Makala

Ukuta wa El-Nino wawakinga wakazi wa Mpeketoni dhidi ya mafuriko

April 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

MARA nyingi raia katika maeneo mbalimbali ya nchi na dunia kwa ujumla, wamekuwa wakishtushwa au kuhangaika punde wanaposikia tangazo la uwezekano wa kutokea kwa mvua ya El Nino na athari zake.

Kuna wale ambao utawaona wakiwa wamefunganya virago wakihama kwenye makazi yao kama tahadhari ya mapema kujiepusha na zahama za mafuriko ziletwazo na El Nino.

Kwa wakazi wa Mpeketoni na viunga vyake, hali ni tofauti.

Hapa, wakazi hawashtushwi na maonyo yoyote yanayofungamana na El Nino na mafuriko.

Hii inatokana na kuwepo kwa ukuta wa jadi ambao umekuwa ukiwasaidia kupima, kukadiria na kufahamu kienyeji iwapo ni kweli mvua, El Nino au mafuriko yashuhudiwayo ni mabaya na ya kutisha na yanayofaa kutorokwa au la.

Ukuta huo ambao miaka ya hivi karibuni umebandikwa jina na wenyeji kuwa ‘Ukuta wa El Nino’ uliachiwa au kuchorwa alama maalumu ya kina cha maji ya El Nino ya mwaka 1997.

Alama au mchoro huo umewafanya wakazi wa Mpeketoni na viunga vyake kutobabaika wakijua fika kuwa wako salama.

Ni tofauti na kuta zilizozoeleka katika fukwe za Bahari Hindi.

Hapa, wasiwasi wa wenyeji tu ni endapo kutakuwa na El Nino nyingine kama ile ya 1997, ambayo itaishia maji yake kuufikia, kuugusa au hata kima cha maji kuukwea ukuta huo hadi kuifikia alama husika.

Ukuta huo wa jadi uko mita kadhaa pembezoni mwa Ziwa Kenyatta.

Ziwa Kenyatta ambapo ‘Ukuta wa El Nino’ uko mita chache pembezoni mwake. PICHA | KALUME KAZUNGU

Ni ukuta ambao ni mojawapo ya gofu la jumba la zamani lililokuwa likitumika kama ofisi za Idara ya Kilimo kabla ya kusambaratika kwake na kutekelezwa hadi jengo hilo kuporomoka miaka ya tisini (1990s).

Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumanne, wazee wa Mpeketoni wakiongozwa na Bw Benson Kariuki, walisema jamii nzima ya eneo hilo haijakuwa yenye kutapatapa wanaposhuhudia mafuriko maeneo mengine ya Lamu, Kenya na ulimwengu.

Bw Kariuki anashikilia kuwa mvua mbaya na mafuriko ya kuogopwa na jamii ya Mpeketoni yalikuwa yale ya 1997 ambayo yaliishia kuufikia ukuta huo na kuukwea kwa karibu mita 2.

Kwenye kimo hicho cha mita mbili ukutani ndipo kulipoachwa alama hiyo ya kudumu.

Mzee wa Mpeketoni, Bw Benson Kariuki akionyesha mstari au alama ya kina cha maji ya El Nino ya mwaka 1997 kwenye ukuta ulioko karibu na Ziwa Kenyatta. Ni alama hiyo ambayo huwapa wakazi wa eneo hilo hakikisho kwamba wako salama dhidi ya El Nino endapo haitafikiwa na maji wakati mvua au mafuriko yanaposhuhudiwa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Wazee wanashikilia kuwa hata baada ya mvua kubwa iliyoshuhudiwa kusita na maji au mafuriko kuisha zaidi ya miongo miwili iliyopita sasa, alama bado ipo.

“Mvua au El Nino mbaya zaidi ambayo ilitushtua sisi wakazi wa Mpeketoni ni ile ya 1997. Hiyo ndiyo iliyopelekea Ziwa letu la Kenyatta kujaa hadi kuvunja kingo zake na maji kutapatapa kote. Ziwa letu lilijaa kwa kima cha karibu mita 12. Ni kutokana na hilo ambapo maji yalizidi kupanda, kuufikia na hata kuukwea ukuta wa gofu hili kwa karibu mita mbili,” akasema Bw Kariuki.

Kwa upande wake, Bi Susan Mwangi, mkazi wa mji wa Mpeketoni, anaieleza alama iliyoachwa ukutani na maji ya El Nino ya mwaka 1997 kuwa ya hakikisho kwao kwamba hali hiyo haitajirudia.

Bi Mwangi anailinganisha alama hiyo ya ukuta na hadithi ya Kitabu cha Mwanzo katika Biblia kwa waumini wa dini ya Kikristo, akisema ni sawa na ule upinde wa mvua wa kwanza au gharika.

Anasema katika Biblia Nuhu aliahidiwa na Mungu kwamba hangeuharibu ulimwengu tena kwa gharika kuu.

Ili kumhakikishia ahadi hiyo, Mungu akatoa upinde uwe kitu cha kuwakumbusha Nuhu na binadamu wengine watakaoishi ulimwenguni kwamba hataifunika tena dunia yote kwa maji.

“Alama yetu ya ukutani tukiiona na tunaposikia maonyo kuhusu El Nino itarajiwayo nchini, hatushtuki. Tunajua fika kuwa hata mvua inyeshe kiasi gani, haitafikia ile mbaya ya 1997. Yaani hii alama uionayo ukutani hapa twahisi ni sawa na ule upinde wa hadithi ya Biblia kuhusu gharika, ambapo Mungu aliahidi watu wake na wanyama wote kwamba hatawaharibu tena kwa gharika,” akasema Bi Mwangi.

Wakazi aidha wanashikilia kuwa uhakika wao kuhusiana na alama hiyo ya ukutani haumaanishi kutozingatia maonyo ya watabiri wa hali ya anga nchini.

Bw Simon Njuguna alisema kuna wengine, hasa wale wanaoishi maeneo ya nyanda za chini za Lamu, ikiwemo Witu, Moa, Dide Waride, Kitumbini, Lumshi A na B, Chalaluma na viunga vyake, ambao kila mara wamekuwa wakitii maelekezo, hivyo kuhama sehemu zao na kuelekea maeneo salama.

Anajitetea kwa kusema serikali au Wakenya wasiwachukulie vibaya wanajamii wa Mpeketoni kwa kudhania kuwa msimamo wao huo kuhusu alama ndiyo mwisho kabisa wa mambo au ni fainali.

“Hapana. Bado tumekuwa tukihimiza wenzetu, hasa wale wanaojijua wanaishi nyanda za chini, kuchukua tahadhari ya mapema. Ila kwetu sisi wa papa hapa Mpeketoni, hatubanduki hadi ile siku ambapo tutashuhudia hayo mafuriko yakifikia au kukaribia alama yetu ya ukutani. Yaani tuko salama ilmradi ukuta usifikiwe au kusombwa na mafuriko,” akasisitiza Bw Njuguna huku akiangua kicheko.