Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sababu za kuchanganya au kubadili msimbo katika lugha ya Kiswahili

May 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

HUMSAIDIA mzungumzaji kujieleza vizuri kwa lengo la kufidia upungufu wa msamiati.

Upungufu huu unaweza kutokana na mzungumzaji mwenyewe kukosa msamiati wa kutosha au lugha anayoitumia kutokuwa na msamiati wa kutosha.

Humwezesha mzungumzaji kuonyesha hisia. Hisia hizi huenda zikawa za kirafiki, furaha au za kuchukiza.

Kujitambulisha katika kundi linalotumia lugha fulani.

Umahiri wa lugha mbili au zaidi: Hii ni hali ambayo mzungumzaji anamudu vyema lugha zaidi ya moja, hivyo basi hujikuta anahama kutoka lugha moja hadi nyingine.

Iwapo katika jamii lugha moja ina hadhi kuliko nyingine, watu hupenda kuchanganya au kubadili msimbo ili kuweza kujinasibisha na hadhi hiyo.

Hasira: Mtu akighadhabika aghalabu huchanganya ndimi katika kauli zake.

Sajili/ Rejista katika miktadha mbalimbali

Sajili ni vilugha vinavyojitokeza katika jamii kutokana na tofauti za kikazi, eneo atokalo mtu, urafiki wa karibu sana, umri au hata tabaka. Aidha, sajili hutumika kwa lengo na nia mbalimbali kama vile:

  • Kurahisisha mawasiliano na pia kuelewana
  • Kufupisha muda wa maongezi
  • Uhifadhi wa kumbukumbu
  • Kujitenga na makundi mengine ya sajili hiyo

Basi, kwa kutumia sajili, tunaweza kupata vilugha kama vile lugha ya wavuvi, sajili ya mahakama, hospitali, dini, shuleni, Sheng’ na vitarafa.

Vitarafa

Hivi ni vilugha ni vinavyotokana na wazungumzaji au wasemaji wake kuwa au kuishi katika eneo moja. Mfano ni Kiswahili cha Kenya na kile cha Tanzania au Uganda.

Umuhimu wa sajili za lugha

Huwezesha watu kuficha siri zao kwa kuwatenga wale wasioielewasajili ile. Vijana aghalabu hufanya hivi wakawatenga wazazi wao kwa kutumia msamiati ambao wazazi wao hawaelewi.

Hufidia mahitaji maalumu ya mawasiliano. Kwa mfano, sajili ya dini itafidia mahitaji maalumu ya mawasiliano katika mazingira ya kibiashara.

Huwezesha mawasiliano baina na kati ya watu, hivyo kuelewana.

Huwasaidia wazungumzaji kutokwenda nje ya mada husika.

Huwezesha wazungumzaji kujikita katika muktadha maalumu kutegemea sajili husika na hivyo kurahisisha mawasiliano. Hii ni kwa sababu wazungumzaji huwa wamefahamu wanashughulikia nini na muktadha wao.

 

[email protected]

Marejeo

Chiraghdin, S. & Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.

Richards, J.C. (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.

Wardhaugh, R. (1986). An Introduction to Socio-Linguistics. New York: Blackwell Publishers.