USWAHILINI: Fahamu kwa kina na uketo mihimili ya Jando na Unyago
Na HAWA ALI
KWA mujibu wa desturi na utamaduni Uswahilini, huaminika kuwa ili binti awe na heshima na kutambuliwa kuwa mtu mzima ni lazima apitie unyagoni.
Japo siku hizi hauthaminiwi sana, unyago kwa watoto wa kike hapo zamani ulizingatia kupevuka (kuvunja ungo) kwa binti.
Binti anapovunja ungo ndipo mama humtaarifu mume wake hali ya binti yao nao huandaa ngoma ya kumuingiza ukubwani kwa kumfundisha majukumu ya kiutu uzima na hasa yanayohusu familia. Ngoma hii huitwa Msondo. Fundi/Mwalimu anayehusika katika utoaji mafundisho haya huitwa Kungwi na yule anayefundishwa huitwa Mwali.
Kwa ufupi, katika mila za Uswahilini, watoto wa kike walifundishwa ili kumruhusu binti awe tayari kuolewa.Hata hivyo, kwa sasa mafunzo haya hayatolewi punde mabinti wavunjapo ungo kwa sababu wengi huwa bado ni watoto wa shule.
Michezo ya mabinti katika unyago ni sehemu ya mazoezi ya kumfanya binti awe na ujasiri kwa kuwa tayari kujaribu kupambana na changamoto mbalimbali katika mazingira yake.
Hapo zamani, hatua ya kutapisha binti hufuata baada ya shughuli ya mafunzo kwa siku 5; siku ya 6 hutapishwa na siku ya 7 ndipo hutolewa wakiwa tayari wamepokea mafunzo kamili.
Zoezi la kutapisha binti wakati wa unyago hufanyika kwa kuchanganya dawa za asili na maji na kisha kupewa wanywe kabla ya kutapishwa.
Hii dawa hutumiwa kama kiapo cha kutunza siri kwa yale yaliyojiri wakati wa unyago na hata wakiwa katika jamii zao.
Jando
Watoto wa kiume hupitishwa katika desturi iitwayo jando. Jando kwa watoto wa kiume ni kipindi cha zamani kilichozingatia kupevuka kwa wavulana wanaopelekwa tohara. Kwa neno jingine Uswahilini, jando pia huitwa itani.
Fundi/Mwalimu wa jando huitwa ngariba.
Vijana wanaopelekwa kwa tohara/jando baada ya siku 3-4 huanza mafunzo ya ukakamavu na ujasiri huku wakiwa bado na maumivu ya tohara.
Katika mafunzo yao, wavulana hawa hufundishwa nyimbo mbalimbali za kutafsiriwa na yule anayefundisha.
Mtoa mafunzo baada ya tohara huitwa mikanga. Huyu ndiye huwa na jukumu la kumuadibisha mvulana aliyeonekana mtovu wa nidhamu kabla ya kufanyiwa tohara. Pia mikanga/Nikanga hufundisha maadili ya jamii na kuwakaribisha vijana katika majukumu ya kiutu-uzima.
Katika jando, vijana waliotahiriwa hupewa mafunzo ya kuwajengea hali ya kujiamini na kujitambua kama watu wazima.
Jamii nyingi za Uswahilini tangu karne ya 18 zilikuwa waumini wa dini mbalimbali, na hivyo lengo kuu la kufanya tohara lilikuwa kuwafanyia usafi na kuwatambua kama watu wanaoweza kushiriki katika maamuzi na maendeleo katika jamii.