Ustadh mpamba hotuba anayevutia Waislamu kwa Wakristo
NA KALUME KAZUNGU
WELEDI wa Ustadh Mohamed Shariff Mzee almaarufu ‘Tantawy’ katika kuyatunga na kuyaghani mashairi umemfanya kiongozi huyo wa kidini kupendwa na wengi.
Sifa za Ustadh Shariff katika kutumia kipaji chake cha ushairi kuzipamba na kuzinogesha hotuba misikitini zimeenea si tu katika kijiji chake cha Kizingitini, Lamu Mashariki, lakini pia kwa kaunti nzima ya Lamu na Pwani kwa ujumla.
Mara nyingine pia huenda ukampata Ustadh Shariff akiwa kibarazani au kishorobani, iwe ni kijijini Kizingitini au kwenye Mji wa Kale wa Lamu, akitoa mafundisho ya dini kwa waja, ila kwa wakati huo akitumia mfumo wa ushairi na wala si mbinu ya kawaida ya kutoa mahubiri au mawaidha ya dini kama wafanyavyo maimamu na maustadh wengine.
Bw Shariff, ambaye ni baba wa watoto tisa, alizaliwa katika kisiwa cha Kizingitini kilichoko Lamu Mashariki mwaka 1964.
Kwa sasa ana umri wa miaka 60.
Katika mahojiano na Taifa Leo Jumatano, Bw Shariff alisema yeye hupendelea sana kutoa wosia, hotuba au dar’sa mbalimbali misikitini akitumia mfumo wa ushairi anaoutaja kuwezesha hotuba kueleweka kwa urahisi zaidi huku pia akiburudisha kwa wakati mmoja.
Anafafanua kuwa maneno mengi, hasa yale ya Kiarabu yaliyoandikwa kwenye Qur’an huwa yako katika mfumo wa kishairi.
Anasema ni kupitia mbinu yake ya ushairi ambapo huzifanya hotuba za misikitini kufasirika na kueleweka vyema, hivyo kuwawezesha waumini wanaohudhuria maombi na mawaidha misikitini kuyakamata na kuyagandisha akilini bila kuwaponyoka.
“Mimi napenda mashairi tangu nikiwa mdogo. Nikiwa msikitini, mimi huitumia talanta yangu ya ushairi kutoa nasaha, mawaidha au hotuba na wengi wanapenda mtindo huo wangu. Hilo pekee limenifanya kuwavutia waumini wengi kufuatilia mafundisho yangu ninayotoa misikitini,” akasema Bw Shariff.
Anaongeza, “Maneno mengi ya Kiarabu huwa kwenye mfumo wa kishairi. Hilo linamaanisha kuwa ninapotumia mashairi basi mambo hufasirika na kueleweka vyema zaidi kuliko kunena tu.”
Kiongozi huyo wa dini ya Kiislamu anaamini kuwa ili neno, hasa lile la Kiarabu, liweze kufaulu kuwa neno sahihi na la kueleweka, basi lazima lifanyiwe rufaa kutoka sehemu tatu.
“Neno hilo lazima lichukue rufaa ya Qur’an, Hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W) au kutoka kwa mashairi ya Kiarabu. Na ndio sababu ninathamini sana mashairi katika hotuba zangu kama mbinu mojawapo ya ufafanuzi,” akasema Bw Shariff.
Anasisitiza kuwa mashairi hueleza mambo kwa uwazi, hivyo kuifanya lugha kupambika na kueleweka kwa uzuri na ufasaha zaidi.
Mbali na kuwa ustadh, Bw Shariff pia ni msomi, hasa wa masuala yanayofungamana na elimu ya dini ya Kiislamu.
Lakini kwa nini akabandikwa jina Tantawy ambalo kwa sasa ndilo linalofahamika au kuwika zaidi kushinda lile lake halisi?
Anaeleza kuwa jina ‘Tantawy’ alipewa na Msomi na Mwanachuoni mmoja kutoka Misri aliyefika Lamu kwa wakati mmoja ili kuwaelimisha kuhusu dini.
Bw Shariff anasema baada ya mwanachuoni huyo kustaajabu jinsi alivyokuwa mweledi wa kuisoma na kuichambua Kurani katika umri wake mdogo, hapo ndipo akaafikia kumtunuku jina Tantawy.
“Kwa sasa Tantawy ndilo jina lililokita mizizi eneo hili letu la Lamu kushinda lile langu halisi. Ukiulizia kumhusu Mohamed Shariff Mzee huenda ukamaliza siku nzima bila kumpata. Ila ukiulizia Tantawy, hata dakika moja ni nyingi, utaambiwa ni mimi,” akasema Bw Shariff.
Je, talanta yake ya ushairi chimbuko lake ni wapi?
Ustadh Shariff anakiri kuwa yeye alizaliwa katika familia ya watu wenye sifa za ushairi.
Anamtaja ami au amu yake na mwanamashairi au malenga tajika wa Lamu na Pwani, Sheikh Ahmad Msallam wa Kizingitini.
Anasema Sheikh Msallam ndiye aliyekuwa kichocheo kikuu cha yeye kuyapenda mashairi na kujitosa kwenye tasnia hiyo hadi kufikia alipo.
Sheikh Msallam alifariki mnamo Septemba 10, 2020.
Baadhi ya wakazi wa Lamu waliozungumza na Taifa Leo walimsifu Ustadh Shariff kwa kuwa ‘Mtu wa Watu.’
Kassim Shee, mkazi wa Kizingitini, anamtaja Ustadh Shariff Tantawy kuwa mcheshi na mpenda wote.
“Mimi hupendezwa sana na hotuba zinazoendeshwa misikitini na Ustadh Tantawy ambaye huzitekeleza kiushairishairi. Ni mcheshi na roho safi,” akasema Bw Shee.
Katika kisiwa cha Lamu, wanaomfahamu wanamtaja kuwa kiongozi mtaratibu wa dini ambaye huyafasiri mambo inavyostahili na katika njia isiyoboesha.
“Utasinzia vipi wakati Ustadh Shariff Tantawy akitoa wosia misikitini kwa njia ya ushairi? Mimi hufuatilia darsa zake karibu zote bila kusinzia. Mbinu yake ya ushairi inakuburudisha, kukutumbuiza na kukuweka ange muda wote,” akasema Bw Khamis Ali.
Baadhi ya wale wasiokuwa waumini ya dini ya Kiislamu pia walimtaja Bw Shariff kuwa mpenda dini zote na asiyekuwa na ubaguzi.
“Yeye hutangamana na wote mabarazani na vichochoroni. Anapokuona hakubagui bali yuko tayari mshirikiane kuchambua masuala ya kidini wakati akikutumbuiza kwa mashairi,” akasema Bw Simon Charo, mkazi wa kisiwa cha Lamu ambaye ni Mkristo.
Bw Shariff ni mzawa wa sita katika familia ya watoto 20.
Alisomea Shule ya Msingi ya Kizingitini, Lamu Mashariki kabla ya kujitosa kwenye masuala ya elimu ya dini ya Kiislamu.