Utapiamlo wapungua Turkana baada ya jamii kukumbatia kilimo – Ripoti
WAKAZI 800 kutoka eneo la Turkwel Loima na Naoros, Kaunti ya Turkana wameungana kufanya kilimo kwenye shamba lenye zaidi ya ekari 758 ili kukabili njaa na kupata lishe bora kwa watoto wao na familia kwa ushirikiano na Shirika la msaada kutoka Amerika, USAID kupitia mradi wa ‘Nawiri’.
Jamii hiyo ambayo inafahamika kwa wafugaji wa mifugo, ilihofia kutumia ardhi hiyo ambayo ilikuwa msitu uliokuwa hifadhi ya majoka hatari.
Bw Etoot Ekupurat, alisema kando na ardhi hiyo kugeuka kuwa msitu ambao uliwatia hofu wapita njia, pia ilizingirwa na miti aina ya Mathenge ambayo hunyima mkulima mavuno bora.
Alisema juhudi za shirika hilo liliwasaidia kufyeka kichaka hicho na kuwapa mbegu za kupanda aina mbalimbali ya vyakula.
“Hili shamba lilikuwa msitu ambao haukuwa unapitika. Tulikuwa tunaogopa kutokana na majoka marefu marefu ambayo yalikuwa yakiishi hapo. Wakati ‘Nawiri’ ilianza hivi, ilianza kufyeka ndio ulikuwa mwanzo wetu kulima,” alisema Bw Ekupurat.
Mkulima Peter Enayae, alisema kuwa shamba hilo limekuwa ni sehemu ya pili kwa kutumia ekari 390.
Wakulima hao ambao ni miongoni mwa wakazi walipoteza mifungo kutokana na ukame na vita vya kijamii. Sasa hivi wakinufaika kuwa hata wafugaji wa kuku.
“Tumepanda mashamba mengi na kuna yale ambayo bado kwa sababu bado kuna visiki kiasi. Ndio tunapambana kuhakikisha kuwa tumelima ipasavyo,” alisema Bw Enayae.
Mradi huo, umewawezesha wakazi hao kupata fursa ya kuelimisha watoto wao kwa kuuza mavuno hayo pamoja na kushiriki vyama vya kuchangiana.
Bi Hellen Lookoli alisema kama wanawake, hushiriki kuuza ndengu, maharagwe na matunda kama njia ya kupata pesa.
Kilimo hicho kimewapa matumaini ya kulinda wanyama wao pamoja na kuongeza kiwango cha maziwa.
Hapa kwetu watoto walikuwa wanaumia lakini kwa sasa angalia afya ya watoto, kila mtoto amenenepa. Jamii yetu iko sawa. Tunavyozungumza, wakulima katika eneo hili wameweza kuvuna na pia wanapanga kupanda.
Mkurugenzi wa USAID Nawiri Bw Gabriel Ekuwam, alithibitisha kuwa kesi 183 za utapiamlo zilizoripotiwa Januari 2o24, zimepungua kufikia Desemba 2024, kuripoti kesi 39.
“Kati ya kesi 183, 166 zilikuwa za utapiamlo wa wastani na 17 zilikuwa utapiamlo mbaya sana. Kufikia Deemba, kesi 36 zilikuwa za wastani huku tatu zikiwa mbaya,” alisema Bw Ekuwam.
Kiwango cha utapiamlo miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano huko Naoros, Kaunti Ndogo ya Turkana ya Kati, kikionekana kupungua kwa kiasi kikubwa kutokana ushirikiano kati ya serikali na washirika, ikiwa ni pamoja na USAID Nawiri.
Takwimu kutoka kwa Idara ya Afya ya Kaunti hiyo, zahanati ya Naoros ilionyesha kurekodi visa vya utapiamlo miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano vilipungua kwa asilimi 42 kati ya Januari 2024 na Desemba 2024.