UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya utafiti kidijitali katika ukuaji, maendeleo ya Kiswahili
Na MARY WANGARI
KATIKA siku za hivi majuzi, wadau kadha wa Kiswahili wamejitokeza kupigia debe suala la Kiswahili kufanywa lugha rasmi si tu Kenya, bali pia Afrika Mashariki kwa jumla.
Juhudi hizi zinapaswa kupongezwa na pia zinapaswa kuwa mwamko mpya kwa wadau wa Kiswahili kutilia maanani teknolojia ili kuimarisha nafasi ya lugha hii katika kizazi cha sasa. Kwa mintarafu hiyo, ni muhali kupuuza nafasi ya teknolojia katika ukuzaji na maendeleo ya Kiswahili ili kuweza kukidhi mahitaji ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika karne hii.
Utafiti kidijitali pamoja na lugha kimitambo ni baadhi ya masuala ibuka ambayo yana nafasi muhimu mno si tu kwa lugha za Kiafrika kama vile lugha ya Kiswahili, bali pia lugha za kimataifa. Hii hasa ni kwa kuwa utafiti kidijitali au lugha kimitambo inafidia mapungufu yanayoshuhudiwa katika utafiti kimapokeo au utafiti wa king’amuzi (Intuitive Research).
Kuna sera anuwai zinazoimarisha Teknolojia ya Lugha, hali inayoipa nafasi muhimu kwa lugha zinazotimiza majukumu nyeti kimawasiliano. Teknolojia ya lugha inatoa nafasi kwa Lugha za Kiafrika ambazo hazijapata fursa ya kuwepo katika jukwaa la kidijitali kwa muda mrefu kama baadhi ya lugha zenye asili ya Uropa zilivyo, pia zinatafitiwa na kuainishwa kutumia teknolojia ya lugha lau kwa viwango vidogo sana. Kama wanavyohoji wataalamu De Pauw et al (2006) De Pauw and de Schryver (2008) na wengineo, Kiswahili ni mojawapo wa lugha za Kiafrika ambazo zimedhihirisha uwepo mkubwa kwenye majukwaa ya kidijitali. Isitoshe, katika majilio ya intaneti, lugha kadha za Kiafrika pia zimejikuta katika mazingira haya ya kidijitali-mtandaoni.
Ni bayana kuwa ndio mwanzo mkoko unaanza kualika maua katika utafiti kidijitali au ukipenda matumizi ya teknolojia katika Kiswahili pamoja na lugha nyinginezo za Kiafrika ikilinganishwa na lugha za mataifa yaliyoendelea kama vile Kiingereza, Kifaransa, Kijapani, Kichina, Kijerumani, Kireno miongoni mwa nyinginezo.
Maendeleo katika utafiti kidijitali yamepiga hatua kuu kiasi cha kuzuka kwa Maarifa Kimitambo (AI) – mfumo wa mawasiliano kutumia kompyuta ambao umezuka kwa fujo katika ulingo wa teknolojia na kubadilisha pamoja na kurahisisha utendakazi kwa njia ambayo hata isingeweza kukisiwa. Ni vyema kufahamu kuwa kumekuwa na juhudi kadha za utafiti wa Kiswahili kwa kutumia teknolojia ya lugha kutoka kwa wanaisimu na wataalamu mbalimbali wa Kiswahili. Baadhi ya tafiti hizi zimeangazia Kiswahili kwa kuchunguza viambajengo vyake mbalimbali. Tafiti hizi kidijitali hutumia programu aghalabu hujikita kwenye kanuni za lugha na zile za kimitambo au ukipenda kikompyuta.
Kuna mbinu mbalimbali zinazohusika katika utafiti wa lugha ya Kiswahili kidijitali zinazoambatana na vipengele mbalimbali vya lugha. Dhamira kuu ya utafiti wa Kiswahili kidijitali ni kukuza na kuendeleza Kiswahili kama lugha muhimu ya Kafrika kupitia Uhandisi wa Lugha au Teknolojia ya Lugha.
NADHARIA: Baadhi ya nadharia muhimu zinazotumika katika mchakato wa utafiti wa Kiswahili kidijitali ni pamoja na Nadharia ya Isimu Kongoo au Mtazamo wa Kikongoo na Nadharia ya Msambao wa Uvumbuzi (Diffusion of Innovation Theory) ambayo mwasisi wake ni Everett Rogers (2003). Lengo kuu la mikabala hii ni kujaribu kufafanua jinsi utafiti kidijitali ulivyo na manufaa zaidi katika kizazi cha leo ikilinganishwa na utafiti kwa kutumia mitindo ya kimapokeo.
MANUFAA: Aidha, tafiti za wataalamu kadha waliolivalia njuga suala hili, zimehitimisha kuwa utafiti wa lugha kidijitali una manufaa mengi ikizingatia: Mitambo au tarakilishi zina uwezo mkubwa zaidi wa kukusanya na kuchakata data ikilinganishwa na binadamu. Kiwango kikubwa cha data inayokusanywa inampa mtafiti upeo zaidi wa utafiti, utafiti kidijitali huwezesha kuhifadhi data kimitambo hivyo kulainisha mchakato wote wa utafiti kuanzia uundaji, utathmini kwa kujumuisha kamusi, tafsiri-kimitambo uchanganuzi kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia, kisemantiki,ufundishaji lugha na kadhalika.