Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia za kujifunza lugha (Sehemu ya Pili)

June 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

MBINU hii, kwa Kiingereza, audiological method, ilitokana na haja ya ukalimani nchini Amerika miaka ya 1940s.

Waasisi wa mbinu hii ni wasomi Bloomfield (1942) na Fries (1945).

Kiambajengo kikuu katika nadharia hii ni kile kinachosemwa.

Maandishi hayakupewa fursa kubwa bali kile kilichosemwa ndicho kilikuwa cha muhimu sana.

Bloomfield alisema kuwa lugha si katika maandishi bali ni kile ambacho kinasemwa.

Nadharia hii inahusisha kusimulia mada mbalimbali na kupima uwezo wa kusikia.

Wapigiaji debe wa mbinu hii walipenda sana kutumia muziki, nyimbo, usimulizi na kughani.

Walisisitiza stadi za:

  1. Kusikiliza
  2. Kuzungumza
  3. Kusoma
  4. Kuandika
  5. Kuona

Mbinu ya kushirikisha jamii (Community language learning method)

Mwasisi wa nadharia hii ni Curran (1976).

Kwa mujibu wa nadharia hii, hoja kuu ni kwamba lugha ni watu. Hii inamaanisha kwamba huwezi kutenga jamii na lugha.

Waasisi walidai kwamba ili uweze kumfundisha mwanafunzi mgeni basi nenda kwenye jamii husika.

Aidha, walidai kwamba iwapo utaamua kufundishia darasani basi darasa lako lifanye angalau lifanane kwa kiasi fulani na jamii ya lugha husika.

Isitoshe, ili uweze kufundisha watu ni lazima ushirikishe watu wanaotumia lugha hiyo. Mwanafunzi atapata vichocheo vya aina nyingi katika jamii na kubaini ni mambo gani yanafaa na mambo gani hayafai. Nadharia hii inaipa kipaumbele jamii kama chombo muhimu katika kujifunza lugha.

Mbinu ya ukimya (Silence method)

Nadharia hii inaamini kwamba kila lugha ina mfumo wake tofauti na lugha nyingine.

Hivyo basi, ufundishaji wa lugha ya pili ni sharti ulenge kumfanya mjifunzaji wa lugha kuwa mmilisi au kukaribia kuwa mmilisi wa lugha anayojifunza

Ili kuweza kutimiza hili, mwalimu anahitaji kujenga mazingira ya utani katika darasa jambo ambalo litaleta matokeo mazuri ya umilisi wa lugha husika. Nadharia hii inamhitaji mwalimu kufanya tathimini kwa wanafunzi wake ili kubaini kama kuna mabadiliko.

 

[email protected]

Marejeo

Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili in Teacher Training Colleges in Tanzania”. Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

Mtembezi, I. J. (1997). Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia. Dar es Salaam: BAKITA.