UMBEA: Starehe ya mapenzi ni kupata raha na amani katika maisha
Na SIZARINA HAMISI
SITACHOKA kuzungumzia ndoa, uhusiano na maelewano baina ya wapendanao.
Hii ni mbali na maoni na maswali mengi ambayo nimekuwa nikipokea, wengine wakifurahi kwa yanayoandikwa, wengine wakikosoa na hata wengine kunichamba bila huruma.
Dhana ya mapenzi ina wigo mpana na ndio maana wengi wetu tunapoamka na kufanya kazi ama shughuli zetu hadi mwisho wa siku, masuala ya mapenzi huwepo akilini, tukifiria, kuota ama kutamani kwa jinsi moja ama nyingine.
Ukiwa ni mtu mzima uliye rijali, siku haitapita bila kufikiria jambo moja ama mawili yanayohusu mapenzi.
Jukumu langu sio kumzodoa mtu ama kumkwaza yeyote, bali ni kukumbushana mengi tunayofahamu na kushauriana pale inapoonekana dhahiri tunakosea.
Kwenu ninyi mlio katika mapenzi, hasa wanandoa, kwanza yawapasa mfahamu kitu, mapenzi ni tunu au zawadi maalum kutoka kwa Mola wetu
Starehe ya mapenzi ni kupata raha na amani katika maisha yetu, hivyo wanaochezea na kuyavuruga kwa makusudi kwa kuumiza hisia za wenzao na kuwasababishia simanzi, si watu wa kupendeza mbele ya macho ya wale wanaojua hasa nini maana ya mapenzi.
Mojawapo ya barua pepe niliyopata hivi karibuni ni kutoka kwa kaka ambaye alionyesha bayana kutoridhika na tabia yangu ya kimbelembele cha kuzungumzia vitendo vya akina kaka katika mapenzi.
“Ningependa nikueleze kwamba wengine tunachukizwa unavyoandika mambo ya wanaume kufurahisha mabibi zao. Mwanaume ni kukaa ngumu, sio kuchekacheka na mwanamke…” Sehemu ya ujumbe kutoka kwa kaka ambaye nitalibana jina lake.
Nami nakujibu kaka, kwamba naheshimu mawazo yako, naheshimu msimamo wako. Lakini ukweli siku zote utabaki kuwa ukweli, kwamba kwenye upendo hushamiri upendo na kwenye chuki hushamiri chuki.
Mkeo ni zawadi kutoka kwa Mola, anatakiwa awe pumziko na tulizo la moyo wako, anatakiwa akupe amani na sio karaha. Lakini mazingira haya yanahitaji kupaliliwa, ukiwa mtu wa kuweka sura ya kazi na kunguruma kila siku, maisha yako yatakuwa ya kunguruma. Utazeeka kabla ya wakati wako sababu ya makunyanzi ya kwenye uso. Badala ya kufurahia maisha, maisha yatafurahishwa na vibweka vyako.
Shida iliyopo kwa baadhi ya wanaume ni kutumia vibaya mfumo dume hasa katika suala nyeti kama mapenzi. Mapenzi si ubabe, mapenzi ni upole na ukarimu.
Pamoja na kwamba mmebarikiwa kwa kupewa nafasi ya kuwa kichwa katika nyumba lakini linapokuja suala la kurekebisha tofauti zinazojitokeza katika mahusiano yenu, si vyema kutumia njia za kibabe.
Upendo
Ukweli utabaki kwamba wanawake wana hisia na wamebarikiwa upendo wa hali ya juu, ndio maana wakapewa dhamana ya kubeba mtoto tumboni kwa miezi tisa na pia kumnyonyesha na kumlea kwa miaka kadhaa bila kulalamika wala kuchoka.
Nasema ni watu wa hisia kwa sababu, huridhika sana na kujisikia vizuri wanapopewa zawadi za hali na hata maneno pia.
Ukitaka kuishi kwa maelewano na mwanamke, mpende na umuheshimu.
Pamoja na dhana potofu iliyopo kwamba mwanaume haridhiki na mwanamke mmoja, jitathmini vya kutosha kabla ya kuamua kuishi kulingana na kauli hii.
Ridhika na mpenzi uliye naye, heshimu hisia zake na thamini mapenzi yake kwako na mpe kile kitu roho inapenda.
Kwa akina dada, msikilize na mheshimu mumeo, kwani ukienda kinyume cha hapo, huwa hawakawii kubadilika hasa wanapokwazwa.
Kama kweli unampenda, basi muonyeshe unamheshimu, hapo utampata.