Makala

Unaleta Katiba Day na uliipinga kwa refarenda? Wakenya wauliza Rais Ruto mitandaoni

Na CHARLES WASONGA August 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya Wakenya wamemtaja Rais William Ruto kama mnafiki kwa kutangaza Agosti 27 kuwa Siku ya Katiba (Katiba Day) ilhali aliongoza kampeni ya kupinga Katiba hiyo mnamo 2010.

Aidha, walisema ni kinaya kwa kiongozi wa taifa kuisifu Katiba hii ambayo serikali yake imetuhumiwa kuidharau, kuikiuka na kutoiheshimu.

Wengi wanataja matukio ya hivi karibuni ambapo maafisa wa polisi wamehusika katika vitendo vya ukiukaji wa haki za kibinadamu kama vile mateso, utekaji nyara na mauaji ya kiholela ya watu wanaosawiriwa kuwa wakosoaji wa serikali.

Aidha, utawala wa Rais Ruto umeelekezewa kidole cha lawama kwa kutoheshimu uhuru wa wanahabari na vyombo vya habari unaolindwa katika vipengele vya 33, 34 na 35 vya Katiba ya sasa.

Kwenye taarifa aliyotoa Jumatatu Agosti 25, 2025, Rais Ruto aliisifu Katiba hii iliyozinduliwa 2010 akiitaja kama “mojawapo ya ile iliyoletwa mageuzi na maendeleo katika historia ya binadamu.”

Kiongozi wa taifa alisema Katiba Dei itaadhimishwa kila mwaka kupitia shughuli za uhamasisho wa kiraia katika shule, asasi za serikali kuu na serikali za kaunti na katika mabalozi ya Kenya katika mataifa ya ng’ambo.

Kulingana na Dkt Ruto, Katiba Dei itawakumbusha raia kuhusu wajibu wao wa “kuzingatia, kutunza, kulinda na kutekeleza Katiba hii.”

Lakini wakosoaji kupitia mtandao wa kijamii walimkumbusha kwamba mnamo 2010, wakati wa kampeni za kura ya maamuzi kuhusu katiba hii, aliipinga kwa nguvu zake zote.

Huku akiongoza kambi ya “LA”, Dkt Ruto alidai kuwa katibu hiyo ilihalalisha uavyaji mimba, ushoga na sera za kuwanyima raia haki zao za umiliki wa ardhi.

Wakili Willis Otieno akauliza kupitia akaunti yake ya X: “Ni vipi unasherehekea Katiba ambayo ulipinga. Mbona unasherehekea katiba ambayo hauheshimu?”

Kwa upande wake wakili na mkereketwa wa chama cha Democracy for the Citizens’ Party (DCP) Ndegwa Njiru akaeleza: “Ni ajabu kwamba mtu ambaye alipinga Katiba hii sasa anajifanya kuwa mtetezi wake sugu. Hauwezi kuchafua kitabu kwa miaka 15 kisha ghafla unajitangaza kwa mtetezi wake.”

Lakini mtaalamu wa masuala ya uongozi na utawala Barasa Nyukuri anajibu kwa kusema kuwa Rais Ruto kama kiongozi wa taifa anajipata katika hali ambapo ni sharti atetee katiba ya sasa ambayo aliapa kulinda na kuitunza.

“Kwa kutangaza Agosti 27 kama Katiba Dei, Rais Ruto anatekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa sababu, kando na kwamba aliipinga Katiba hii 2010, mnamo Septemba 13, 2022 aliapishwa kwayo. Kwa hivyo, ni sharti aitetee kwa vyovyote vile,” Bw Nyukuri anaeleza.

Lakini Wakenya waliendelea kushikilia kuwa utawala wa Dkt Ruto haujadhihirisha kwa vitendo kwamba unaheshimu Katiba hii.

“Serikali hii ya Kasongo imekuwa ikikiuka Katiba hii kwa kudharau maamuzi ya mahakama, inahujumu ugatuzi kwa kuchelewesha utoaji wa mgao wa fedha kwa serikali za kaunti, unaendeleza visa vya dhuluma dhidi ya wakosoaji wake na waandamanaji huku ikiteka Bunge,” akasema Brian Maina, mwanaharakati na mwanachama wa Bunge la Wananchi, tawi la Bustani ya Jevanjee, Nairobi.