Makala

‘Utamu wa safari ya baharini ni abiria kujazana kwa jahazi’

March 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

JE, kuna madhara gani kwa abiria na mizigo kujazana kwa vyombo vya usafiri wa majini?

Utapata makumi ya abiria, mifugo, ikiwemo punda na kondoo, magunia ya viazi, maboksi ya unga wa mahindi na ngano, kuni, na fanicha, vyote vikiwa vimebebwa kwenye jahazi moja kubwa kutoka kisiwa cha Lamu au jeti ya Mokowe kuelekea visiwa vya Mtangawanda, Pate, Mkokoni, Faza, Kizingitini, Kiwayu, Ndau na kwingineko.

Mojawapo ya sheria muhimu za usalama wa usafiri nchini, iwe ni kupitia vyombo vya uchukuzi wa barabarani, baharini au angani ni kwamba katu usijaze au kubeba abiria kupita kiasi.

Ila kwa wakazi wengi wa Lamu wanaotumia uchukuzi wa baharini wakitumia ama mashua, maboti, majahazi au ngalawa wao mara nyingi husema heri kuwa pamoja kufaana safari.

Aghalabu utasikia baharia wa Lamu akinena ‘utamu wa safari, hasa ile ndefu ya baharini ni abiria kujazana kwa jahazi.’

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa mashua na majahazi hasa yale makubwamakubwa yanayosafirisha abiria mwendo wa masafa marefu baharini, yamekuwa yakibeba abiria wengi na mizigo bila kujali hatari inayowakodolea macho.

Sababu zinazowasukuma wasafiri wa baharini Lamu kupendelea kusafiri wakiwa makundi makundi ni zipi?.

Bw Ahmed Yusuf, mkazi wa Faza, anasema usafari kwa kutumia vyombo vya baharini huwa ni wa upweke mno, hasa endapo utahusisha mwendo mrefu.

Anasema badala ya baharia kusafiri kwa boti au mashua akiwa pweke, mara nyingi wao hupendelea sana kukusanyana kabla ya kujazana na kuondoka wakisafiri kutumia chombo kimoja.

“Kusafiri mkiwa wengi ni raha. Watu hawaboeki chomboni. Hata safari iwe ndefu namna gani, tukisafiri makundi makundi tutapiga gumzo kupisha wakati ilmuradi tufike salama tuendako. Gumzo zetu ndizo zinasaidia kufupisha safari. Ukijitosa gumzoni wakati ukisafiri utafanya kushtukia umewasili bandarini bila kuboeka,” akasema Bw Yusuf.

Maryam Lali, mkazi wa kisiwa cha Lamu, anaeleza kuwa kusafiri mkiwa wengi chomboni pia kunapunguza au kuondoa kabisa uoga miongoni mwa wasafiri.

Anasema kwa sababu umoja ni nguvu, kila msafiri anapomtazama na kupiga gumzo na mwenzake chomboni huwa anazidi kupata nguvu mpya na kuwa jasiri hata kama wahusika wako katikati ya bahari ya kina kirefu.

Mashua yakiwa yamejaa abiria na mizigo yapita karibu na kivuko ca Mkanda kuelekea kisiwa cha Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anaweka paruwanja siri ya kusafiri mkiwa wengi chomboni kwamba huwa wenye kutiana moyo.

“Hata kuwe na tufani na mawimbi makali namna gani baharini hadi kiasi cha kutingisha chombo, sote tukiangaliana kwa macho na kushikana   mikono tunatorosha uoga nafsini mwetu. Ukisafiri peke yako utagubikwa na fikra nyingi, hivyo kujikunyata kwa uoga pembeni mwa mashua. Hali hiyo inaweza kukufanya kuona au kuhisi kana kwamba safari haisongi,” akasema Bi Lali.

Wakazi wa Lamu wanasema usafiri wa wengi mashuani una manufaa tele, hasa kwa akina mama wenye watoto zaidi ya mmoja.

“Ukiwa una watoto kadhaa usioweza kuwapakata wakati ukisafiri, wasafiri wenzako botini au mashuani huingilia kati na hukusaidia kuwabeba watoto hao hadi kufika kule mnakoelekea. Hicho ni kinyume kabisa na wakati ukisafiri peke yako ambapo utahangaika na wana wako,” akasema Bi Nuru Athman.

Bw Hassan Farid naye anataja umuhimu wa kusafiri mkiwa wengi mashuani kwamba kunawapa mwanya au fursa ya kutangamana na kutagusana na watu wa tabaka zote, hivyo kujenga umoja wa kijamii na hata kitaifa.

Wakazi wakisafiri kwa mashua kutoka kisiwa cha Mtanawanda kuelekea kisiwa ca Lamu. Mabaharia Lamu wanasema ‘Utamu wa safari ya baharini ni kujazana kwa mashua’. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema mbali na kujenga umoja, mnaposafiri mkiwa wengi na mkiwa mnatoka au kuelekea visiwa mbalimbali vya Lamu kunawawezesha kutaarifiana yaliyoko na yanayojiri kwenye visiwa hivyo.

Lamu ina zaidi ya visiwa 35 ambavyo vimegawanywagawanywa na Bahari Hindi.

“Hebu piga hii picha, kwamba mkazi wa kisiwa cha Pate anaingia na kusafiri kwa mashua moja na mwenzake wa Kizingitini au Faza. Hapa wanapashana kila mmoja yaliyojiri kwao. Yaani kusafiri pamoja au tukiwa wengi kunatusaidia kufahamishana habari za tutokako na tunakoelekea,” akasema Bw Farid.

Licha ya manufaa na furaha wapatayo wakazi wa Lamu wakati wakisafiri botini au mashuani wakiwa wengi, pia ifahamike kwamba karaha ipo.

Mkurugenzi wa Idara ya Majanga ya Dharura na Uokozi wa serikali ya Kaunti ya Lamu, Shee Kupi, anasema kuna hatari kubwa wakati unaposafiri kwenye mashua au boti iliyobeba abiria kupita kiasi.

Bw Kupi anasema mara nyingi mashua yaliyojaa abiria kupita kiasi ikitrokea ajali baharini, wahasiriwa au maafa huwa mengi.

Anashauri wasafiri kuheshimu sheria zinazofungamana na usalama wakati wanaposafiri ili kuepuka ajali na maafa.

“Lazima tuwe makini tunaposafiri. Ni heri mashua ukiiona yamejaa uache usubiri chombo kingine kuliko kujilazimisha kuingia ndani na kisha kuishia kuangamia endapo ajali itatokea. Punde abiria mnapozidi idadi ya wafaao kusafiri botini au mashuani hilo linamaanisha hata jaketi-okozi hamvai. Hicho ni kinyume kabisa cha sheria za uchukuzi wa majini,” akasema Bw Kupi.