WAPO wengine wanyama, nyumbani hata porini,
Wale walo na unyama, wasoyala na majani,
Kesha fika kwa mapema, kututia matatani,
Nivusheni baharini, penye mamba wala nchi.
Keshawaona kitambo, wameasi ya adhimu,
Wamo kutupiga kumbo, na kusitiri ilimu,
Daima si haijambo, tumepoteza fahamu,
Nivusheni baharini, penye mamba wala nchi.
Wapo nchini hakika, wamepaka yao sura,
Wajulikana kihulka, walaji hongo ya chira,
Wasopenda ushirika, wenye nyoyo za ngawira,
Nivusheni baharini, penye mamba wala nchi.
Ya mgambo inalia, watoke wote vitini,
Wasije tena ingia, wale uchumi jamani,
Nchini tuje jutia, tukiwa sote wandani,
Nivusheni baharini, penye mamba wala nchi.
TONEY FRANCIS ONDELO
‘Malenga Mjali Siha’
Ndhiwa, Homa Bay
Ulevi wa madaraka
Nataka niwaambiye, vijana na wenye mvi,
Kuhusu kalunguyeye, wavilao vya mvuvi,
Ila chonde baadaye, nisijeitwa mgomvi,
Ulevi wa madaraka, huuzidi wa Konyagi.
Sio kila ayumbaye, endaye vile na hivi,
Basi ukadhani ndiye, mnywa maji ya kilevi,
Wengine ni ‘chama oye, viongo’ walo wajuvi,
Ulevi wa madaraka, huuzidi wa Konyagi.
Wengi wataniuliza, ni vipi hutambulika,
Hao wanotuongoza, kwa kulewa madaraka,
Kwa makini sikiliza, mambo wanayotamka,
Ndu’zangu! wa madaraka, huuzidi wa Konyagi.
Wapo wanojitokeza, wapate kutukuzika,
Raia hutupuuza, ngawa ndo tulowaweka,
Sifa zimepitiliza, mpaka zinamwagika,
Juweni wa madaraka, huuzidi wa Konyagi.
ELENZIAN JK
‘Kalamu Ndogo’
Dodoma, Tanzania
Ukimwi tai nyekundu
Kila lango waingia, nyondenyonde shida nyonda,
Afya yako kulemaa, nyingi wakati kitanda,
Kutuwacha meduwaa, mapenzi yalokushinda,
Ukimwi tai nyekundu, songoa yate maisha.
Komesha yako mahaba, malizia uchu wako,
Ni maisha yaloboba, malizia hamu yako,
Wosia mama na baba, ngumu kutimiza kwako,
Ukimwi tai nyekundu, songoa yetu maisha.
Kuwapa wengi mateso, nduguyo kutupa teke
Zikwa kwa sanda na leso, jeneza mavazi yake
Kililio kwetu Meso, kuukosa penzi lake,
Ukimwi tai nyekundu, songoa yetu maisha.
Unapaswa kumsali, kuna huru kwake Rabi,
Mpende wako kamili, si mwingine ila Robi,
Punguza yako batili, kijana bwana na bibi,
Ukimwi tai nyekundu, songoa yetu maisha.
LEXY SON BREVYN
‘Kiamboni Ustadh’
Nzoia Academy, Kitale
Maradhi ya saratani
Saratani ina hofu, jina tulisikiao,
Saratani linganifu, hauna dunia leo,
Saratani ni sumbufu, haijapata fumbuo,
Saratani ni tishio, yawakera wafumbuzi.
Saratani tatanishi, matabibu watibuo,
Saratani tetemeshi, waganga waganguao,
Saratani huzunishi, kote yazua vilio,
Saratani ni tishio, yawakera wafumbuzi.
Saratani kituoni, haitambui na cheo,
Saratani ni huzuni, walopita hadi vyuo,
Saratani duniani, yaogofya matukio,
Saratani ni tishio, yawakera wafumbuzi.
MAINAH ALFRED MAINAH,
‘Msanifu Makamula’
Mia Moja, Timau
Lala salama Mugisa
Utungo natanguliza, kusema yalo moyoni,
Tumebaki kwenye giza, ni machozi mashavuni,
Itabidi kujikaza, utabaki akilini,
Lala salama Dennis, taonana baadaye.
Twajishika vitwani, bado hatujaamini,
Uliishi spitalini, bila kupata afueni,
Tumebaki kwa huzuni, mtuweke maombini,
Lala salama Dennis, taonana baadaye.
Familia ya Mugisa, sisi sote tunalia,
Na kifo kimetutesa, twabaki tukishangaa,
Kwa hivyo itatupasa, tukubali kutulia,
Lala salama Dennis, taonana baadaye.
Dada wapwa kina kaka, tusiwe na hatihati,
Tuondoeni mashaka, Dennis tabaki hayati,
Na peponi atafika, ni wake huno wakati,
Lala salama Dennis, taonana baadaye.
LIONEL ASENA VIDONYI
‘Malenga Kitongojini’
Seeds High School, Kitale
Tuache kamari
Salamu ninazituma, mliko zipokeeni,
Baba na akina mama, na vijana mitaani,
Nataraji m salama, wazalendo vijijini,
Wosia wangu mmoja, tuache kamari bwana.
Tuiacheni kamari, inayo mengi madhara,
Twayajua sio siri, vijana imeburura,
Mbeleni kuna hatari, chukua hatua bora,
Wosia wangu mmoja, tuache kamari bwana.
Kamari yaua shule, kusoma sasa ni ngori,
Chuoni shakuwa ndwele, kubeti na kumi ngiri,
Kisota wanza kelele, kwa wazazi kuwaghuri,
Wosia wangu mmoja, tuache kamari bwana.
Kamari shakuwa tabu, uchumi inahujumu,
Akina bibi na babu, wamekwepa majukumu,
Wamepatwa uraibu, kubeti baba na mamu,
Wosia wangu mmoja, tuache kamari bwana.
GILBERT KINARA
‘Tabibu Mshairi’
Keumbu, Kisii
Toto hili binadamu
Tarumbeta ishalia, kwa madaha nasimama,
Neno niloazimia, kulilonga kwa ujima,
Sitetereki Rabia, tenami sitoatama,
Hili elewa wangwana, watoto pia nadamu.
Takiriri minatia, hili swala ainati,
Kila pembe shanyatia, kuisakanya kititi,
Vilio vya hayatia, vyanichoma kibuhuti,
Hili elewa wangwana, watoto pia nadamu.
Ni zawadi kwa karima, ipokewe kwa imani,
Malezi kwao lazima, siwatese hadharani,
Tele wanazo neema, ya muhimu tambueni,
Hili elewa wangwana, watoto pia nadamu.
Na huko kuwafanyisha, na ngumu kazi kuwapa,
Katakata nakatisha, wenu mchezo wa kapa,
Starehenu bashasha, kiama huwezi kwepa,
Hili elewa wangwana, watoto pia nadamu.
NATALIE SUMAYE
‘Malenga wa Kifyosu’
Namanga, Tanzania
Tunusuru Mola wetu
Ulimwengu uu huu, una mengi majaribu,
Kote pembe nne kuu, yafanyika ya ghadhabu,
Vifo vya wetu wakuu, na wadogo si ajabu,
Tunusuru Mola wetu, kifo cha tuangamiza.
Kila kupambazukapo, mmoja ametuacha,
Meenda asorudipo, huku tukilia kucha,
waja tutamaukapo, mwengine na si kuficha,
Tunusuru Mola wetu, kifo cha tuangamiza.
Itutokapo huzuni, kingora kinasikika,
Ametuacha jamani, mwanahabari sifika,
Tufanyeze abadani, na sisi tunapunguka?
Tunusuru Mola wetu, kifo cha tuangamiza.
Kifo upate sikio, wakighani usikie,
Kwa kweli chetu kilio, kina machungu kwambie,
Twalia kwa tegemeo, kwa Mungu tushikilie,
Tunusuru Mola wetu, kifo cha tuangamiza.
WANJOHI PETER
‘Kitunguu Machoni’
Wapishi bora
Jua jicho mefungua, sina budi kuamka,
Siku mpya mefikia, namshukuru Rabuka,
Ninataka kitumbua, nende jikoni kuoka,
Kama hakijaungua, ni mchanga meingia.
Kitumbua ni kimoja, na walaji ndio wengi,
Chahitaji ukionja, kiwe na utamu mwingi,
Hii ndio yangu hoja, kimebadilika rangi,
Kama hakijaungua, ni mchanga meingia.
Zimenifikia sifa, za vijana watukutu,
Kila siku kwao dhifa, wasema maisha yetu,
Wamekosa maarifa, hawapo mababu wetu,
Kama hakijaungua, ni mchanga meingia.
Wazazi nao nyumbani, wamekuwa dijitali,
Watoto hawathamani, wanakimbilia mali,
Tuzidukeni jamani, tuielewe hii hali,
Kama hakijaungua, ni mchanga meingia.
FAITH WERU,
Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret.
Ametuacha Njuguna
Mohamedi wa Njuguna, leo hii hayu nasi,
Ombi la kwake Rabbana, rohoye haikuasi,
Hayupo na sisi tena, katika kadamnasi,
Ametuacha Njuguna, kwa Mola katangulia!
Mohamedi wa Njuguna, namba leo hayu nasi,
Elewani waungwana, kamuitika Qudusi,
Daima hatutamwona, miongoni mwetu sisi,
Ilazwe pema peponi, roho ya bwana Njuguna!
Juzi juzi katuhama, kaitwa kenda kwa Mola,
Ulimwenguni waama, sote twasema Inshalah,
Mola amemtazama, Rabbana Muumba Allah,
Ameondoka Njuguna, hayu nasi ikhiwani!
Njuguna jama Njuguna, Mola wetu twakuomba,
Jinsi katwachia jina, roho katwaa Muumba,
Ukweli mwingi hatuna, tungaweza kumpamba,
Ghera nyoyo zinalia, Njuguna kutuondoka!
LUDOVICK MBOGHOLI
Al–Ustadh–Luqman
Ngariba Mlumbi (001)
Mitihani ni ya Rabuka
Mola naomba subira, kwa haya niyapitayo,
Niongoze yako dira, nipite uyatakayo,
Nijalize kwa kudura, nikubali yanijayo,
Mitihani tupitayo, niwe mwenyewe Qadiri.
Ayi leo nalilia, mwenzenu sinayo kazi,
Kuishi ninawazia, nitalani makaazi,
Hata chumba kulipia, talipani sina kazi,
Mitihani tupitayo, niwe mwenyewe Qadiri.
Ima dhiki kiingia, paa kwako huvujia,
Maji taka hupitia, puani unonusia,
Kufuru ukawazia, mbona wakakuzalia,
Mitihani tupitayo, niwe mwenyewe Qadiri.
Wakati ninakulia, niliona vyote vyema,
Mazuri nikawazia, kupata kiwa mzima,
Leo bwana nimekua, ‘tendawili kimekwama,
Mitihani tupitayo, niwe mwenyewe Qadiri.
RAMADHAN ABDALLAH SAVONGE
‘Malenga wa Nchi Kavu’
Kitui