Makala

Usajili wa nyumba za bei nafuu Mukuru waingia awamu ya pili

Na WINNIE ONYANDO September 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

USAJILI wa nyumba za bei nafuu umeingia awamu ya pili katika makazi ya mabanda ya Mukuru.

Haya yanajiri miezi minne tu tangu Rais William Ruto kupeana nyumba 1,080 za kwanza chini ya mradi wake wa Nyumba Nafuu Mukuru.

Zoezi hilo la usajili lilianza Jumatatu katika wadi ya Nairobi South likilenga takribani wakazi 2000 kutoka mitaa ya mabanda ya South B.

Usajili huo unaongozwa na Ruth Wekesa wa Bodi ya Makazi ya Bei Nafuu pamoja na diwani wa eneo hilo, Bi Waithera Chege. Katika awamu hii, nafasi 4,500 zitatolewa kwa waliotuma ombi la kumiliki nyumba hizo awali kutoka maeneo ya South B na Imara Daima.

Diwani wa Nairobi Kusini Bi Chege aliwahimiza wakazi wa eneo lake kukumbatia mpango huo kwani utawasaidia kumiliki nyumba kwa urahisi.

Diwani wa Nairobi Kusini Bi Waithera Chege na Ruth Wekesa wa Bodi ya Makazi ya Bei Nafuu wakiwahutubia wakazi wa Nairobi Kusini. PICHA|WINNIE ONYANDO.

Baadhi ya wanufaika waliokuwa wakihudhuria usajili huo walipongeza hatua hiyo wakisema imebadilisha maisha yao kutoka makazi duni ya mabanda hadi nyumba za kisasa na zenye heshima.

Kando na hayo, wakazi waliohudhuria zoezi hilo pia walipata nafasi ya kuuliza maswali moja kwa moja kutoka kwa maafisa wa makazi.

Usajili huo utafungwa leo, (Septemba 16,2025) na utafunguliwa tena kesho (Jumatano) kwa wale watakaotaka kumiliki nyumba hizo.

Serikali imetangaza kuwa kuanzia Januari mwaka ujao, itaanza kujenga na kupeana nyumba ya chumba kimoja na viwili katika awamu inayofuata ya mradi huo.

Akipeana nyumba hizo 1,080 Mai 25, 2025, Rais Ruto alisema kuwa, “Nataka kuwaambia wakazi wa Mukuru, mna furaha lakini mimi hata ndio nina furaha zaidi kwa sababu ndoto yangu imetimia. Ndoto ya kuinua maisha ya watu wa chini, niwaweke juu. Hii ndio siku muhimu zaidi katika maisha yangu ya kisiasa.”

Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Nyumba Nafuu Sheila Waweru wakati huo alisema nyumba zote zipo wazi kuchukuliwa kupitia kwa mpango wa ulipaji wa muda mrefu ambao unaruhusu wanunuzi kulipia kwa viwango vidogo kwa muda wa miaka 30.

Awali, Bi Waweru, alitoa wito kwa Wakenya kuchangamkia mpango mpya utakaowawezesha kumiliki nyumba za bei nafuu kwa urahisi.