ULIMBWENDE: Jinsi ya kufanya ili ngozi yako iwe laini na ya kung’aa
Na MARGARET MAINA
USO ni sehemu muhimu sana na watu wanaojielewa huchukua muda mwingi kuhakikisha wanavutia; hasa wanawake.
Yaani ukitaka kujua ni jinsi gani mwanadada au mwanamke anapenda urembo basi wewe mwangalia tu usoni.
Siri moja ambayo mwanadada anafaa kufahamu ni kwamba ni muhimu kujiaminisha kuwa wewe ni mrembo kuliko watu wanavyokuchukulia.
Ukishajiamini mwenyewe unatakiwa sasa kufanya mambo yafuatayo kudumisha mwonekano mzuri.
Osha ngozi yako kila siku
Katika kusafisha ngozi kuna mambo mengi unapaswa kufanya. Jitahidi kuifanya ngozi yako kuonekana nyororo na safi muda wote. Hii itakusaidia kuonekana mrembo kwa asilimia zote.
Ondoa ngozi iliyokufa, sugua ngozi ili kuondoa mafuta na uchafu unaokuwa umeganda katika ngozi yako.
Jaribu kuchagua bidhaa bora za kutumia katika kusafisha ngozi yako.
Fanya mazoezi
Mazoezi yanakufanya uwe mkakamavu siku zote. Pia mazoezi yanasawazisha mwili na kufanya uwe na umbo la wastani lenye mwonekano wa kuvutia.
Mazoezi ni miongoni mwa vitu vinavyochangia afya ya ngozi na urembo. Fanya mazoezi na hata ikiwezekana kuwa na ratiba ya kukuelekeza ni wakati gani unatakiwa kuwa uwanjani au vyumba spesheli vya kufanyia mazoezi. Hii iwe ni sehemu ya maisha yako.
Epuka vipodozi vya mara kwa mara.
Kuna watu wamezoea kupaka vipodozi karibu kila mara. Kufanya hivi kunaiacha ngozi muda wote ikiwa imefungana na kukosa hewa safi ya kutosha.
Ifahamike kwamba sio kila kipodozi ni urembo. Vipo vingine huharibu ngozi yako. Unashauriwa kuonana na wataalamu wakupe ushauri kuhusu ni kipodozi kipi sahihi cha kutumia, lakini pia epuka kupaka vipodozi na ukalala navyo.
Mara nyingi vipodozi vyenye kemikali vinasababisha kulegea kwa ngozi.
Pata usingizi wa kutosha
Sio kwa afya ya mwili na akili tu, bali usingizi wa kutosha husababisha mtu kuonekana mrembo. Kulala kwa muda unaofaa kunakufanya usionekane mchovu na macho yako yanakuwa maangavu siku zote.