USHAURI: Jinsi unavyoweza kukabili kero ya mawakala
Na SAMMY WAWERU
BW Muriuki Kamau amekuwa mkuzaji wa nyanya kwa zaidi ya miaka 20 na ni uwekezaji ambao umechangia pakubwa katika kumuinua kimaisha na kimaendeleo.
Alianza ukulima wa nyanya 1994 kwa mtaji wa Sh3,000 pekee. Alitangulia kwa robo ekari na kufikia sasa analima kiungo hicho cha mapishi katika karibu ekari 20.
Ili kufanya mzunguko wa mimea (crop rotation) eneo analovuna nyanya Bw Kamau hupanda maharagwe maalum ya Kifaransa, French beans. Mimea iliyoorodheshwa katika familia ya maharagwe husaidia kudumisha rutuba udongoni pamoja kuongeza Nitrojini.
Licha ya ufanisi aliopata mkulima huyu, safari haijakuwa rahisi. Wasemavyo wahenga na wahenguzi; hakuna safari isiyokosa milima na mabonde, Kamau anayefanya shughuli za kilimo kaunti ya Kirinyaga amekumbana na masaibu ya hapa na pale.
Mojawapo ni mabadiliko ya hali ya anga, ukame na athari za magonjwa. Mnamo 1998 alikadiria hasara ya nyanya zenye thamani ya Sh240, 000 na 2005 pigo lingine la zaidi ya Sh1.6 milioni kwa sababu ya changamoto hizo.
Anasimulia kuwa 2005 alipata jumla ya mazao ya Sh1,000 licha ya kuwekeza mamilioni ya pesa shambani. Ni pigo lililomlazimu kuuza lori lake ili kulipa madeni.
Mkulima huyo amewekeza pakubwa katika kilimo cha nyanya, ambapo ana jenereta mbili anazotumia kupampu maji na kukumbatia mfumo wa kunyunyizia mimea maji kwa mifereji.
Mto Thiba, ndio chanzo chake cha maji, mtaro ukielekezwa katika shamba lake.
“Suala la uhaba wa maji nililitatua kwa kununua jenereta ambapo hutumia Mto Thiba kukimu minyanya kiu cha maji,” asema.
Changamoto kuu na iliyosalia donda ndugu kufikia sasa ni kero ya kuwepo kwa mawakala. Nyanya ni miongoni mwa mazao yaliyovamiwa na wafanyabiashara hawa. Mengine yasiyosazwa na mawakala – wakichukuliwa kuwa daraja kati ya mkulima na soko ni viazi, mboga, karoti na matunda.
Kabla Bw Kamau akate kauli kuunda mtandao wa moja kwa moja sokoni, alikuwa amehangaishwa ajabu na mawakala. “Kreti ya kilo 130 wanaikarabati kukapia kilo 180, ilhali bei yao ni ile ya kuacha mkulima akiuguza majeraha ya gharama,” alalamika.
Ni muhimu kutaja kuwa mkulima ndiye mbeba gharama ya upanzi kuanzia matayarisho ya shamba, pembejeo kama mbolea, mbegu, dawa na leba. Mkulima huyo sasa huuza mazao yake katika masoko mbalimbali Nairobi.
Kuepuka mjeledi
Kulingana na Mwithukia Njenga kutoka e-Farmers Africa, shirika linaloleta pamoja wakulima kote nchini na Bara Afrika na kuwaunganisha na wateja kupitia mitandao, wakulima wataepuka mjeledi wa mawakala iwapo watafanya utafiti wa kutosha kabla kuvalia njuga kilimo.
Anaeleza kwamba utafiti unajumuisha mimea rahisi kukuza, gharama yake na soko.
“Akishajua anachotaka kukuza, ajisaili iwapo kina soko la haraka,” asema Bw Njenga.
Ni katika hilo na wakati mkulima anaendelea kutunza mimea yake anapaswa kutafuta soko, akiongozwa na wateja wake waliko na bei ya mazao. Njenga anasema kujiri kwa teknolojia na ambayo inaendelea kuimarika ni jukwaa rahisi kutafuta soko bila kujikuna kichwa.
“Mitandao ya kijamii hususan Facebook imerahisisha kupata wateja. Kuna makundi ya kijamii ya wakulima, mazao yakisalia wiki kadhaa kuvunwa ayapige picha na kuzipakia humo akitaja bei. Wanunuzi watamtafuta,” afafanua.
Wanunuzi haohao ndio watakuwa wateja wa siku zijazo ambapo anahimizwa kufungua kundi linalowaleta pamoja katika WhatsApp.
Hata hivyo, Njenga anashauri mkulima kuwa makini asiuze mazao yake bila kulipwa kwani katika mitandao hiyohiyo ndiko wahuni na matapeli wamekita kambi.