Makala

ULIMBWENDE: Vitu vya asili vinavyoweza kuondoa utofauti wa rangi unaosababishwa na mionzi ya jua

September 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

TUKIWA kwenye shughuli za kila siku tunaathiriwa na mionzi ya jua. Hali hii imekuwa ni jambo la kawaida.

Mionzi hii haifikii tu ngozi zetu lakini pia huweza kusababisha mabadiliko fulani katika ngozi na kuzifanya zionekane zimefifia au kuwa nyeusi zaidi.

Chukulia mfano wa mtu anayetembea juani kwa muda mrefu. Utaanza kuona rangi ya kipaji cha uso kikiwa tofauti na sehemu nyingine za uso.

Na kwa wale wenzetu wanaovaa nguo zinazoacha wazi maeneo ya kifua au mgongo, utagundua rangi za maeneo hayo ziko tofauti na sehemu zingine za mwili.

Hali hii inajulikana kama suntanning. Hutokea pale ngozi inazalisha zaidi chembe hai zinazoifanya sehemu hiyo kuwa na rangi nyeusi (melanin), ikijaribu kujilinda dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na mionzi ya jua

Kuna njia za asili na rahisi ambazo unaweza kuzitumia ili kusaidia kuondoa utofauti wa rangi ya ngozi unaoletwa na mionzi ya jua.

Nyanya na asali

Mahitaji:-

  • nyanya 1 na asali (kijiko kikubwa)

Namna ya kufanya

Kuna njia mbili unazoweza kutumia kuandaa. Chukua nyanya, ikate katikati na uchovye asali upande huo ulioukata kisha anza kupaka sehemu iliyoathirika.

Jinsi ya pili ni uchukue nyanya uisage na kisha uchanganye asali na uanze kupaka. Subiri kwa dakika 20. Baada ya hapo, oga kisha jifute kwa kitambaa safi. Fanya hivi kila siku kupata matokeo bora.

Tango na asali

Mahitaji:-

  • tango 1
  • asali (kijiko 1 cha chai)

Namna ya kufanya:

Saga tango kisha changanya na asali. Paka mchanganyiko huu sehemu iliyoathiriwa, subiri kwa robo saa kisha oga. Tumia njia hii mara moja au mbili kila siku.

Limau na sukari

Mahitaji:-

  • limau
  • sukari (kijiko kikubwa 1)

Namna ya kufanya:

Kamua limau kupata juisi kiwango cha kijiko kimoja hivi na uchanganye sukari kwenye maji ya limau. Tumia mchanganyiko huu kama scrub katika sehemu iliyoathiriwa kwa ku-masaji taratibu kwa dakika tatu kisha oga. Fanya hivi mara kwa mara kupata matokea mazuri zaidi.

Apple cider vinegar na Baking soda

Mahitaji:-

  • baking soda (kijiko 1 cha chai)
  • vinegar (kijiko 1)

Namna ya kufanya:

Changanya baking soda na vinegar kupata mchanganyiko ambao sio mzito sana. Paka mchanganyiko huu kama scrub na subiri kwa dakika 10 halafu oga. Tumia hii mara moja au mbili kwa wiki.

Papai

Mahitaji:-

  • papai lililoiva

Namna ya kufanya:

Chukua papai, menya halafu ulisage. Paka mchanganyiko huu sehemu iliyopata madhara na usubiri kwa dakika 20. Muda huo ukishapita, nawa kwa maji fufutende. Paka kila siku au mara kwa mara mpaka utakapopata matokeo yatakayo kuridhisha.

Viazi ulaya

Mahitaji:-

  • kiazi

Namna ya kufanya:

Kata kiazi katikati kisha anza kusugua sehemu husika taratibu.

 

Mbali na njia hizi zilizotajwa, pia inashauriwa kutumia mafuta maalum (sunscreen) ili kuikinga ngozi dhidi ya madhara ya mionzi ya jua.