Unga wa watoto uliochakatwa wavutia masoko ng’ambo
EDWIN Mairo na Everlyne Alpha ni wajasiriamali wenye hadithi ya kuvutia, ambapo safari yao kuzindua kampuni ya kuchakata unga ilianza kwa uchuuzaji.
Wawili hao ndio waasisi wa Gemini Flour Mills, kampuni ya kusindika mseto wa unga iliyoko Changamwe, Kaunti ya Mombasa.
Ilizinduliwa mwaka 2017, Mairo akifichua kwamba walianza kwa kuchuuza unga.
“Tulikuwa tukichuuza unga wa nafaka mbalimbali kwenye mitaa ya mabanda, na hatimaye tukagundua familia nyingi watoto wao wameathirika na kero ya Utapiamlo,” anasema.
Gemini Flour Mills husiaga nafaka kama vile wimbi, mtama, maharagwe ya soya, mbegu za mchicha (maarufu kama terere), na kwa sasa wanaendeleza utafiti wa kuchanganya unga wa mchele, majani ya terere, kunde na kamande (fortified flour).
Hatua hiyo imetokana na masoko ya nje ya nchi waliopata kupitia mdhamini.
Fortified flour, ni unga wa mseto wa nafaka zenye madini na virutubisho mbalimbali.
“Tumepata kandarasi na Shirik Lisilo la Kiserikali (NGO) kusindika nafaka hizo, ili wasambaze mchanganyiko wake Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC), Sudan na sehemu kadha nchini Kenya,” Mairo anadokeza.
Maeneo yanayolengwa ni yenye visa vya watoto kuugua Utapiamlo, kwa sababu ya janga la njaa na ukame.
Utapiamlo, ni mojawapo ya kero inayoathiri watoto wa maeneo kame nchini (ASAL) kufuatia uhaba wa chakula na ukosefu wa mlo wenye virutubisho na madini faafu.
Kulingana na Shirika la Takwimu Kenya (KNBS), Utapiamlo ni changamoto kuu nchini ambapo data zake zinaonyesha kwa idadi milioni 7 ya watoto wenye chini ya umri wa miaka 5, milioni 1.82 kati yao (sawa na asilimia 26) wanaugua maradhi hayo.
Aidha, ugonjwa huo unaathiri uwezo wao kukua.
Kampuni ya Mairo na mwanzilishi mwenza ikiwa ilisajiliwa rasmi 2019, anakiri sasa inawika eneo la Pwani hasa katika Kaunti ya Kilifi na Kwale.
Cha kutia moyo, ni kwamba anahudumu na wakulima wanaokuza nafaka anazotumia, hatua ambayo imewapa afueni dhidi ya kero ya kusaka soko.
Isitoshe, wameondolewa mahangaiko yanayochochewa na mabroka na mawakala.
Anahudumu na idadi isiyopungua wakulima 1, 600.
Wengi wao, ni wakulima wa mashamba madogo na ya kadri.
Ni kutokana na jitihada zao, Gemini Flour Mills ilikuwa miongoni mwa wajasirimali waliopata fursa kushiriki Maonyesho ya Sankalp Barani Afrika 2024, makala ya 11 Jijini Nairobi.
Aidha, kampuni hiyo ilishiriki kupitia ufadhili wa Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) na Scaling Up Nutrition Business Network (SBN).
Kauli mbiu ya maonyesho hayo ilikuwa ‘Kupiga jeki Ujasirimali Barani Afrika ili Kuwahi Maendeleo ya Kimataifa’.
GAIN na SBN, ndio wameshika mikono vijana hao.
Idadi kubwa ya wakulima Mairo na Alpha wanahudumu nao ni wanawake (asilimia 58), huku vijana wakiwa asilimia 40, na kiwango kilichosalia kikiwa ni wazee.