• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umilisi wa lugha na isimu

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Umilisi wa lugha na isimu

Na MARY WANGARI

KATIKA makala ya leo, tutaangazia mada kuhusu umilisi wa lugha na isimu ya Kiswahili miongoni mwa wanafunzi, walimu na wanajamii kwa jumla.

Kwa muhtasari, dhana hii ya umilisi wa lugha inaweza ikafafanuliwa kama uwezo wa kutumia lugha vilivyo huku dhana ya isimu jinsi tujuavyo, ni sayansi ya lugha.

Hivyo basi, umilisi wa kiisimu ni ule uwezo wa mtumiaji lugha wa kubuni na kutumia sentensi kuambatana na kanuni za kisarufi katika lugha husika.

Aidha umilisi wa kiisimu humwezesha mtumiaji wa lugha kutambua makosa katika sentensi za lugha hivyo kutumia lugha kwa usahihi na kwa ufasaha.

Umilisi wa kiisimu unaweza kuelezwa vilevile kama vigezo vya kiisimu au sarufi ambavyo hupatikana katika viambajengo vya lugha.

Kulingana na tafiti, umilisi wa lugha unaweza ukachanganuliwa kwa kutumia mikabala anuai ambayo ni pamoja na: mkabala wa kupenda kuzungumza lugha, mkabala wa hali ya kupenda au kuchukia sayansi ya lugha, mkabala wa umilisi wa isimu ya lugha na mkabala wa hali ya kupenda au kuchukia kitu au mtu.

Mikabala hii ya umilisi wa lugha kiisimu inaweza kuainishwa katika vigezo anuwai ambavyo ni kama vifuatavyo:

Mikabala chanya – Hii ni mitazamo inayomwezesha mwanafunzi au mtumiaji wa lugha kwa jumla kufahamu lugha upesi na kumudu kuitumia ifaavyo kuambatana na kanuni za lugha husika.

Kigezo hiki hujengwa kwa muda katika hisia na huhusisha hali ya mwanafunzi kupenda na kutumia lugha husika.

Mikabala hasi – Hii inahusisha kigezo cha kuchukia kitu na hujengwa kwa muda katika hisia za binadamu au ukipenda mtumiaji lugha.

Mikabala ya jinsia – Ni kigezo cha kibayolojia jinachojikita katika hali ya kuwa mwanamme au mwanamke.

Mikabala hii huashiria hali ya kuchukia au kupenda ama jinsia ya kike au jinsia ya kiume.

Mikabala mingine inayohusika katika umilisi wa lugha inahusisha azma, ari na motisha ya kujifunza lugha, majaribio pamoja na mitihani inayotumiwa na wakufunzi katika juhudi za kupima kiwango cha umilisi wa lugha na isimu miongoni mwa wanagenzi.

[email protected]

Marejeo

Chomsky, N. (1965). Aspects of the theory of syntax. Cambridge: Mass MIT Press.

Habwe & Karanja (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi. Phoenix Publishers.

Wanyoike, P. (1978). Vikwazo katika mafunzo ya Kiswahili Kenya. Lugha 5-3

 

  • Tags

You can share this post!

Washirika zaidi wa Trump waambukizwa Covid-19

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Ufafanuzi wa wataalam kuhusu...