Unywaji wa pombe unachochea saratani ya ini- ripoti
WAKENYA wasiopungua 2,237 wenye umri kati ya miaka 15 na 85 watapoteza maisha yao kila mwaka kufikia 2050 kutokana na saratani ya ini inayosababishwa na ongezeko la ubugiaji pombe kwa wingi nchini, inaashiria ripoti mpya.
Takwimu zilizotolewa na Shirika la Lancet zinaonya kwamba saratani ya ini, ambayo ni ya tatu hatari zaidi kwa maradhi yote ya saratani, itaangamiza mamia ya watu endapo visababishi vinavyoweza kuzuiwa havitaangaziwa.
Saratani ya ini (HCC) tayari ni kero kubwa nchini hususan kwa wanaume wenye umri wa miaka 40, kulingana na shirika la Amerika, US Library of Medicine.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa kuhusu Saratani Nchini, Dkt Elias Melly, alithibitisha ripoti hiyo Ijumaa akieleza Taifa Leo kuwa masuala yanayochochea saratani ya ini nchini yanatokana na maradhi ya ini, Hepatitis B na C na kemikali sumu.
Kulingana na data ya serikali aliyotuma Dkt Melly, saratani ya ini iliorodheshwa nambari 11 miongoni mwa saratani hatari zaidi nchini 2022 ikichangia visa vipya 833 na vifo 819 huku ikiathiri watu 1,372 kwa kila 100,000 (asilimia 2.4) kwa miaka mitano.
Hata hivyo, saratani ya ini inageuka kwa kasi kuwa tishio kuu zaidi nchini.
“Kumekuwepo ongezeko la visa vya ini. Tutachapisha hivi karibuni data kamili kuhusu saratani zote, ambayo siwezi kutoa kwa sasa, lakini bila shaka, ongezeko la visa vya saratani linahofisha mno ikilinganishwa na ilivyokuwa 2022,” Dkt Melly alieleza Taifa Leo.
Ripoti mpya ya Lancet inaonyesha kuwa kote duniani, visa vya saratani vitaongezeka karibu maradufu kufikia 2050, na kuwaua takriban watu 1.37 milioni ifikapo katikati mwa karne hii iwapo masuala kama vile uzani kupita kiasi, pombe na hepatitis hayatasuluhishwa.
Ripoti imefichua kuwa kwa sasa Afrika ina visa 73,844 vya saratani ya ini idadi inaoyokadiriwa kuongezeka kwa asilimia 30.2 ifikapo 2050, kumaanisha idadi ya visa haitapungua kila mwaka katika kipindi cha miaka 25 ijayo.
Watafiti wanasema unywaji pombe – ambao ni chanzo kikuu – unakadiriwa kusababisha zaidi ya asilimia 21 ya visa vyote vya saratani ya ini kufikia 2050, ongezeko la asilimia mbili kutoka 2022.
“Saratani ya ini ni ya sita kwa ongezeko na ya tatu kwa kusababisha vifo vinavyohusiana na saratani ulimwenguni.
Idadi ya visa vipya vya saratani ya ini vitaongezeka karibu maradufu kutoka 0.87 milioni 2022 hadi 1.52 milion 2050, iwapo mkondo uliopo sasa hautabadilika,” ilisema Lancet.
Wanasayansi wanasema kwa kuzingatia kiwango cha unywaji pombe kwa sasa nchini na duniani, visa vipya vya saratani – ugonjwa wa tatu kuua watui – vitaongezeka hadi kufikia 1.52 milioni kila mwaka kutoka 870,000 ikiwa hali ilivyo sasa itaendelea.
TAFSIRI: MARY WANGARI