Makala

ULIMBWENDE: Jinsi unavyoweza kuitunza ngozi kuondoa ukavu

March 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MARGARET MAINA

[email protected]

UKIWA una ngozi kavu, unahitaji uangalizi wa hali ya juu sana kwa sababu ngozi hii huwa inakibiliwa sana na mikunjo na chunusi.

Hali hii hutokea sana kipindi cha baridi ambapo ngozi huwa inakuwa kavu.

Licha ya hayo, kuna vitu unavyoweza kufanya ili kuweza kuitunza ngozi kwa kupunguza ukavu na huku ukiipa ulinzi dhidi ya hali tunayoweza kuiita ni kuzeeka mapema kwa ngozi.

Osha uso wako kila siku kwa kutumia sabuni ya kusafishia uso ambayo haina kemikali na wala usitumie sabuni ambayo itaondoa asili ya mafuta kwenye ngozi yako.

Tumia vilainishaji (moisturiser) kwenye ngozi kila siku wakati wa mchana.

Unatakiwa kupaka kilainishi kwenye ngozi yako kwa kuanzia juu kwa kuzungusha mduara na sio kuvuta au kusugua ngozi yako.

Paka losheni kwenye ngozi yako kabla ya kwenda kulala. Ni vyema kutumia losheni ambazo zina Alpha Hydroxy Acids.

Alpha Hydroxy Acids hukausha, huua na kuondoa tabaka la ngozi ya nje huku ikilainisha ngozi mpya inayotoka.

Kamuone daktari

Kama ngozi yako ni kavu na inaelekea kuwa nyekundu yenye mistari inayouma au vipele, unatakiwa kumuona daktari wa ngozi.

Hali hii pia inaweza kusababishwa na hali ya hewa au vitambaa kama vile pamba, vitu tunavyopaka kwa ajili ya kutunza ngozi, sabuni na kadhalika.

Daktari anaweza kukushauri ni losheni gani utumie kulainisha ngozi yako na kuondoa wekundu kwenye ngozi yako

Kama ni miezi ya baridi husababisha ngozi yako kuwa kavu, matumizi ya mara kwa mara ya vilainishi yatasaidia ngozi yako kuwa angavu na nyororo.