Umuhimu wa tunda la Pitaya yaani Dragon fruit
Na PETER CHANGTOEK
TUNDA la pitaya au ‘dragon fruit’ ni nadra mno kupatikana katika maeneo mengi nchini Kenya.
Tunda lenyewe lina manufaa mengi ya kiafya, na ni wakulima wachache ambao hushughulika na uzalishaji walo nchini.
Pitaya huuzwa kwa bei kuanzia Sh1,000 kwa kilo, na kuna wakati ambapo lilikuwa likiuzwa kwa zaidi ya Sh2,000 kwa kilo moja, katika mojawapo ya madukakuu nchini, na wakati huo, matunda hayo yalikuwa yakitolewa nchini Vietnam.
Mmea wa pitaya ni wa familia ya mkangusi (cactus), na sehemu nyingi za mmea huo huliwa; maua, matunda, miongoni mwa nyinginezo.
Matunda ya mmea huo huliwa yanapoiva, au hutumika kutengeneza sharubati. Ladha ya tunda hilo inakaribiana na ya peasi lililochanganywa na tunda aina ya kiwi.
“Kilo moja ya pitaya huuzwa kwa Sh890. Ni familia ngapi wataweka hiyo kwenye bajeti zao? Kwa wakati huu, tunda hilo hupatikana tu katika supamaketi. Tusipochukua hatua ya kuzalisha kwa ajili ya familia zetu, litabaki tu kuwa tunda la wale wanaojiweza, licha ya manufaa ya kiafya ya tunda hilo,” anashauri Jennifer George, mzalishaji wa matunda hayo jijini Nairobi, ambaye pia huwahamasisha watu kuhusu manufaa ya tunda hilo.
Anthony Mugambi, amekuwa akishughulika na ukuzaji wa mmea huo kwa muda wa miaka mitano sasa, na ameonja matunda ya kazi yake.
“Kuna watu kadha wa kadha, ambao huweka oda hata kabla sijachuma shambani. Mimi huuza kilo moja ya matunda hayo kwa Sh1,000,” asema Mugambi, akiongeza kuwa matunda mawili au matatu yana uzani wa kilo moja.
Kwa mujibu wa Faith Ndungi, mtaalamu wa lishe katika Chuo Kikuu cha Egerton, ni kuwa, matunda ya pitaya lina manufaa mengi kiafya.
“Yana vitamin B1, B2, B3 na C, karotini, protini, kalisiamu, chuma, na fosiforasi,” asema, akiongeza kuwa, mbegu za tunda hilo zina madini aina ya Omega-3.
Mtaalamu huyo anadokeza kwamba, tunda hilo lina uwezo wa kuzuia maradhi ya saratani, maradhi ya moyo na shinikizo la damu.