Makala

MATUNDA: Uongezaji thamani unasaidia kuepuka kero ya mawakala

October 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

HATUA ya serikali mwaka huu kutia saini mkataba na ile ya China, Kenya kuuza maparachichi yake nchini humo ilipokelewa kama shangwe na wakulima wanaozalisha matunda hayo.

Hapa nchini, sekta ya kilimo ni mojawapo iliyovamiwa na mawakala, ambao wanaendelea kutuhumiwa kuharibu soko. Kuanzia ukuzaji wa mboga haswa kabichi, viazi, karoti na mahindi, ni mazao ambayo wakulima wake wanaendelea kulalamikia kero ya mawakala.

Kenya pia ni tajika katika ukuzaji wa matunda kama maparachichi, maembe, machungwa, karakara, matundadamu almaarufu tomarillo, ndizi, mapapai, matikitimaji, miongoni mwa mengine. Mkataba kati ya Kenya na China, Kenya kupata soko la maparachichi nchini humo ni afueni kwa wanaokuza matunda hayo.

Kwa kuwa China ni taifa lililoimarika kimaendeleo na kiteknolojia, si ajabu maparachichi tunayowauzia yakaongezwa thamani halafu bidhaa zitokanayo nayo tukazinunua.

Kwa hakika, ni jambo tunalopaswa kujifunza kama taifa lililojaaliwa na ukwasi mwingi utokanao na sekta ya kilimo. Kikwazo cha kutafuta soko la maparachichi pia avocado, kinaonekana kutatuliwa na China, lakini ni muhimu kukumbuka Kenya inazalisha matunda mengi.

Ukizuru mengi ya masoko utaona matunda yaliyooza yametapakaa, pengine kwa sababu ya ukosefu wa soko au vifaa maalumu kuyahifadhi yakiwa freshi.

Hilo si tofauti na taswira iliyoko shambani. Si ajabu, ukakuta mkulima akiyalisha mifugo kwa sababu ya ukosefu wa wateja. Mbali na matunda, wakulima wa kabichi, viazi na karoti, si mara moja au mbili wameskika wakilisha mazao yao mifugo.

Kizungumkuti hicho kimechochewa na mawakala wanaoyanunua wanavyotaka, mkulima akikokotoa hesabu ya gharama aliyotumia kuyazalisha anaona ni heri ayalishe mifugo wake au yaozee shambani.

Isitoshe, ni wachache mno wenye vihifadhio kama vile majokofu.

Ili kukwepa changamoto hizo zote na hasara, wanahimizwa kukumbatia mfumo wa kuongeza mazao thamani. Hata ingawa hatua hiyo ina gharama yake, ni nafuu ikilinganishwa kutupa mazao mara kwa mara, au kuyaacha yaoze.

Awali Daniel Kiboi ambaye ni mkulima wa matundadamu kaunti ya Nyeri alihangaishwa na suala la soko.

“Si siri, soko limeshikwa mateka na mawakala ambao wameharibu bei kupindukia. Kilo moja ya Tree tomato (matundadamu) wakati mwingine ilikuwa ikinunuliwa Sh50, usisahau nimeyasafirisha hadi Nairobi. Bei hiyo ni hasara tupu,” aeleza Bw Kiboi.

Hata hivyo, mkulima huyo aliondokea kero hilo baada ya kutathmini njia mbadala, akaafikia kufungua kiwanda. Ilimgharimu mtaji wa Sh3 milioni kufanikisha shughuli hiyo, ambapo huongeza matundadamu thamani kwa kuunda jemu na sharubati.

Isitoshe, Kiboi sasa ana wakulima wanaomuuzia matunda hayo kutoka kaunti hiyohiyo ya Nyeri, Kirinyaga na Laikipia. “Kilo moja ya tomarillo ukiiongeza thamani haipungui Sh400,” asema.

Ingawa David Karira, mkulima wa matunda hayo Nyeri hahangaiki kutafuta soko, anasema wakati mwingine hulazimika kusuburi malipo kwa muda wa zaidi ya wiki mbili. “Wengi wa wafanyabiashara ninaowauzia hunilipa baada ya kuyauza,” aeleza Bw Karira.

Ili kuepuka changamoto za aina hiyo, Daniel Kiboi anamshauri Karira kutathmini suala la kuyaongeza thamani. “Atagundua kuyaongeza thamani kuna faida kuliko kuyauza moja kwa moja. Pia, atapata wakulima wateja wengi na kubuni nafasi za ajira,” amhimiza.

Ufunguzi wa kiwanda chake ulihusisha halmashauri ya ujenzi (NCA), iliyoidhinisha kilipojengwa na ya mazingira; Nema.

Kiboi pia anasema mmoja anahitaji kupata kibali cha biashara kutoka kwa serikali ya kaunti. Vilevile, shirika la kutathmini ubora wa bidhaa, Kebs sharti lishirikishwe, na ni hatua aliyotekeleza mjasirimali huyo.

Harry Thuku, mtaalamu, anasema wakulima wanaweza kuungana kwa makundi au kupitia vyama vya ushirika (Sacco), ili wafanikishe ujenzi wa kiwanda cha kuongeza mazao thamani. “Ujenzi wa viwanda ni mojawapo ya ajenda nne kuu za serikali, hivyo basi wakulima wanahimizwa kuungana ili kusaidia kuifanikisha,” ashauri Bw Thuku.

Kulingana na mdau huyu, suala la mazao kuharibikia shambani hasa msimu wa mvua kubwa, kuoza kwa sababu ya kukosa soko na kulishwa mifugo kwa ajili ya kero ya mawakala, itapungua pakubwa endapo wakulima watakumbatia mfumo wa uongezaji thamani.

Pia, bidhaa zilizoongezwa thamani zina soko au malipo bora.