• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
Umoja wa Nyanza na Mlima Kenya waja katika kura ya 2027?

Umoja wa Nyanza na Mlima Kenya waja katika kura ya 2027?

NA MWANGI MUIRURI 

MIRENGO kadha ya kisiasa eneo la Mlima Kenya imeanza harakati za kuchumbia mrengo wa Azimio ambao utaachwa na upweke ikiwa Raila Odinga atafaulu kuteuliwa mwenyekiti wa tume ya muungano wa Afrika (AU).

Ususi wa mpango huo umesemwa kushirikishwa chini kwa chini na wandani hata wa Rais William Ruto na wale wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, hali ambayo inatazamiwa kuzua mawimbi makali 2027.

“Ni ukweli kwamba tuko na mipango ya kuungana kupitia muungano wa wazalendo wetu walio ndani ya Azimio na pia ndani ya Kenya Kwanza,” akasema mwandani wa Bw Kenyatta Bw Zack Kinuthia.

Bw Kinuthia ambaye alisimamia kitengo cha mshirikishi wa vijana wa Mlima Kenya ndani ya Azimio la umoja alisema kwamba “tuko kwa majadiliano makali na ya kina kuhusu 2027 na tutashtusha na kutetemesha wengi na muungano ambao tunalenga kuzindua”.

Alisema wengi wa wafathili wa Azimio kutoka Mlima Kenya kwa sasa wameanza kujipanga upya kutokana na uwezekano wa Bw Odinga kuondokea siasa za uchaguzi hapa nchini “baadhi yao wakiwa ndani ya serikali sasa lakini lengo letu la pamoja likiwa ni kujaribu kurekebisha hali kupitia muungano wa kisiasa ukileta pamoja wadau kutoka nje ya Mlima Kenya “.

Bw Kinuthia alisema awamu ya kwanza ndiyo inatekelezwa kwa sasa ikiwa ni ya kuunganisha baadhi ya wanasiasa ambao wako na uwezo wa kuwakilisha eneo hilo katika majadiliano na wengine kuhusu kinyang’anyiro cha 2027.

Aidha, amesema wanangojea uhakika kwamba Bw Odinga atajitoa kwa siasa iwapo atapata wadhifa huo wa AU.

“Awamu ya pili itakuwa ya kusaka ushirika na maeneo mengine pamoja na vyama vyao huku awamu ya tatu ikiwa ni sisi kuunda chama chetu cha Mlima Kenya na hatimaye Kutia mikataba ya uhusiano na uwaniaji,” akasema.

Mmoja wa anayesemwa kuwa katika mikakati hiyo ni mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro ambaye hivi majuzi amekuwa akipigiwa debe kama aliye na uwezo wa kuibuka kuwa Rais.

Kampeni zake zimekuwa zikivumishwa na Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu pamoja na Mbunge wa Gatanga Bw Edward Muriu na ambao tayari wameamrishwa na wakuu wao kwa serikali kukoma mdahalo huo.

Hata hivyo, Bw Nyoro amekuwa akiendeleza siasa zake nje ya Mlima Kenya akionekana kusuka muungano wa wanasiasa walio na sura ya kitaifa.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Bw Babu Owino alikiri kwamba “tuko na ushirika wa maono ya mbele na Bw Nyoro pamoja na wengine wengi ambao tunaamini Taifa hili linahitaji fikira mpya za kulistawisha”.

Bw Owino alisema kwamba “mambo ni mengi yanayoendelea lakini yatakuja kujiweka wazi katika siku zijazo huku kukizuka msisimko wa ajabu”.

Bw Nyutu alisema kwamba “kunyamaza hapa kwa Mlima hakujamaanisha kitaifa tumezimwa na kwa sasa Bw Nyoro ako mbioni kuunda madaraja na wengine tukisubiri kipenga na ambapo tutaungana na wengine wengi kulipa Taifa hili na Mlima Kenya afueni dhidi ya udikteta”.

Wengine walio katika njama hiyo ni pamoja na Kinara wa Narc Kenya Bi Martha Karua, gavana wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru, kinara wa Usasa kwa Wote Bw Mwangi wa Iria, aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth na Mbunge maalum Bi Sabina Chege.

Bw Jeremiah Kioni ambaye ni mshirika wa Bw Kenyatta, Karua na wengine ndani ya Azimio alisema kwamba siku ya kiama inakuja na itatetemesha siasa za 2027.

“Tunajipanga na tunaongea na washirika wetu wa kisiasa na kifedha. Hatubagui yeyote bora tu ako na msimamo unaowiana na wetu kwamba ni lazima tujikomboe 2027 dhidi ya mtandao wa uongo na hadaa unaotawala kwa sasa,” akasema.

Wengine katika muungano wa kijamii walithibitisha kwamba njama hiyo inasukwa.

“Ni ukweli kwamba tunakimbizana na mdahalo wa kuungana kama Mlima. Mbinu mbadala ni kuungana na wengine na tupate muungano ambao umetuwakilisha vilivyo kinyume na hali ya sasa ambapo hatuna mkataba na serikali ya Rais Ruto,” akasema mwenyekiti wa Wazee wa Agikuyu Bw Wachira Kiago.

Katika mahojiano na kituo cha runinga cha Inooro TV, mbunge wa bunge la Afrika Mashariki Bw Kanini Kega na Seneta wa Nyeri Bw Wahome Wamatinga walidokeza kwamba kuna njama ya kuunda chama cha Mlima Kenya cha kutumika 2027.

“Tunafaa kuwa na chama chetu cha kutuongoza 2027. Hali hii ya kuwa ndani ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho hatuna ushawishi inatupeleka kombo,” akasema.

Hali hiyo imesemwa kuwa na nguvu kiasi kwamba serikali ya Rais Ruto imebabaika na ndio kujinusuru, Rais na Naibu wake wamekuwa wakitembea Mlima Kenya ili kujaribu kuthibiti hali lakini ukaidi ukizuka waziwazi katika mikutano yao na kuishia raia kuwakemea.

[email protected]

 

 

  • Tags

You can share this post!

Zamu ya wakulima kunyolewa kupitia ushuru  

Transfoma ya polo nusra ing’olewe na mbwa akijisaidia...

T L