• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Viambajengo vya nadharia ya Semiotiki

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Viambajengo vya nadharia ya Semiotiki

Na MARY WANGARI

Nadharia ya semiotiki vilevile imegawika katika vitengo vinginevyo mathalan:

  1. Semiotiki ya kiakili
  2. Semiotiki ya kiutamaduni
  3. Semiotiki viumbe hai
  4. Semiotiki ya kifasihi
  5. Semiotiki ya kimuziki
  6. Semiotiki ya kijamii
  7. Semiotiki ya violwa na kadhalika.

Fauka ya hayo, semiotiki inamulika jinsi kazi ya fasihi inavyowasiliana na wasomaji.

Nadaharia hii inaeleza zaidi jinsi matini inavyofasiriwa na namna inavyooana na wasomaji wake.

Viambajengo vya nadharia ya Semiotiki

Nadharia hii imejikita katika maelezo ya mwanaisimu mashuhuri Ferdinard de Saussure aliyeeleza kuwa lugha ni mfumo wa ishara ambazo huangaza na kuunda mkufu wa ishara.

Alidai kuwa kila ishara huwa na sehemu mbili zifuatazo:

Ishara yambwa/kiashirii – Sehemu hii husimamia sauti au wasilisho la kimaandishi/matini

Kifasiri/kiashiriwa – Ni sehemu ambayo ni maana ya kiashirii

Kwa muhtasari, maelezo haya yanadhihirisha kuwa kiashirii ni neno lenyewe na kiashiriwa ni maana yenyewe ya kiashirii.

Madai haya yanamaanisha kuwa kiashirii ni picha-sauti ilhali kiashiriwa ni dhana na ishara ni jumla ya matokeo ya uhusiano baina ya kiashirii na kiashiriwa. Kwa mujibu wa Ferdinard, semiotiki huangalia matini yoyote ile kama iliyosheheni ishara mbalimbali zinazofungamanishwa na maana ya kifasihi.

Kwa mfano, kiashirii cha neno ‘chui’ ni sauti ya kiutamkaji au herufi za kiuandikaji lakini kiashiriwa ni mnyama wa porini. Kwa hivyo uhusiano uliopo ni wa kinasibu.Wanasemiotiki hata hivyo wanashikilia kuwa, kiashirii huweza kuwa kile kile bali kinachoashiriwa kinaweza kuwa tofauti.

 Kwa mfano:

Barani Ulaya, neno ‘pombe’ huweza kuwa ishara ya urafiki, pongezi, wema, ukarimu au mapenzi lakini kiashirii kinabaki kuwa neno ‘mvinyo’. Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa kiashirii kimoja kinakuwa na viashiriwa vingi katika lugha ya kawaida.

Mwanaisimu mwingine Peirce anaendeleza uchunguzi wa Saussure wa ishara kuwa na sehemu mbili kiashirii na kiashiriwa na anaongezea kipengele cha tatu ambacho ni sehemu ya kifasiri. Anaeleza kuwa ishara ina misingi inayoibua aina tatu za ishara ambazo ni kama zifuatazo:

  1. Kielekezi
  2. Ishara-tanakali
  3. Taashira.

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Mulokozi, Mugyabuso & Kahigi K.(1979). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es Salaam: Tanzania Publishing                   House.

Njogu, K. & R.M. Wafula (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Shihabuddin, C. (1970). Utangulizi. Malenga wa Mvita. Nairobi: Oxford University Press.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia ya Semiotiki

Ajali baina ya gari la pesa, basi yaua watano

adminleo