande wowote mathalani kisiasa ama kuegemea chama tawala au upinzani.
Mazingira ya lugha ilipo. Je ni lugha ya taifa? Watu wanaokuzunguka wanatumiaje?
Ni muhimu kuelewa kwamba lugha haihusu sarufi na fonolojia pekee bali pia ni chombo cha mawasiliano. Hivyo basi, inahitaji kufundishwa kimawasiliano zaidi.
Muktadha wa ufundishaji lugha
Dhana hii inarejelea mazingira halisi ambapo tukio la ufundishaji lugha hufanyika. Muktadha wa ufundishaji lugha huhusisha wadau wakuu watatu ambao ni mwanafunzi, mwalimu, na jamii.
Mwalimu anapaswa kutoa kazi na mazoezi ya lugha kwa wingi. Ili kufanikisha shughuli ya ufundishaji wa lugha, ni sharti mwalimu azingatie mambo yafuatayo:
i. Ni muhimu kwa lugha kutumiwa katika mazingira halisi na yanayostahili ukilenga kwenye stadi nne za lugha
ii. Lugha itumiwe kwa kuzingatia muktadha.
iii. Kunapaswa kuwepo na matumizi ya mazingira halisi ya darasa mathalani picha, katuni na kadhalika.
iv. Himiza ushirikiano miongoni mwa wanafunzi baina yao na baina ya wanafunzi na mwalimu.
v. Tumia mbinu zaidi ya moja. Mfano vikundi, majibizano.
vi. Fafanua kwa uangalifu masuala ya kisarufi.
vii. Mwalimu ni sharti ajue maono ya mwanafunzi kama vile huzuni, ucheshi miongoni mwa mengine.
viii. Kuunda mazingira ya utani darasani.
Ufundishaji wa darasa mseto
Kwa mujibu wa TUKI (2013), mseto ni hali ya kuwa na mchanganyiko wa makabila au vitu mbalimbali kutengeneza kitu fulani.
Hapa ni mchanganyiko wa darasa lenye wanafunzi wanaotoka sehemu mbalimbali na wenye umri tofauti, malengo tofauti na kadhalika.
Hivyo basi, ni sharti mwalimu atofautishe sana katika ufundishaji wake na awe makini ili asije akawakwaza baadhi ya wanafunzi.
Marejeo
Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili in Teacher Training Colleges in Tanzania”. Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318
Mtembezi, I. J. (1997). Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha yaKufundishia. Dar es Salaam: BAKITA.
Kamusi ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) kwa sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI).