Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uchambuzi wa hadithi 'Masharti ya Kisasa' (Alifa Chokocho)

August 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

ANWANI ya hadithi hii inasawiri maudhui yaliyomo ndani yake.

Mambo yote yanayomkuta Dadi yanatokana na yeye kutofahamu ni nini kinachoashiriwa na mkewe kila anaposema “masharti ya kisasa”.

Mwishowe anatawaliwa na wivu unaozua matatizo.

Mtunzi anadhamiria kuonyesha jamii kwamba wivu wa kupindukia ni hatari sana kwa maendeleo.

Anajadili kwa kina kiini cha migogoro kati ya wanandoa, ahadi za maisha, elimu, urembo, umbea na masengenyo, itikadi na utamaduni na nafasi ya mapenzi ya dhati.

MAPENZI NA NDOA

Ndoa ni zao la mapenzi na mapenzi huhimili ndoa. Mapenzi na ndoa hukumbwa na changamoto mbalimbali. Baadhi ya wapenzi huwawekea wenzao masharti ya kufuata ili kudumisha uhusiano.

Kidawa alimpa Dadi masharti ya mapenzi ya kisasa kama vile kuosha vyombo, kufagia nyumba, kukuna nazi na kadhalika.

Dadi asingemkataza Kidawa kufanya jambo lolote kwa vile asingesikia wala kutii kwa sasa sababu kila wakati alikumbushwa kuhusu masharti ya kisasa aliyowekewa na Kidawa kabla ya kuoana.

Aliyavumilia masharti haya kwa miaka tisa. Hali hii inamfanya Dadi kuanza kushuku kuwa Kidawa ana uhusiano wa nje kimapenzi, jambo ambalo analifuatilia kijinga na hatimaye kujidhuru.

Wanawake wanateua kupendwa na wanaume wengi, hali inayowalazimu kuwafanyisha mitihani ili waweze kuchagua mume wa ndoa. Ingawa wanaume wengi walimpenda Kidawa, anahiari kuishi na yule ambaye angefuata masharti yake kama vile kuzaa mtoto mmoja.

Ijapokuwa Kidawa alimpa Dadi mitihani mingi na akawashinda wanaume wote, ni dhahiri kuwa hiki si kigezo cha kuchagua mume.

Kuna mambo mengi yanayofaa kuchunguzwa kabla ya watu kula yamini ya ndoa, kwa mfano kiwango cha elimu, ufahamu wa mambo, uhuru wa kusema, na kadhalika.

Kuna ukosefu wa uaminifu kati ya wanandoa.

Dadi anashuku iwapo mkewe anamwendea kinyume kimapenzi. Anashuku kuwa Kidawa ana uhusiano mwingine wa kimapenzi na Mwalimu Mkuu.

Alipanga kumfuata mkewe kazini usiku mmoja kwa nia ya kumfumania na ‘mpenzi wa kando’ ili athibitishe kuwapo kwa uhusiano wa kimapenzi kati yao.

Alipopanda ghorofani na kuchungulia dirishani, alibaini kuwa hakukuwa na uhusiano wowote wa kimapenzi, ila kwa bahati mbaya alianguka na kuumia vibaya.

Kujipamba na kujirembesha kwa Kidawa kunamtia Dadi shaka. Anashuku kwamba mkewe amejipamba kwa ajili ya kumfurahisha Mwalimu Mkuu. Dadi anapokosa kutambua urembo wa mkewe, Kidawa anakasirika kutokana na fikra potovu za mumewe.

Kuna changamoto tele katika kusaidiana, hasa lijapo suala la majukumu ya nyumbani. Dadi anapokosa kuondoa na kuviosha vyombo baada ya kula, Kidawa anakasirika sana.

Baadhi ya watu huchunguza na kusema mengi sana dhidi ya wanandoa. Bi Zuhura anamuuliza Dadi iwapo amemaliza samaki amuuzie au amebakiza wa kumpikia mkewe nyumbani. Dadi anakasirika kwa vile suala la atakayepika halikufaa kumhusu Bi Zuhura hata kidogo. Aliona kuwa anajipenyeza kwa mambo ya ndani ya ndoa kati yake na Kidawa.

Mwandishi anajadili kazi wazifanyazo wanawake walioolewa. Ni changamoto kubwa kwa Kidawa kufanya kazi ya umetroni ambayo humlazimu kukosekana nyumbani usiku. Mchana huwa akifanya biashara ya kuchuuza bidhaa. Kidawa hana wakati kabisa wa kuwa nyumbani na kumhudumia mumewe.

Hali hii pamoja na kujirembesha kwake hasa anapoenda kazini kunamfanya Dadi aanze kushuku kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na Mwalimu Mkuu.

Kuna tofauti kubwa katika viwango vya elimu. Inabidi Kidawa ambaye amesoma hadi darasa la kumi na mbili amtafsirie Dadi baadhi ya maneno ya Kiingereza.

Wivu unamfanya Kidawa kutotaka kumwona Dadi akiwatazama na kuvutiwa na wanawake waliojipamba kwa mavazi na vipodozi. Anamuonya mumewe akome kuwatazama wanawake wa aina hiyo.

Tatizo la mawasiliano ni changamoto nyingine. Dadi alisongwa na fikra iwapo Kidawa alijipamba kwa ajili yake au Mwalimu Mkuu. Kidawa alipomweleza ni kwa ajili yake, hakusema lolote. Kidawa alipomweleza Dadi kuwa ilifaa aviondoe vyombo na kuviosha maadamu yeye alipika, alinyamaza. Hakumuuliza Kidawa iwapo alimpenda Mwalimu Mkuu. Badala yake, anapanga njama ya kuwafumania kisiri ambapo matokeo yake ni yeye kujidhuru.

MIGOGORO NA SHAKA

Dadi anavutana na hisia ndani yake. Anashuku iwapo Kidawa ana uhusiano wa kimapenzi na Mwalimu Mkuu. Hali hii inamfanya kununa na kupanga kuwafumania wawili hao wakila uroda, ambapo alianguka na kuumia vibaya.

Kuna mvutano hasa Dadi anapomtaka mkewe Kidawa aache kazi ya umetroni. Anashuku kwamba Kidawa humwendea kinyume kimapenzi kila anapoelekea kazini usiku. Pia kuna mgogoro kati ya Kidawa na Dadi kwa sababu ya biashara anayoifanya ya kuchuuza bidhaa. Dadi alitaka kumkataza mkewe asitembeze bidhaa tena. Kidawa asingekatazika kwa vile daima alimrejesha Dadi kwa masharti ya ndoa ya kisasa.

Mvutano mwingine unatokana na mavazi yanayovaliwa na wanawake. Dadi anawatazama na kuvutiwa na wanawake kutokana na mavazi yao pamoja na kujirembesha kwao. Kidawa anamkataza ila anasongwa na fikra hasa akikumbuka jinsi mwanamke aliyeolewa anavyojipamba na kujipeleka kwa mwanamume mwingine.

Kuna mgogoro unaotokana na majukumu ya nyumbani. Kidawa anataka Dadi aviondoe vyombo mezani na kuviosha maadamu yeye alipika. Anataka wasaidiane. Dadi anapokataa, Kidawa anamkasirikia. Kujirembesha na kujipamba kwa Kidawa kunamtia Dadi wasiwasi tele. Kidawa alijirembesha ili ampendeze mumewe. Badala yake, Dadi anawaza kwamba kujirembesha huko kwa Kidawa ni kwa sababu ya Mwalimu Mkuu.

Mvutano unasababishwa pia na tofauti za viwango vya elimu na ufahamu wa mambo kati ya Kidawa na Dadi. Inabidi Kidawa ayatafsiri baadhi ya maneno katika lugha ya Kiswahili ili Dadi aelewe. Dadi angezumgumza na Kidawa ili aiondoe shaka ya kwamba mkewe anahusiana na Mwalimu Mkuu kimapenzi, ila aliongozwa na ujinga. Anaparamia paipu ili athibitishe hayo. Hatimaye anaanguka na kuumia.

ELIMU

Ili kufanikisha elimu, Mwalimu Mkuu hana budi kutia bidii kazini. Anakwenda kufanya kazi usiku ili kuzipunguza. Walinzi waliwajibika kuwalinda wanafunzi shuleni. Walipowasikia watu wakimtaja mwizi, walifika ghafla jengoni na walipomuona Dadi amepanda juu ya paipu, walidhani ni mwizi aliyekuwa akiwachungulia wasichana.

Kidawa anafanya kazi ya umetroni kwa bidii ili awalinde wasichana bwenini wakati wa usiku. Tofauti katika viwango vya elimu husababisha kutoelewana na mvurugano katika ndoa.