Ushindani mkali wa kibiashara wainua mji wa Mpeketoni
NA KALUME KAZUNGU
USHINDANI mkali unaoshuhudiwa wa kibiashara kwenye mji wa Mpeketoni, Kaunti ya Lamu umeinua pakubwa hadhi ya mji huo ambao kila kuchao unashuhudia maendeleo, kukua na kupanuka.
Mji wa Mpeketoni unaopatikana Lamu Magharibi ni wa pili kwa ukubwa kote Lamu baada ya Mji wa Kale upatikanao katika kisiwa cha Lamu.
Mpeketoni ilizinduliwa kama skimu miaka ya sabini (1970s) na mwanzilishi wa taifa hili, Mzee Jomo Kenyatta, ambapo eneo hilo lilikuwa ni la watu wachache tu.
Zaidi ya miaka 50 baadaye, Mpeketoni imegeuka na kuwa mji unaokua kwa kasi zaidi ikilinganishwa na miji mingine yoyote kote Lamu.
Hili linatokana na utiriri wa shughuli za biashara, kilimo, uchukuzi na maendeleo mengine mengi yanayoshuhudiwa kila upande mjini humo.
Miongoni mwa faida za ushindali mkali wa kibiashara ushuhudiwao mjini Mpeketoni ni kwamba kila mmoja anayejituma, iwe ni katika biashara au kilimo huelekeza sana nguvu zake katika kutoa huduma na bidhaa bora kwa wateja wake.
Ni kutokana na ushindani huo mkali ambapo wateja, wanunuzi au wakodishaji huduma mjini humo wameweza kukidhiwa vilivyo kimahitaji kwa kujali tabaka zote, iwe ni la juu, tabaka la wastani na hata lile la chini kabisa.
Kukua kwa mji wa Mpeketoni pia kumesaidia pakubwa kuwakutanisha watu mbalimbali, ambapo hupata fursa kujadili masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Ikumbukwe kuwa Mpeketoni ni kitambulisho tosha cha mji ambao ni makazi ya karibu makabila yote zaidi ya 40 nchini Kenya.
Ni dhahiri kwamba miaka ya sasa mji wa Mpeketoni umekua na kuvutia watu wa jamii tofautitofauti, kutangamana na kuishi pamoja na kufikia hadhi ya kuwa ‘cosmopolitan’.
Ni kutokana na hilo ambapo mji huo wa Mpeketoni umekuwa kiungo muhimu kisauti, hasa katika maamuzi yanayofungamana na siasa, si kwa kaunti ya Lamu pekee bali pia nchini.
Ni mjini Mpeketoni ambapo pia utapata biashara za hoteli, mikahawa na gesti zikinoga si haba.
Mbali na biashara, kilimo, iwe ni cha mahindi, maharagwe, pojo, korosho, nazi, pamba nakadhalika pia kimekuwa kikifanya vyema Mpeketoni.
Bidii ya wakazi wa eneo hilo katika kutekeleza ukulima imefanya eneo hilo kutambulika kuwa jungu kuu la ukuzaji na uvunaji wa chakula kinachotegemewa na wakazi wa kaunti nzima ya Lamu.
Ni mjini Mpeketoni ambapo wakulima pia wamekumbatia teknolojia za kisasa katika kutekeleza kilimo chao. Hapa, utawapata wakitumia matingatinga kutayarisha mashamba yao na kukuza mimea kwa njia ya kisasa. Hali ni hivyo katika kuvuna mazao shambani.
Wakulima pia wamekuwa wakitumia simu zao za mkononi kujitafutia soko la mitandaoni, kupokea fedha na kulipia huduma zingine nyingi.
Bw Joseph Mwangi Migwi, ambaye ni mkulima mashuhuri wa pamba eneo la Mpeketoni, anataja juhudi na kujitolea kwa watu wa eneo hilo katika kilimo na biashara kuwa hatua mwafaka inayoufanya mji huo kupanuka na kujizolea sifa za maendeleo kila kuchao.
“Hapa Mpeketoni sisi huwa hatushindani kwa ubaya. Twashindana kimaendeleo tu. Huyu akitekeleza hili kujiinua kimaisha, mwingine naye huwa yuko mbioni kutekeleza lile ilmuradi kila mmoja ajiinue kimaisha. Na ndio sababu mji wetu unakua kwa kasi ya kuridhisha,” akasema Bw Migwi.
Bi Susan Karanja naye anasema endapo utalaza damu, basi utajikuta wewe pekee ukiwa ndiwe uliyesalia nyuma, wakati wenzako walishasonga au kupiga hatua kubwa mbele.
“Mji wetu unafurahisha. Kila mmoja amejenga nyumba za kifahari, iwe ni za kibiashara au makazi. Vituo vya mafuta, mitambo ya kusaga, maduka ya jumla, vyote vinapatikana hapa. Watu wa hapa wamejituma vilivyo. Ukibaki nyuma shauri yako,” akasema Bi Karanja.
Licha ya mji wa Mpeketoni kushuhudia maendeleo na ukuaji wa kasi, hali hiyo hata hivyo haijaendelea kuwa nywee kwani baadhi ya watu kutoka sehemu mbalimbali wanaoingia na kuanzisha makazi mjini humo wamebeba vijitabia vyao ambavyo haviridhishi.
Hapa utawapata baadhi ya watu waliopotoka kimaadili, wakiwemo vijana wanaotumia dawa za kulevya.
Kuna wengine ambao wamekuwa wakiendeleza wizi au kupora watu usiku.
Kesi kadhaa za watu kuibiwa simu, pikipiki na fedha zimeripotiwa kwenye mitaa mbalimbali ya mji wa Mpeketoni, yote hayo yakihesabiwa kuwa miongoni mwa ‘hasara’ za ukuaji huo wa mji.
Isitoshe, wingi wa watu, hasa wale wenye ukwasi wa hela umesababisha mji wa Mpeketoni kuvamiwa na makahaba ambao hurandaranda usiku wakijitafutia riziki.
Kuvuma kwa maendeleo ya mji wa Mpeketoni pia kulichangia magaidi wa Al-Shabaab kutoka nchi jirani ya Somalia, mnamo Juni 15, 2014, kuulenga mji huo, kuushambulia, kuharibu mali na kuua wakazi.
Zaidi ya wakazi 90, wengi wao wakiwa ni wanaume, waliuawa kwa ama kuchinjwa au kupigwa risasi na kuteketezwa na Al-Shabaab kwa usiku mmoja.
Magari zaidi ya 40 na nyumba zaidi ya 30 pia ni miongoni mwa vilivyoteketezwa na magaidi hao kwa usiku huo huo mmoja.
Licha ya doa hilo jeusi kugubika Mpeketoni miaka 10 iliyopita, mji huo bado haujapoteza dira katika maendeleo yake kwani kwa sasa nyumba mpyampya tayari zimejengwa na watu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
“Twashukuru kwamba licha ya Al-Shabaab kuulenga mji wetu na kuuteketeza wakidhani wangeusambaratisha, sote tumeungana kuusimamisha upya mji huu. Yaani tumeushinda ugaidi. Hapa ni maendeleo tu,” akasema Bw Kamau Mbuthia, mkazi wa mtaa wa Umoja mjini humo.