Umuhimu wa kujiandikia kiapo cha ndoa
NA BENSON MATHEKA
BAADA ya kuvishwa pete, Leah Ambani, aliomba maikrofoni, akachukua karatasi iliyopigwa chapa kutoka kwa msaidizi wake, na kukariri shairi lililojaa sifa na ahadi tele kwa mumewe.
Jamaa, marafiki na wageni walioalikwa kushuhudia harusi yao walishangilia. Ilikuwa mara ya kwanza bi harusi kujisomea kiapo alichoandika katika kanisa hilo.
Enzi ambazo wanaharusi walikuwa wakizingatia utaratibu wa dini au jamii zao kubadilishana viapo vya ndoa zimefikia ukingoni huku watu wengi wakiamua kuandika viapo vyao wenyewe wakati wa harusi.
Idadi kubwa ya wachumba wanachagua kuandika viapo vyao wenyewe kinyume na enzi za awali ambapo watu walikuwa wakifuata viapo vilivyowekwa kama kanuni na dini zao.
Mabadiliko ya wakati na kuporomoka kwa mila na tamaduni za baadhi ya jamii kumechangia hali hii.
“Sio kwamba ni kupotoka. Dunia imebadilika mno huku watu wengi wakielimika. Ni dunia ambayo watu wanahitaji uhuru wa kujiamulia mambo na ndoa kama taasisi muhimu inafaa kuachiwa wahusika kujiamulia mambo ikiwa ni pamoja na kubadilishana viapo vyao wenyewe wakati wa harusi,” asema mshauri wa ndoa na mwelekezi wa sherehe za nikahi Bi Rose Muthoni.
Anasema hatua ya wachumba kuandika viapo vyao inafaa kwa sababu inampatia mhusika fursa ya kuelezea hisia zake za dhati kwa mwenzake.
“Kufuata kanuni za kidini au kimila kulikokuwa kukifanyika awali kuliwanyima wapenzi fursa ya kuelezea hisia zao kikamilifu.
Kuandika kiapo na kukisoma mbele ya wageni wakati wa harusi kunaongeza ladha ya huba,” asema na kuongeza kuwa enzi za wachumba kufuata kanuni za dini na madhehebu sasa zimepitwa na wakati.
Dini nyingi na madhehebu huwataka wafuasi wao kukariri viapo vilivyoandikwa na ambavyo vimekuwepo kwa miaka mingi, mtindo ambao hauwavutii watu wengi siku hizi.
Hata hivyo, Muthoni asema kuna baadhi ya dini zinazoshikilia kwa dhati kanuni za arusi na hazikubalii wafuasi wao kuandika viapo vyao wenyewe.
Wafuasi wa dini hizi wasiokubaliana na msimamo wa dini au dhehebu lao huamua kufunga ndoa chini ya usimamizi wa viongozi wa kiserikali .
Muthoni asema wanaoandika viapo vya ndoa hutumia maneno teule kuelezea hisia zao jambo ambalo baadhi ya dini zinapinga.
“Wengi hudondoa vifungu vya mashairi ya mapenzi, sinema na nyimbo wakielezea wanavyokusudia kuishi na kupamba ndoa yao. Kubadilishana viapo vya ndoa ni hatua inayokoleza utamu wa sherehe za ndoa na inafaa kuachiwa wapenzi kujieleza,” asema.
Bw Mike Okinyi, 28, aliyefunga pingu za maisha miezi sita iliyopita asema alimwelezea padre wake nia yake ya kuandika kiapo chake lakini akakataa katakata kusimamia harusi yao.
“Nilishauriana na mchumba wangu na padre wa kanisa lake alituruhusu kuandika viapo vyetu na akaongoza sherehe yetu ya ndoa,” asema.
Okinyi asema tofauti na viapo vilivyoandaliwa na dini au madhehebu, viapo vya kujiandikia vina uzito, vinaelezea hulka unazotamani kwa mwenzio na unayotazamia kutoka kwake katika maisha yenu ya ndoa.
“Fauka ya yote, vinaongeza ladha ya sherehe ya harusi,” asema.
Kauli hii inapigwa jeki na Bi Diana Kajuju, 32, anayesema kuwa mbali na kubeba ujumbe halisi wa mapenzi viapo vya kujitayarishia ni dhibitisho kamili ya huba.
Kajuju anasema aliandika viapo vyake na kufikia sasa vinamsaidia mno katika ndoa yake.
“Mimi na mchumba wangu tunapokumbuka tuliyoahidiana tunavumiliana. Kama tungetegemea kanuni za dini yetu huenda ndoa yetu ingetatizika,” asema.
Muthoni anaunga kauli ya dada huyu akisema utaratibu wa viapo unaowekwa na dini umeshindwa kuzuia mitafaruku katika ndoa.
“Ingawa lengo la viapo hivyo sio kudhibiti ndoa, nyingi ya zilizofuata kanuni za kidini husambaratika mapema na kuwafanya wapenzi kusononeka ingawa kulingana na dini waliapa kuishi pamoja hadi kifo kiwatenganishe. Ndiposa binafsi, nasisitiza dini zinazowazuia wapenzi kuandaa viapo vyao zibadilishe mtindo,” asema.
Kwa mujibu wa maelezo ya kamusi ya mtandao la Wikipedia, viapo vya ndoa ni maelezo mafupi, matamu yakuvutia.
Aidha, Wikipedia inasema mhusika anaweza kutayarisha tungo ndefu akielezea jinsi maisha yake yalivyobadilika alipokutana na mchumba wake.
Naye Bi Linda Bardes, anayejulikana kimataifa kama The wedding coach asema kwenye makala yaliyochapishwa katika tovuti ya weddingvowsandceremonies.com kwamba viapo vya ndoa hudumisha moto nikaha.
“Unaweza kuendelea kukariri viapo hivyo vya kujitungia kila wakati na kudumisha cheche za mahaba zikiwaka,” asema Linda.
“Ninaamini ndoa yangu ya miaka saba imeshamiri kwa kukumbuka viapo tulivyobadilishana wakati wa harusi. Tulijiandikia viapo hivyo na tunashukuru,” asema Leah Ambani, mkazi wa Nairobi, akiongeza kuwa vimefanya ndoa yake kuwa ya amani
Linda anasema kuandaa viapo vya ndoa kunahitaji mhusika kujielewa kwanza, ndoto zake na za mchumba wake na anayotaka kutimiza katika maisha ya ndoa.
“Katika kiapo chako, elezea ndoto zako, malengo uliyonayo, mahaba, masuala ya pesa, familia na hata nyumba ukizingatia hali ya mwenzako,” asema.
Muthoni na Linda wanakubaliana kuwa viapo vya kujiandalia vinachangia katika kukuza uhusiano kati ya mke na mume baada ya ndoa.
“Ukivisoma mara kwa mara baada ya ndoa, vinakuwa sehemu ya maisha yako. Unaweza kumkabili mchumba wako na kumwambia kwamba hivi ndivyo ulivyoniahidi uliponioa,” asema Muthoni.
Kulingana na mshauri huyu, mtindo huu wa wachumba kuandika viapo vyao umeshika kasi miongoni mwa wachumba walioelimika na unaashiria enzi ya mabadiliko makubwa katika maandilizi ya harusi.