Makala

USAFI: Jinsi ya kukitunza kinywa chako

March 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

PENGINE umeshawahi kuongea na mtu na ukajikuta unakosa hamu ya kuendelea sababu kinywa kinatoa harufu mbaya.

Kinywa ni muhimu kufanyiwa usafi wa hali ya juu ili kuhakikisha unapunguza na hata kumaliza kabisa harufu mbaya.

Kwa bahati mbaya, huwa hatujui kama midomo yetu inatoa harufu mbaya.

Hii inakuwa vigumu kutatua tatizo sababu unaweza kudhani uko sawa kumbe unawapa watu wakati mgumu mnapozungumza.

Harufu mbaya haifurahiwi, hasa ikiwa inatoka kwenye vinywa vyetu.

Kutosafisha vizuri kinywa vizuri

Kwa kawaida unatakiwa kusukutua kinywa chako angalau mara mbili kwa siku; asubuhi na usiku kabla ya kulala.

Wakati wa kusafisha kinywa, hakikisha umesugua vizuri ulimi. Ulimi ndiyo sehemu kubwa ambapo bakteria wanajistawisha.

Vilevile, ni ulimi unaosababisha kinywa kunuka. Ni vizuri kama utasafisha vizuri ulimi ili kuondoa harufu mbaya. Badilisha mswaki angalau kila mwezi.

Kutokula chakula vizuri

Harufu ya kinywa inaashiria kutokula chakula na kinywaji kwa muda mrefu.

Kuwa na njaa husababisha mdomo kuwa mkavu. Mara nyingi harufu mbaya ya kinywa hupotea mara tu baada ya kula chakula kizuri na mdomo ukiwa una mate ya kutosha.

Ni muhimu kuepuka vyakula na vinywaji vinavyoongeza harufu kali mdomoni na kukupunguzia maji mwilini; mfano pombe, viungo kama kitunguu maji au kitunguu saumu.

Kinywa kikavu

Bakteria huishi kwenye kinywa kikavu. Kama hupendi kunywa maji mengi na kinywa chako kinakuwa kikavu mara nyingi basi jua kuwa kunuka kinywa kwako ni jambo la kawaida.

Hakikisha mdomo haukauki

Kwa kawaida mdomo mkavu hutoa harufu mbaya. Hii ndio sababu kuwa kinywa chako kinanuka sana asubuhi sababu mdomo wako unatengeneza mate machache sana ukiwa umelala. Mate ni adui wa harufu mbaya mdomoni sio tu kwa sababu yanaondoa bakteria na masalia ya chakula, bali mate yana vimengenyo vinavyoua na kuzuia kuzaliana kwa vijidudu kwenye kinywa. Ili kuzuia kunuka, jaribu kufanya haya:

  • kunywa maji mengi ili kuondoa ugaga na mabaki ya chakula na bakteria
  • piga mswaki kabla ya kulala
  • kula ndizi au tufaha
  • kula tango
  • harufu ikizidi, muone daktari au mtaalamu wa afya ya meno na kinywa kwa jumla.