Makala

Upekee wa kabati la Mswahili

February 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

MSWAHILI asili yake ni Pwani.

Huyu ni mja aliyefungamana na tamaduni za kipwani ambazo sanasana ni Uislamu na tamaduni za Kiarabu na Kiajemi, ambaye pia lugha yake mama ni Kiswahili.

Aghalabu Mswahili hutumia lugha ya Kiswahili kama kielezeo cha utamaduni wake.

Kimsingi, Mswahili pia anaweza kuelezwa kama mtu mahuruti-yaani ni mtu chotara ambaye ni lazima awe ametokana na mwingiliano wa pande mbili ambao ni Wabantu na watu wanaonasibishwa na Waarabu.

Ikumbukwe kuwa katika siku za hivi karibuni dhana ya “Mswahili ni nani?” imejadiliwa kwa upana na wanataalama mbalimbali kwani imekuwa tata si haba.

Utata wote unatokana na kigezo kwamba kuna watu wasio ‘Waswahili’ lakini wanaizungumza kwa ufasaha lugha ya Kiswahili ilhali pia kuna ‘Waswahili’ wenyewe.

Kutokana na hilo, Mswahili pia ameelezewa kuwa mtu mwenye kiwango kikubwa cha umilisi wa lugha ya Kiswahili.

Vilevile , ni mtu ambaye amefungamana sana na mila na desturi za jamii ya watu watumiayo lugha ya Kiswahili kiasi hata cha kumuathiri kifikira, kimtazamo na kiitikadi.

Yaani Mswahili anaweza kuwa ni mtu ambaye anazungumza vizuri lugha ya Kiswahili kwa kufuata taratibu zote za kiisimu na utamaduni wa lugha ya Kiswahili.

Tangu jadi, Waswahili wametambulika kuwa washirika wenye nguvu sawa na wafanyabiashara wa Kiarabu, Waajemi na Wahindi.

Mbali na dini na lugha, wakazi hawa wa Pwani huwa na muundo wa kijamii unaofanana.

Miongoni mwa mambo hayo ni jinsi wanavyopenda starehe au kuishi maisha ya hadhi, hasa majumbani mwao.

Ni kwenye nyumba ya Mswahili kuna vitu ambavyo katu huwezi kuvikosa.

Miongoni mwa vitu hivyo ni kabati.

Kabati ni samani au aina ya sanduku kubwa la wima linalotengenezwa kwa mbao, chuma au bati.

Watu hutumia kabati au sanduku kuhifadhia vitu kama vile nguo, vyombo au mafaili.

Aidha kwa Waswahili halisi, wao hawakuwa na kabati, ila chombo chao sawia walichotumia kutwa nafasi ya kabati ni kasha.

Kasha ni sanduku kubwa gumu linalotumiwa kuwekea mali, ikiwemo dhahabu, nguo na vyombo vingine vya thamani.

Kulingana na Mzee Mswahili wa Lamu, ambaye pia ni kiongozi wa dini ya Kiislamu, Ustadh Mahmoud Abdulkadir Mau, kasha la Mswahili hutengenezwa kwa njia ya kipekee kwani hata mti unaotumiwa huwa wa thamani kubwa na imara.

Mzee Mswahili wa Lamu na kiongozi wa dini, Ustadh Mahmoud Abdulkadir Mau. Asema makabati na makasha ya sasa yapatikanayo kwa nyumba za Waswahili sio halisi bali yale ambayo yametawaliwa na muigo wa jamii nyingine, hasa Wahindi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema upekee mwingine wa kabati au kasha la Mswahili ni jinsi linavyokolezewa nakshi au urembo na kulifanya kupendeza na kuvutia kwa macho si haba.

Anasema thamani ya kasha au kabati la Mswahili pia huwa ni ya juu mno.

Utapata kasha au kabati la Mswahili likiuzwa miaka hiyo ya jadi kwa fedha zisizopungua kati ya Sh50,000 na Sh100,000.

Anasema kasha au kabati la Mswahili pia halikukosa kioo, ambapo wanawake hutumia kujiremba kabla ya kuanza shughuli za siku.

Kabati na kitanda miongoni mwa samani nyingine za kisasa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Ustadh Mau aidha anataja makabati au makasha yanayotumiwa na Waswahili wa leo kwamba sio yale kindakindaki.

“Hizi kabati au kasha za leo uzipatazo kwenye nyumba za Waswahili sio zile halisi tuzijuazo. Samani hizi za leo, iwe ni kabati, kasha au hata vitanda zimeathiriwa sana na tamaduni za Kihindi au Wahindi. Ila kabati za Waswahili wa jadi huwa ni za mlango mmoja tu au wakati mwingine miwili. Kabati ya Mswahili ni yenye kutiwa nakshi au mauamaua ili kuleta urembo,” akasema Bw Mau.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu na Mswahili, Bw Mohamed Shee Mbwana, anasema kinyume na miaka ya sasa, samani nyingi za Waswahili, hasa kabati au kasha zilikuwa zikitengenezwa kwa miti maalum na inayovuma kwa kuwa na mbao ngumu, ikiwemo mbambakofi, msaji na msinga.

“Makabati ya leo yamewekwa kwa nyumba za Waswahili ambazo ni za kileo tu zilizojaa athari za ulimwengu wa Kimagharibi. Ila kabati kindakindaki la Mswahili huwa na mlango mmoja na mbao ni ngumu. Huwa mbao zimechongwa na kuwa na nakshi asilia. Ugumu wa mbao ndio uliwawezesha Waswahili kuhifadhi vitu vya thamani kama vile dhahabu na pesa kwani makasha yalikuwa sawa na sefu. Mti uliotumika haukuwa ni wenye kuharibika kwa urahisi,” akasema Bw Mbwana.

Bi Fatma Athman wa Lamu, anafafanua kuwa kabati au kasha lilikuwa likiwekwa sebuleni pia likitumika kama pambo katika nyumba kutokana na urembo wake uliokoleza au kusheheni.

“Kasha au kabati zetu zilikuwa muhimu sana kwa nyumba. Mababu zetu na sisi wenyewe tulitumia kuhifadhi na kutunza nguo, kuweka vyombo nakadhalika. Utapata leo watu wakitumia kabati kuwekea televisheni au runinga.

Mbali na kabati na kasha, vitu vingine vya kimsingi ambavyo katu huwezi kuvikosa kwa nyumba ya Mswahili kindakindaki ni kitanda cha usutu au mwakisu. Hiki ni kitanda ambacho hutengenezwa au kuwambwa kwa kamba kama vile za miyaa, shupatu au ngozi.

Kitanda cha Mwakisu kikiwa ndani ya nyumba ya makavazi ya Waswahili kisiwani Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU