Unyama wa kutisha: Takwimu zaonyesha kila watoto 10 Gusiiland, watatu wamedhulumiwa kimapenzi
INGAWA uhamasishaji mkubwa umetolewa dhidi ya unyanyasaji wa kingono, visa vya watoto kudhulumiwa kingono katika eneo pana la Gusii lingali donda sugu.
Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa zaidi ya watoto 7,200, hudhulumiwa kingono na kulawiti kila mwaka na wataalam hao wanaamini kwamba kesi nyingi zaidi haziripotiwi.
Visa vya unyanyasaji wa kingono kwa watoto katika kaunti za Kisii na Nyamira vinazidi kuongezeka.
Unapotembelea Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH) na kuuliza kuhusu kesi ngapi za unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wanazoshughulikia kwa siku moja, utashangazwa na takwimu utakazopewa.
Kwa kawaida hospitali hiyo hupokea angalau visa visivyopungua kumi kila mwezi. Wengi wa watoto hawa ni kati ya umri wa miaka 7-12.
Inakadiriwa kuwa takriban asilimia 30 ya watoto katika Kaunti ya Kisii wananyanyaswa kingono angalau mara moja katika maisha yao. Hii ina maana kuwa watoto 3 kati ya 10 katika Kaunti ya Kisii aidha hunajisiwa au kulawitiwa.
Jambo la kuchukiza zaidi kuhusu unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto katika Kaunti ya Kisii ni kwamba mara nyingi, mhalifu huwa ni mtu wa karibu anayejulikana vyema na mwathiriwa.
Mfano wa visa viwili
Ili kukudadavulia hali ilivyo, ‘Taifa Leo’ inatoa mfano wa visa viwili vya hivi punde kuwahi kutokea katika kaunti za Nyamira na Kisii.
Oktoba mwaka jana, msichana wa miaka 9 katika kijiji cha Sironga, eneobunge la Mugirango Magharibi alinajisiwa na fundi wa kushona viatu.
Janadume hilo lenye umri wa miaka 40, linasemekana kumshawishi mtoto huyo kwenda kwa nyumba yake baada ya kumwahidi kuwa lingempa pipi amumunye.
Msichana huyo alikuwa ametumwa na mamake akamchukulie kiatu chake alichokuwa amepelekewa kukishona.
Jamaa huyo ni jirani wa mwathiriwa na anamfahamu vyema mtoto huyo kwa kuwa mama yake kwa miaka mingi amekuwa mteja wake kwani wao humpelekea viatu awashonee vinapokatika au kutoboka.
Msichana huyo alipopelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Nyamira, madaktari huko walithibitisha majeraha mabaya aliyoachiwa msichana huyo katika sehemu zake za siri.
“Msichana huyu alipata majeraha mabaya na anafuja damu. Imebidi afanyiwe upasuaji kuzuia ufujaji huo,” Dkt Angella Ogendi, mmoja wa wahudumu katika hospitali hiyo aliiambia Taifa Leo wakati huo.
Isingalikuwa ni maafisa wa polisi waliofika haraka, mshonaji viatu huyo asingalikuwa anaishi kwani wanakijiji waliojawa na hasira baada ya kufahamishwa kuhusu kitendo alichokifanya, walikuwa ange kumteketeza.
Wiki mbili baada ya tukio hilo, msichana mwingine wa umri wa miaka 13, kutoka mtaa wa Nyankongo, vyungani mwa mji wa Kisii alipitia masahibu sawia na hayo.
Mwanafunzi huyo wa darasa la tano, katika shule ya msingi ya Nyambera, anasemekana kunajisiwa na binamu yake aliye na umri wa miaka zaidi ya 30.
Inasemekana, jamaa huyo alitumia fursa ya mama ya mtoto huyo kutokuwa nyumbani kutekeleza uovu huo kwani alikuwa ameenda kanisani.
Hajiwezi kutembea
Mama huyo ambaye hajiwezi aliporudi nyumbani, alipata msichana wake hajiwezi kutembea na mara moja alipiga ripoti kwa maafisa wa usalama vijijini maarufu kama, ‘Nyumba Kumi’, wenye afisi zao mjini Kisii.
Cha kushangaza ni kwamba, baada ya ‘Nyumba Kumi’ kumkamata mshukiwa huyo na kumpokeza kwa maafisa wa polisi, jamaa huyo aliachiliwa katika mazingira tata. Hilo liliwafanya mama huyo na Nyumba Kumi hao kuamini kwamba maafisa fulani wa polisi walikuwa wamepewa “Kitu Kidogo” kumwachilia mwanaume huyo.
Iliwalazimu Nyumba Kumi hao kuzuru kituo cha polisi cha Nyanchwa kusaka majibu jinsi mshukiwa huyo alivyoachiliwa.
Mtoto aliyedhulumiwa alikuwa na matatizo kutembea au hata kupanda gari lililowapeleka kituoni Nyanchwa. Kila alipojaribu kusongesha miguu ili kupiga hatua za kutembea, alichora makunyanzi usoni mwake, ishara kwamba alikuwa akihisi uchungu mwingi.
Ripoti ya Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Uhalifu (2018-2022), ilionyesha kuwa unyanyasaji wa jumla wa watoto kingono katika Kaunti ya Kisii ni zaidi ya asilimia 30, ambayo inajumuisha unajisi kwa asilimia 11.8.
Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa unajisi ambao hapo awali ulikuwa wa asilimia 18.35 uliongezeka hadi asilimia 25 katika Kaunti ya Kisii mwaka wa 2020.
Kaunti ya Nyamira, mambo ni mabaya hata zaidi. Ripoti hiyo ilionyesha kwamba asilimia ya watoto walionajisiwa mwaka 2020 ni 69.4.
Mtetezi wa haki za watoto kutoka kaunti ya Nyamira Bi Hyline Mogambi, anasema aghalabu waathiriwa wengi katika visa hivi hawapati haki kwa kuwa ufisadi mkubwa umekithiri idara za polisi na mahakama.
“Inasikitisha kuwa afisa wa polisi anaweza kupokea hongo ili aachilie mshukiwa anayemharibu mtoto mchanga. Huwa najiuliza hivi, afisa huyo anayechukua hongo iwapo siku moja mtoto wake ndiye atakayedhulumiwa kingono, je atahisi vipi?” Bi Mogambi akasema.
Haribu mwanawe
Pia anaongeza kwamba, wakati mwingine inapotokea kuwa baba ndiye ameharibu mwanawe, familia hiyo hujaribu kunyamazia swala hilo kwa kuwa watahofia kusemwa vibaya katika jamii.
Kulingana na Bi Mogambi, wakati mwingine mambo hayo humaliziwa kichini chini katika korti zinazofahamika vyema kama Kangaroo courts.
Mwanaharakati huyo anahoji kuwa mara nyingi, baadhi ya machifu ndio huamua kesi katika korti hizo za Kangaroo. Maamuzi yao mara nyingi, hayampatii mwathiriwa haki na mhalifu atakapoona hakuna adhabu kali aliyopewa, atazidi kufanya uovu kama huo mara kwa mara.
“Badala ya kuripoti kisa kama hicho kwa polisi au hata maafisa husika, utapata mama akifunika uovu wa bwanake kwani atahofia atafukuzwa katika hilo boma ikiwa ataripoti,” Bi Mogambi anaongeza.
Mshikadau huyo anahoji kuwa ni vyema kuripoti kisa chochote cha dhulma dhidi ya watoto na anahisi kwamba, uhalifu kama huo utamalizwa ikiwa wanaoutekeleza watapewa adhabu kali kama vile kutumikia vifungo vikubwa gerezani.