• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia ya Simulizi/ Naratolojia

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia ya Simulizi/ Naratolojia

Na MARY WANGARI

NADHARIA hii inahusiana na usimulizi wa hadithi.

Hadithi ni fabula inayoelezewa kwa mtiririko wa kimantiki unaosimulia kuhusu tukio fulani.

Prince anafafanua dhana ya simulizi kama uelezaji wa tukio moja au mengi ya kihalisia au kibunilizi.

Kulingana na maelezo ya Gérard Genette, simulizi ni mfuatano halisi au wa kibunulizi ambao ni kiini au yanayolengwa na usemi fualani.

Kulingana naye, simulizi huhusisha utambwaji wa matukio. Nadharia hii huchunguza sifa zinazohusisha simulizi na kuzitenganisha nyingine.

Msingi wake umewekwa na Mwanafalsafa Plato ambaye anadai kuwa usimuliaji hulingana na udhihirishaji.

Plato anazua vipengele viwili ambavyo ni mimesia na digesia.

Mimesia – Katika kipengele hiki, mtunzi hajitokezi waziwazi kama msemaji

Digesia – Hapa msemaji anaweza kutambulika na hadhira yake. Aidha, mtaalamu Lord Raglan katika kazi yake ya ‘The Hero’ iliyosheheni maisha ya mashujaa wa kitamaduni kama vile Oedipus, Robi Hood amechangia sana katika kukua kwa nadharia hii.

Anaeleza kwamba ni lazima kuwe na mfuatano maalumu wa matukio katika uandishi kama vile kutabiriwa kwa kuzaliwa kwa shujaa, kuzaliwa kwake, maajabu yake, ukombozi wake na hatimaye kifo chake kutokana na usaliti. Wahakiki wa kinaratolojia wamebainisha dhana mbili katika usimulizi: wakati hadithi na wakati matini.

Wakati Hadithi

Huu ni wakati inaochukua hadithi husika kuanzia mwanzo hadi mwisho. Wakati unaweza kueleweka kwa urahisi kwa kuwa unaweza kuwa baina ya siku moja, miezi mitatu au hata miaka mingi inayohusisha vizazi.

Wakati Matini

Dhana ya wakati matini ni wakati unaochukua kusoma kazi. Wakati huu ni vigumu kutathminiwa ila itategemea muda atakaouchukua msomaji na kasi yake.

Hali kadhalika, kuna wakati ambapo wakati matini unakuwa mrefu ukilinganishwa na wakati hadithi. Hili limejitokeza katika hadithi ya S. A Mohammed ya ‘Kiza katika Nuru’, ambapo Mvita amefika ofisini na hajatenda lolote bado kwa muda mrefu ilhali msomaji anaendelea kusoma.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Mulokozi, Mugyabuso & Kahigi K.(1979). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.

Njogu, K. & R.M. Wafula (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Shihabuddin, C. (1970). Utangulizi. Malenga wa Mvita. Nairobi: Oxford University Press

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vitengo vya Semiotiki

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Viambajengo vya Nadharia ya...

adminleo