Ushahidi tata katika kesi ya urithi wa mali ya bwanyenye wa Pelican Signs
NDUGUYE bwanyenye Balkrishna Ramji Maribhai Devani, Hasmukh Jumanne Januari 27, 2026 aliikabidhi Mahakama ya Milimani Wosia asili wa ndugu alioapa Juni 3, 2019 siku nne kabla ya kuaga dunia katika hospitali ya Aga Khan, Nairobi.
“Huu ndio Wosia niliopewa na kampuni ya mawakili ya Dally & Inamdar Juni 19, 2019 na naukabidhi hii mahakama kama ushahidi katika hii kesi,” Hasmukh alimpa hakimu nakala ya Wosia wa ndugu yake.
Hasmukh alimfafanulia hakimu mwandamizi Rose Ndombi kwamba ndugu yake aliwagawanyia binti zake watatu mali yake iliyojumuisha mamilioni ya pesa kweney benki za nchini na ng’ambo, makampuni yake yaliyomo Nairobi na Limuru.
“Ndugu yangu aliwapa bintize mali zake na wala hakuwapa wafanyakazi Samuel Ndinguri na Addah Nduta kama inavyodaiwa na Dinta Devani, Ndinguri na Nduta,” alisema Hasmukhu.
Dinta pamoja na mumewe Abhay Singh Pathanja anayeishi nchini Amerika pamoja na Ndinguri na Nduta wameshtakiwa kughushi Wosia wa Balkrishina kujigawia mali na kuwatapeli binti wengine wawili wa marehemu-Kalpa na Shilapa Prakesh Tajeru anayeishi London.
Hasmukh aliambia korti kwamba alishuhudia binti watatu wa marehemu wakigawanywa mali na kampuni ya mawakili ya Dally & Inamda mnamo Juni 19, 2019 jinsi baba yao alivyotaka.
Hasmukh alifichua kwamba ndugu yake-Balkrishna- alimwita katika Hospitali ya Aga Khan na kumweleza kwamba anataka kugawia bintize watatu mali zake kwa vile “siku zake za kuondoka ulimwenguni zimekaribia.”
Mahakama ilielezwa na Hasmukh kwamba ndugu yake aliungama hayo alipokuwa amelazwa Hospitali ya Aga Khan akiugua.
Mbali na Aga Khan alisema nduguye pia alikuwa amepelekwa nchini Uingereza kwa matibabu maalum.
“Baada ya ndugu yangu kufariki nilipokea simu kutoka kwa kampuni ya mawakili ya Dally & Inamdar kufungua Wosia wa Balkrishna agawe mali zake kwa watoto wake watatu- Kalpa, Dinta na Shilapa Paresh Tejura,” Hasmukh alimweleza hakimu mwandamizi Rose Ndombi.
Ndugu huyo wa marehemu alisema Shilapa hakuhudhuria hafla hiyo ya kusomwa kwa Wosia huo.
“Ndugu yangu aliwapa bintize pesa , maploti na makampuni kulingana na jinsi alivyokuwa ameandika katika Wosia wake,” alisema Hasmukh.
Alisema Kalpa alipewa kampuni ya Pelican Sign Limited inayoandika vibao kwenye barabara kuu humu nchini, nyumba mtaani Kileleshwsa na mashamba eneo la Limuru na pesa.
“Baada ya kusomwa kwa wosia huo kila mmoja alifurahi na hakuna mtu aliyeuliza swali. Wote waliridhika,” hakimu alifahamishwa.
Ndugu huyo wa Balkrishna alisema alishangaa baadaye kusikia madai kwamba Dinta aliwapora dada zake, mali waliyogawiwa na Balkrishna kwa kughushi sahihi ya baba yake na kuwasilisha katika mahakama kuu ya Milimani akidai yeye ndiye mmiliki wa Pelican Signs Limited.
Hasmukh alidokeza haya alipotoa ushahidi katika kesi aliyoshtakiwa Dinta, mumewe Abhay Singh Pathanja na waliokuwa wafanyakazi wenye vyeo vya juu katika kampuni yao ya Pelican- Samuel Ngugi Ndinguri na Addah Nduta Ndambuki ya kughushi Wosia wa Balkrishna Devani na kujipatia mali huku wakiwatapeli Kalpa na Shilapa.
Wanne hawa wamekana mashtaka manane ya kula njama kutenda uhalifu wa kughushi Wosia wa Balkshrina Devani.
Akitoa ushahidi, Kalpa alisema kwenye Wosia alioandika baba yake wakiwamo madaktari wawili wa Hospitali ya Aga Khan alipewa kampuni ya Pelican, Mashamba eneo la Limuru naye Dinta akapewa ploti karibu na uwanja wa Nyayo.
Dada ya Shilapa Paresh Tejura alipewa pesa zilizokuwa katika akaunti za I&M na Bank of Baroda na nyingine kwenye Benki mjini London anakoishi.
Kalpa alisema Dinta alighushi Wosia wa baba yao mwezi mmoja baada ya kuaga na kuwapora yeye na Shilapa.
Kalpa alisema cha kushangaza ni kwamba ushahidi ambao Dinta aliwasilisha katika kesi ya urithi inayoendelea Mahakama kuu ni kwamba “baba yao alitia sahihi stakabadhi za kumpa urithi mwezi mmoja baada ya kufa na kuzikwa kwake.”
Balkrishna aliaga Juni 4, 2019 na ushahidi Dinta aliowasilisha Mahakama kuu ulikuwa umetiwa sahihi na baba yao Julai 14, 2019.
“Swali linaloleta kizugumkuti ni- Je Baba alifufuka akatia sahihi stakabadhi za kuhamisha urithi kwa Dinta kisha akarudi kaburini?” Kalpa alishangaa kortini.
Mahakama ilielezwa bwanyenye Devani alikuwa mgonjwa kiasi kwamba “hangeweza kuendeleza shughuli za makampuni yake.”
Kesi inaendelea.