ULIMBWENDE: Epuka matumizi holela ya vipodozi vyenye kemikali
Na MARGARET MAINA
KWENYE mahojiano na Anne Kamau, mkazi wa Nakuru ambaye amevitumia vipodozi vya asili kwa muda baada ya uso wake kuchipuka na kufanya mabaka ya kutisha, anasema hali yake sasa imeimarika pakubwa.
“Ninawasihi wanawake kuepuka matumizi mshobemshobe ya vipodozi vya kemikali,” anashauri Anne.
Badala ya kutumia vipodozi vikali ambavyo wakati mwingine huweza kusababisha maradhi kama saratani kwa sababu ya kemikali vilivyo nazo, ni vyema ukatumia vipodozi vya asili ambavyo ni rafiki kwa ngozi yako.
Hata hivyo, ni vizuri kutambua kwamba aina yoyote ya ngozi ni nzuri mradi isiwe na harara, upele au mabaka.
Watu weusi na weupe wasipozifanyia ngozi zao matunzo bila shaka zitaharibika na kupoteza mvuto.
Zipo njia mbalimbali za kuifanya ngozi yako iwe na weupe wa kipekee kwa kutumia vitu vya asili ambavyo hupatikana jikoni kwako, tena kwa urahisi.
Ili kuing’arisha ngozi yako, unaweza kuvitumia vitu kama vile;
Limau
Limau linaweza kuufanya uso wako ukapata weupe wa kipekee na kwa wale wenye ngozi nyeusi wakawa waang’aavu.
Kata limau nusu. Ile nusu nayo ikate nusu, hivyo utapata robo. Sugua limau katika uso wako na uruhusu juisi yake iingie katika ngozi yako.
Baada ya shughuli hiyo, acha juisi hiyo ibaki usoni kwa dakika 15.
Safisha uso wako kwa maji ya moto. Fanya hivyo angalau mara mbili kwa wiki na utaona mabadiliko.
Asali na maziwa ya unga
Chukua kikombe, weka maziwa ya unga kijiko kimoja, asali kijiko kimoja na juisi ya limau nusu kijiko.
Changanya kisha paka usoni na usugue taratibu. Acha ikae usoni kwa robo saa na kisha osha taratibu kwa maji moto. Utayaona matokeo baada ya muda mfupi.
Nyanya na unga wa mahindi
Chukua nyanya moja, isage kisha changanya na unga wa mahindi. Jaribu kuufanya mchanganyiko wako mwepesi ili upakike na ukae usoni. Sugua uso wako kwa mchanganyiko huo na uache ukae usoni kwa dakika 20.
Mchanganyiko wa matunda
Chukua tango, nanasi na papai bichi, kisha visage kwa pamoja.
Mchangayiko laini utakaopatikana hapo ndiyo dawa yako. Usugue uso wako taratibu kutoka chini; yaani kidevuni kwenda juu. Uache ukae usoni kwa dakika 20 kisha osha kwa maji baridi.