Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uhusiano wa Isimu na taaluma nyinginezo (Sehemu ya Pili)

February 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

Isimujamii na Isimu Saikolojia

SAIKOLOJIA ni taaluma ambayo hujishughulisha na michakato ya kiakili, uzalisha wa matamshi katika kujifunza lugha na tabia za watu katika jamii.

Taaluma hii inahusiana na isimujamii kwa kuwa mwanaisimu jamii hutumia saikolojia kuchunguza matumizi ya lugha miongoni mwa wanajamii.

Saikolojia humwezesha kutafiti na kueleza michakato ya ubongo katika kujifunza lugha na umri ambao watoto hujifunza lugha.

Pia mwanaisimu jamii huchunguza na kutoa ufafanuzi kwa nini watu hutofautiana kitabia hivyo ufafanuzi huo huzingatia viengele mbalimbali kama vile mazingira wanakotoka watu hao, historia za familia zao na hulka asili za wahusika kutokanana lugha anayotumia mzungumzaji  ni rahisi kwa mwana isimu saikolojia kutambua mzungumza wa rika gani ni mtoto, kijana au mzee.

Isimujamii na Isimu Historia

Uhusiano kati ya taaluma hizi ni kuwa mwanaisimu jamii huweza kuchunguza lugha za wazungumzaji na kupata taarifa zinazohusu jamii husika.

Lugha inayotumiwa na jamii huweza kutoa taa#ifa fulani kuhusiana na msamiati wa lugha hiyo pamoja  na ukale wa msamiati kama ulivyokuwa ukitumika hivyo basi mwanaisimu huchunguza na kutambua mabadiliko yaliyotokea na yanayoendelea kutokea katika lugha kwa mfano katika lugha ya Kiswahili neno oa lilikuwa lola wakati fulani enzi za jadi.

Isimujamii na Isimu Muundo

Kulingana na Massamba na wenzake (2001), isimu muundo ni utanzu wa sarufi unaojishughulisha na uchanganuzi wa mpangilio wa maneo katika sentensi na uhusiano  wa vipashio vya lugha katika kuonyesha au kuboresha mpangilio wa vipashio vya lugha katika sentensi ili kujenga upatanisho wa lugha wenye mantiki.

Isimujamii humsaidia mwanaisimu kuzingatia kanuni na sheria ambazo hufuatwa katika mfuatano unaokubalika na wenye kuleta maana inayoeleweka na kila lugha huwa na utaratibu wake maalum wa kutunga kipashio katika tungo.  Kwa mfano, sentensi inaweza kuwa:

Kunywa mrija kwa soda.

Muundo wa  sentensi ni mzuri lakini hauna maana; hivyo muundo ungepaswa kuwa:

Kunywa soda kwa mrija.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili in Teacher Training Colleges in Tanzania”. Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

Mtembezi, I. J. (1997). “Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia”. Dar es Salaam: BAKITA.

Mulokozi, M. M. (1991). “English versus Kiswahili ni Tanzania’s Secondary Education”. Swahili Studie Ghent.