UMBEA: Ukimpata mnayependana kwa dhati, msifanye mzaha
Na SIZARINA HAMISI
KATIKA tembea yangu na pitapita mitaani pamoja na mazungumzo ya walio katika uhusiano, nimebaini kwamba wengi wanaishi kwa mazoea na sio kwa upendo wa dhati.
Mazungumzo yangu na baadhi ya akina dada yakabaini kwamba wengi wanaishi pengine na waume ama wapenzi wao, sababu ya watoto, sababu hawana kipato cha kujikidhi ama sababu ya kuhofia jamii; watu watasemaje nikiachana na mume wangu?
Hata hivyo wapo baadhi ambao wamebahatika kuwa kwenye ndoa yenye upendo wa dhati.
Katika hali ya kawaida, huwa sio rahisi sana kukutana na mwanamume ama mwanamke ambaye mtapendana kiuhalisia, kwa dhati mpatiane ule upendo usiokuwa na matarajio yoyote kutoka kwa mwenzako.
Kwamba sio rahisi kukutana na mtu ambaye utampenda sana, naye akupende kupitiliza.
Inaweza ikakutokea hivyo mara moja katika maisha yako lakini ni nadra kuweza kutokea tena kwa mara nyingine.
Yupo ambaye anaweza akuambie alikuwa na mwenzake aliyempenda sana, lakini kutokana na sababu mbalimbali, alijikuta ameoa au kuolewa na mtu mwingine kwa sababu ya uhitaji wa ndoa kwa wakati huo.
Yawezekana akawa anapata shinikizo kutoka kwa ndugu, jamaa au marafiki. Anajikuta ameanzisha uhusiano na mtu mwingine na baadaye kufunga naye ndoa. Wengi wanaoingia kwenye ndoa za aina hii huwa wanapitia kipindi cha mateso katika uhusiano mpya.
Hivyo unapopata nafasi ama wasaa wa kuwa na uhusiano na mwanamke ama mwanamume ambaye mnapendana kwa dhati, ukiweza shikilia uhusiano huo, kwani ni mara chache sana kuwa katika uhusiano halisi wa aina hii.
‘Bora tuishi’
Mara nyingi wanaofunga ndoa, hufanya hivyo sio kwa upendo wa dhati, bali katika harakati za kutimiza wajibu, kwamba naye ahesabiwe ameoa ama kuolewa, lakini kiwango cha kumpenda kinakuwa ni nusu na wala sio kamili. Hivyo unakuta wanandoa wa aina hii wanaishi pamoja, wanazaa watoto lakini hawana upendo wa dhati baina yao. Inakuwa ni bora tuishi.
Katika yote ni vyema kuelewa thamani ya kupendana, na unapokutana na mwenzako mkapendana na mkaweza kuwa pamoja na kuishi pamoja, inafaa ushikilie uhusiano huo, kwani ni nadra kutokea.
Wengi hawatambui kwamba kuishi na mtu unayempenda ni bahati na sio jambo la kawaida, kwani hali ni tofauti kwenye ndoa ama mahusiano mengi. Wanaichukulia hali hii kama jambo la kawaida na pale uhusiano unaposambaratika na kupata mtu ambaye hagusi moyo, ndipo majuto huanza. Utakuta mwanamke huyu ama mwanamume anajuta sababu mazingira hayaruhusu tena kurudi kwa yule aliyempenda.
Umewahi kutathmini kwamba iwapo unaishi na mtu ambaye unampenda halafu na yeye anakupenda kwa dhati ni nini itakuwa faida ya uhusiano wenu? Inaweza kuwa ni furaha katika maisha yenu, mtastarehe vizuri kwa sababu kila mmoja atakuwa na amani na mwenzake.
Hivyo dada ama kaka iwapo upo katika uhusiano na mwenzako unayempenda, naye anakupenda, itumieni vizuri fursa hiyo, msiiache ipotee, kwani ikitokea hivyo mtakumbuka baadaye, mtatamani hali irudi ilivyokuwa, lakini huenda kusiwe na nafasi hiyo tena.
Kwa nini utengeneze mazingira ya kuja kujuta baadaye, wakati nafasi unayo ambayo ni sasa? Madhara ya kuingia kwenye ndoa na mtu ambaye hauna upendo naye kwa asilimia mia moja ni makubwa sana. Usipokuwa makini, matatizo ya usaliti ndipo yanaibuka.
Mnapokutana wawili ambao kweli mkijitathmini mnapendana kwa dhati, msifanye mzaha. Msiringiane. Tengenezeni maisha yenu vizuri na muweke mikakati ya kudumisha uhusiano wenu.
Tengenezeni mapito yenu, ishini kwa malengo ili muweze kufika mahali mjivunie mikakati yenu.