• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 5:55 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uhusiano wa Isimu na Lugha kwa mujibu wa Sapir na Whorf

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uhusiano wa Isimu na Lugha kwa mujibu wa Sapir na Whorf

Na MARY WANGARI

LEO ninalenga kujibu maswali ya msomaji wetu kama alivyouliza:

Habari za leo Bi Marya,

Mimi ni mdau wa lugha ya Kiswahili.

Ombi langu kwako; unisaidie kujibu maswali ya isimujamii yafuatayo:

 

1)    Elezea uhusiano wa isimu na lugha kwa mtazamo wa Sapir–Whorf

2)   Jadili sera mbalimbali na maoni ya kitaalamu (juu ya) kuhusu matumizi ya lugha na lugha za kufundishia katika nchi ya Tanzania.

3)   Onyesha uelewa wako (juu ya) kuhusu upangaji wa lugha kwa kutumia mifano mukthadha wa Tanzania.

4)   Isimujamii ni  utanzu mpya. “Elezea isimujamii ilivyotokea na maendeleo yake mpaka sasa

Natanguliza shukrani zangu.

WANAISIMU Sapir na Whorf wanafafanua kwamba lugha huathiri sana na kudhibiti jinsi wazungumzaji na watumiaji wa lugha wa jamii fulani wanavyoufasili ulimwengu wao.

Kulingana na wanaisimu hawa, muundo wa maana katika lugha ndiyo msingi wa mawazo au utaratibu wa fikra.

Isitoshe, mwanadamu hawezi kufikiri kamwe bila kutu mia lugha.

Jambo hili linamaanisha kuwa kwa vile mawazo na fikra za mwanadamu zinatawaliwa na lugha basi inawezekana kudhibiti fikra za wanajamii kwa kuidhibiti lugha yao.

Katika muktadha wa nchi nyingi za Kiafrika, hoja hii imethibitika bayana.

Kwa mfano, idadi kubwa ya Waafrika wanahusisha maarifa au ustaarabu na lugha ya Kiingereza.

Hii inatokana na kasumba potovu iliyoenezwa na wakoloni kwamba lugha ya Kiingereza ni lugha yenye hadhi huku wakidunisha lugha za Kiafrika.

Hivyo uwezo wao wa kudhibiti matumizi ya lugha kwa kututoa katika matumizi ya lugha mame umefanikisha kuelekeza fikra za baadhi ya Waafrika kwenye mawazo kwamba ithbati ya kuwa mstaarabu au msomi kufahamu Kiingereza.

Mbali na uhusiano uliopo baina ya jamii na lugha, hakuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya lugha na jamii kwa sababu zifuatazo:

  1. Kwanza, sio lazima lugha iwe ya watu wa jamii ile ile. Mathalani, Kiswahili sio lugha ya Waswahili peke yao.
  2. Watu wanaoishi katika nchi fulani sio lazima wawe wa asili ya nchi hiyo. Hivyo basi, jina la jamii haliwezi kuwiana na lugha wanayoongea.
  3. Lugha moja huwa na vilugha kadha ndani mwake. Kwa mfano, lugha ya Kiingereza ina kile nitasema Viingereza kadha ndani yake kwa maana kwamba inasheheni lahaja chungu nzima.
  4. Kuna jamii yenye jina tofauti na lugha wanayozungumza, mathalani Wamarekani, hawazungumzi Kimarekani bali Kiingereza.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

 

Marejeo

Ipara, I. O. & Maina, G. (2008). Fani ya Isimujamii kwa Shule za Sekondari. Nairobi: Oxford University Press (OUP).

King’ei, K. (2010). Misingi ya Isimujamii: Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (TATAKI). Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Msanjila, Y.P. na wenzake (2010). Isimujamii: Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

You can share this post!

Ufisadi: Nani msema kweli?

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana ya lugha na utamaduni...

adminleo